Watumishi 40 kukatwa mishahara upotevu wa Sh213 milioni

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel ameagiza watumishi zaidi ya 40 wa Halmashauri ya Sengerema kukatwa mishahara kutokana na taarifa kuonyesha kuwa hawakupeleka benki mapato ya Sh213 milioni.


Sengerema. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel ameagiza watumishi zaidi ya 40 wa Halmashauri ya Sengerema kukatwa mishahara kutokana na taarifa kuonyesha kuwa hawakupeleka benki mapato ya Sh213 milioni.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 24, 2022 kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Sengerema kilichokuwa kinajadili hoja za ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Amesema CAG kwenye ripoti yake amebaini watumishi hao na wakusanya mapato  hawajachukuliwa hatua yoyote ya kisheria ikiwemo kuripoti kwenye vyombo vya uchunguzi.

Miongoni wa watumishi hao ni watendaji  kata na mawakala waliotolewa maelekezo na Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya siku moja wilayani Sengerema Mei 7, 2022 na kuagiza hadi Julai 7,2022  wawe wamelipa fedha hizo.

Halmashauri ya Sengerema na Buchosa ni miongoni mwa halmashauri nane zinazounda Mkoa wa Mwanza ambapo kwenye ripoti ya CAG imebaini fedha nyingi hazipekekwi benki huku mashine za kukusanyia mapato zikionyesha fedha hizo zimekusanywa.

" Kuanzia sasa wakatwe mishahara yao ili fedha hizo zilipwe ndipo hatua nyingine zichukuliwe," amesema Gabriel.

Diwani wa Igalula, Faustine Shibiliti amesema Serikali inatakiwa kutafuta dawa ya kuwadhibiti watumishi wanaofuja fedha za umma kinyume na utaratibu.

"Watumishi hawa wanatakiwa kuwajibishwa ili iwe fundusho kwa wengine, waone kutafuna fedha za umma  ni kosa," amesema Shibiliti.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga ameahidi kushughurikia suala hilo hadi fedha hizo zipatikane.