Watu milioni 40 wanakabiliwa na njaa Afrika

Muktasari:

  • Mwanamfalme Rahim Aga Khan ambaye ni kiongozi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) amesema karibia watu milioni 40 barani Afrika wanakabiliwa na tatizo la njaa linalosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Nairobi. Mwanamfalme Rahim Aga Khan ambaye ni kiongozi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) amesema karibia watu milioni 40 barani Afrika wanakabiliwa na tatizo la njaa linalosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Rahim amesema hayo, leo Alhamisi Desemba 8, 2022 akizungumza kwa njia ya mtandao kwenye tamasha la Kusi lililoandaliwa na Kampuni ya Nation Media Group (NMG), Nairobi nchini Kenya.


“Hadi sasa karibia watu milioni 40 ndani ya bara la Afrika wanakadiriwa na njaa inayosababishwa na ukame,” amesema


Aidha, Rahim amesema matatizo mengi yanayolikumba bara la Afrika yanasababishwa na mabadiliko ya tabianchi hivyo tamasha hilo litumike kuleta suluhu ya changamoto hizo.


“Bara la Afrika linakumbana na matatizo mbalimbali yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama vile; mafuriko, ukame na ukosefu wa chakula,” amesema.


Rahim ambaye pia anaongoza Kamati ya Mazingira na Hali ya Hewa ya AKDN, ameipongeza NMG kwa kuanzisha mijadala yenye tija kwa bara la Afrika.


“NMG inaonyesha mwanga wa uongozi kwa kuchochea mijadala yenye misingi ya kiuanamajumui ili iweze kutatua changamoto za Afrika,” amesema.


 “Kila siku joto Afrika linaongezeka haya ni madhira ya mabadiliko ya tabianchi ambayo bara la Afrika lina mchango mdogo sana kwenye kusabisha athari hizi. Tamasha hili litasaidia katika kupata suluhu ya matatizo ya mabadiliko ya tabianchi na yatatekelezwa,” ameongeza.


Rahim amesema kwa upande wao, AKDN wanaendelea kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwenye nchi 14 ambazo taasisi yao imefika barani Afrika.


Tamasha hilo lenye kaulimbiu inayosema “Mabadiliko ya Tabianchi: Kuchunguza Majibu na Suluhu za Kiafrika” pia limehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango kwa njia ya mtandao.