Watumiaji dawa za nguvu za kiume mambo safi -VIDEO

Msajili wa Baraza la Tiba za Asili na Mbadala, Dk Ruth Suza 

Muktasari:

  • Ujana ni dawa inayotibu nguvu za kiume ambapo leo Machi 13, 2018 Serikali imetangaza kuitambua

Dar es Salaam. Serikali imetangaza rasmi kuzitambua dawa tano zilizotengenezwa kiasili baada ya kuzikagua ikiwemo 'Ujana' inayotibu nguvu za kiume.

Dawa hizo zimetangazwa leo Jumanne Machi 13, 2018 na Msajili wa Baraza la Tiba za Asili na Mbadala, Dk Ruth Suza katika mkutano na waandishi wa habari.

Amezitaja dawa hizo kuwa ni Ujana, IH Moon, Coloidal Silver, Sudhi na Vatari zinazotibu magonjwa mbalimbali.

Dk Suza amesema walikitumia kitengo cha Boring cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupitia Mkemia Mkuu wa Serikali.

Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Naibu Waziri wa Afya Dk Faustine Ndugulile ametoa agizo kwa waganga wote wa tiba asili na tiba mbadala kuacha mara moja kutoa matangazo yao mbalimbali kupitia vyombo vya habari na mabango ya barabarani.

"Nawataka waganga wote kujiepusha na matangazo yanayokinzana na sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kuondoa mabango yaliyozagaa mitaani yanayoonyesha kuwa wanaweza kutibu na kuponya magonjwa mbalimbali kama Ukimwi na matangazo mengine," amesema.

Aidha Dk Ndugulile amekemea wale wote wenye mashine aina za 'Quantum' kuacha mara moja kuzitumia kwa kuwadanganya wananchi kuwa zinaondoa sumu mwilini.