Wauawa kwa mapanga wakisuluhisha ugomvi wa ndugu

Wauawa kwa mapanga wakisuluhisha ugomvi wa ndugu

Muktasari:

  • Watu wawili wa kijiji cha Itunduma kilichopo Kata ya Mtwango mkoani Njombe, wameuawa kikatili baada ya kwenda kwa jirani yao kusuluhisha ugomvi.

Njombe. Watu wawili wa kijiji cha Itunduma kilichopo Kata ya Mtwango mkoani Njombe, wameuawa kikatili baada ya kwenda kwa jirani yao kusuluhisha ugomvi.

Akizungumza kwa simu leo Septemba 12, Mwenyekiti wa kijiji cha Itunduma, Mikson Nyagawa amewataja watu hao kuwa ni Lorence Mhema (60) na Tulizo Nyagawa (32) alipozungumza na Mwananchi kuelezea tukio hilo la mauaji lililotokea kijijini hapo.

Amesema ilikuwa Septemba 8 mwaka huu saa 3 usiku, ambapo alipigiwa simu na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho kuwa kuna watu wanapigana kitongoji cha Nyamagala.

Amesema baada ya kumuuliza ilionekana kuwa anayeleta fujo ni mtuhumiwa, Thomas Mhema akijaribu kufanya fujo kwa kupigana na wananchi pamoja na mama yake mzazi aliyefahamika kwa jina maarufu Supagombolwe.

Amesema baada ya muda kidogo alipokea taarifa kutoka kwa mtendaji huyo kuwa yametokea mauaji ndipo alipomwambia watafute gari ili kujiridhisha juu ya tukio hilo.

"Tulipofika pale kweli tulikuta watu wale wamekatwa katwa na mapanga na wameshafariki," alisema Nyagawa.

Amesema chanzo cha ugomvi huo inasemekana kuwa ni ushirikina ambapo kijana huyo alikuwa anamtuhumu kuwa mama yake mzazi na baba yake mzazi kuwa wanamroga baada ya kwenda kwa mganga wa kienyeji.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Hamisi Issah alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, akisema marehemu walikwenda kuamulia ugomvi wa wanandugu.

Alisema marehemu hao kabla ya kukutwa na umauti walisikia kelele ambazo ziliashiria kutaka msaada kutoka nyumba ya jirani ndipo walipoamua kwenda ili kusuluhisha ugomvi huo.

Amesema watu hao wameuawa kwa kukatwakatwa na mapanga na mtuhumiwa huyo baada ya kufika eneo hilo ambalo kulikuwa na mgogoro.

"Kuna bwana mmoja alikwenda kufanya mauaji lakini aliyemkusudia akapiga kelele watu wakaja kulichotokea watu wa jinsia ya kiume walivyosogea walikatwa mapanga," alisema Issah.

Alisema mauaji mengi ambayo yamekuwa yakitokea mkoani Njombe yanahusisha familia, ambapo amezitaka familia kuacha tabia hiyo isiyofaa kwenye jamii.
Amewataka wazazi kuwalea watoto katika maadili mema ikiwa ni pamoja na kuwapeleka nyumba za ibada ili kujifunza makatazo ya mungu na amri zake.

"Wananchi wasikate tamaa kama kuna mwenzao anahitaji msaada waende tu huyu ni mtu amefanya taiminingi amewaua Hawa," amesema Issah.