Watumishi Buchosa watakiwa kuchangamkia chanjo ya Uviko 19

Watumishi Buchosa watakiwa kuchangamkia chanjo ya Uviko 19

Muktasari:

  •  Watumishi wa Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wametakiwa kujitathimini na  kujitokeza kuchanja chanjo ya Uviko 19 ambayo inasuasua


Buchosa. Watumishi wa Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wametakiwa kujitathimini na  kujitokeza kuchanja chanjo ya Uviko 19 ambayo inasuasua

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa Bruno Sangwa, kwenye kikao kazi kilichowashirikisha  wakuu wa shule za Sekondari 23 zilizoko kwenye Halmashauri hiyo.

Amewataka walimu wakuu  kuonyesha mfano kwa walimu wengine kwa kuchanja chanjo hiyo inayotolewa na Serikali bila malipo.

Sangwa amesema Halmashauri ya Buchosa imekuwa nyuma kwa watumishi wa kada  zote kwa kuchanja chanjo ya Uviko 19 licha wao kuhamasisha wananchi kuchanja.

"Ninawakata nyie mkatoe mfano kwa walimu wenu mnaowaongoza mkajitokeze kuchanja  chanjo ya Uviko 19 muwe mfano  na wengine wawafuate "amesema Sangwa.

Mkuu wa shule ya Sekondari Kome Dunia Luhula amesema maelekezo yaliyotolewa na viongozi wao watayafanyia kazi na kuhamasisha walimu wengine wajitokeze kupata chanjo hiyo.

Mmoja wa wakazi wa kata ya Nyehunge Anastazia John amesema Mwitiko mdogo wa jamii kuchanja chanjo ya Uviko 19 unatokana  na watu kutokupata elimu ya kutosha juu ya chanjo hiyo hasa kwa jamii ya vijijini ikiamini kuwa chanjo hiyo huenda inamadhara.