Watumishi wa umma wapya watakiwa kutunza siri

Kaimu katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Donald Bombo akizungumza wakati wa mafunzo kwa waajiliwa wapya katika vituo vya huduma za Afya mikoa ya Mbeya, Katavi, Songwe na Rukwa yaliyofanyika leo jijini Mbeya.

Muktasari:

  • Ajira hizo 324 ni za mwaka mmoja ambapo watahudumu katika vituo vya huduma za afya kwa Mikoa ya Mbeya, Rukwa, Katavi na Songwe kupitia taasisi ya Mkapa Foundation wakishirikiana na HJFMRI na serikali.

Mbeya. Waajiriwa wapya katika vituo vya huduma za afya katika Mikoa ya Mbeya, Katavi, Rukwa na Songwe wametakiwa kuzingatia taratibu za utumishi wa umma ikiwamo kutunza siri na kutokuwa chanzo cha migogoro kwenye maeneo ya kazi.

Hayo yamesemwa leo Septemba 26 na kaimu katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Donald Bombo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waajiriwa hao wa kada tatu tofauti ikiwa ni Tehama, masjala na watathimini na ufuatiliaji yaliyofanyika jijini hapa.

Bombo amesema watumishi hao lazima wazingatie sheria na taratibu za utumishi wa umma hususani kutotoa siri, kuwa na mawasiliano na uhusiano pamoja na kuzingatia uvaaji wa stara kwenye maeneo ya kazi.

Ameongeza kuwa wawapo kazini wajiepushe na migogoro badala yake waondoe vikwazo ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa na wananchi katika vituo vya afya.

“Nimeambiwa ajira zenu ni za mwaka mmoja, mkiwa kazini kuweni na vifua vya kutunza siri, jiepusheni na migogoro, pimeni taarifa kabla ya kuzisambaza, jitofautishe na wengine,” amesema,

“Sisi serikali tunaamini tumepata watu kwani waliotuma maombi walikuwa wengi ila mmechaguliwa nyinyi hivyo kuwani mabalozi wa kutatua changamoto na siyo vinginevyo,” amesema Bombo.

Ofisa mradi mwandamizi Taasisi ya Mkapa Foundation, Rasilimali Watu Afya, Violeth Mlay amesema waajiriwa hao wamepatikana kupitia ajira zilizotangazwa kupitia taasisi hiyo kwa kushirikiana watekelezaji wenza, Taasisi ya HJFMRI kwa kushirikiana na serikali.

Amesema jumla ya waombaji 7,716 walituma maombi, Mkapa Foundation ambapo utaratibu wa usahili ulifuatwa kwa ukaribu na serikali kwa kushirikiana na HJFMRI ili kupata watumishi 324 kwa ajili ya Mikoa Mbeya, Rukwa, Katavi na Songwe.

“Mbeya watakuwa 152, Rukwa na Songwe 61 kila Mkoa na Katavi ni 52, matarajio yetu ni kuboresha huduma za Ukimwi kwa wananchi katika vituo vyote vya afya ikiwamo zahanati na hospitali,” amesema Violeth.

Jane Mwasumbi ambaye ni mtathimini na mnufaika wa ajira hiyo, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na kuwa mara ya kwanza kuwa kwenye utumishi wa umma.

“Lazima tuzingatia maelekezo ya mafunzo haya, wengi ni wageni katika utumishi hivyo itatusaidia kuzingatia maadili ya kazi ikiwamo uwajibikaji, umakini na kulinda nidhamu,” amesema Jane.

Renatus Kayage amesema maelekezo waliyopewa na viongozi watayazingatia kuhakikisha wanatumia mwaka mmoja wa ajira hiyo kuwanufaisha wananchi ambao ndio walengwa kwenye kupata huduma.

“Wamesisitiza mawasiliano, siri za ofisi na uweledi lazima tuishi humo kuhakikisha tunatumia mwaka mmoja wa kazi yetu kuwa mabalozi kuwahudumia wananchi,” amesema Kayage.