Wauza nyama Mpanda wadaiwa kutumia sumu kuua nzi buchani

Baadhi ya wachinjaji nyama wakiendelea na shughuli za uchinjaji eneo la machinjioni ililopo Mpanda kabla ya bidhaa hiyo haijapelekwa buchani. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

Baadhi ya wafanyabiashara wa bucha za nyama Manispaa ya Mpanda wamedaiwa kutumia dawa zenye sumu kuua nzi buchani hali inayodaiwa kuwa hatari kwa afya za walaji.

Katavi. Baadhi ya wafanyabiashara wa bucha za nyama Manispaa ya Mpanda wamedaiwa kutumia dawa zenye sumu kuua nzi buchani hali inayodaiwa kuwa hatari kwa afya za walaji.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 9, 2022 Ofisa Mifugo Mkoa wa Katavi, Zediel Mhando amesema wamebaini kuwepo tatizo hilo akilaani tabia hiyo.

Amesema kufuatia kuwepo tatizo hilo wameamua kutoa elimu kwa wafanyabiashara wote wa nyama wazifahamu sheria na taratibu ikiwamo kukata leseni.

“Wapo wafanyabiashara kwenye miundombinu yao tumebaini mapungufu mengi sana, uhifadhi mbovu wa nyama, wanahifadhi kwa kuchanganya na nyama iliyooza kwenye friza,”amesema Mhando akaongeza.

“Hii ni changamoto kubwa sana au anaendelea kuuza nyama iliyooza kisheria hairuhusiwi lazima tulinde afya za walaji, kitu kingine ni matumizi ya sumu,”

Ameongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara hao wanatumia sumu kali kuua nzi kwenye bucha zao ikiwamo kupuliza dawa ya mbu aina ya rungu akidai kuwa wahusika watachukulia hatua za kisheria.

“Bucha zao zitafungwa lakini mabucha karibia yote tuliyopita hayana leseni ni tatizo kubwa, lazima wawe na leseni, wasajiliwe na wafuate taratibu zinazoelekezwa na bodi ya nyama,” amesema

Mmoja wa walaji wa kitoweo hicho, Neema Hassan akizungumza na mwananchi amekiri baadhi ya wafanyabiashara wa bucha za nyama kuuza nyama zilizooza.

“Nilinunua nyama iliyooza baada ya kuifikisha nyumbani ilikuwa inanuka inatoa fuza niliirudisha, wakanibadilishia naomba mamlaka husika wakague mara kwa mara,”

Mmoja wa wafanyabiashara wa nyama, Shaban Hamis amesema baadhi ya wanaotumia sumu hizo lakini changamoto hizo zinasababishwa na kutokuwa na elimu ya kutosha.

“Baadhi wanatumia sumu kuua wadudu kwasababu huwaelewi madhara yake mfano kutumia sumu aina ya rungu kuua nzi buchani wengi hawafahamu madhara yake,”

“Wametupatia elimu tumeelewa, tutakata leseni pia kama walivyoelekeza, tulikuwa hatuyafahamu haya, asubuhi ilikuwa ni kuinama na kuchinja tu, tunaosha sehemu yeyote ile,”amesema

Ofisa Mkaguzi Bodi ya nyama kanda ya Magharibi, Kulwa Joseph baada ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao eneo la machinjio ya Manispaa ya Mpanda amewataka kufuata taratibu  ili ubora wa nyama uendelee kuwa salama.

“Lengo la kuwapa elimu hii ni kuhakikisha nyama kutoka kwa mzalishaji, mfugaji hadi kumfikia mlaji ubora wake usimamiwe, msipotekeleza faini zinafuata” amesema Joseph