Wawakimbia wenza wao kliniki kisa kupima VVU
Muktasari:
- Wanaume mkoani Shinyanga wanawakimbia wake zao kwenda nao kliniki, kisa wanaogopa kupima VVU
Shinyanga. Baadhi ya wajawazito mkoani Shinyanga wamekuwa wakifanyiwa ukatili na wenza wao pale wanapowataka kwenda nao kliniki kupima maambukizi ya Ukimwi.
Hayo yamesemwa na mganga mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt Yudas Ndungile kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika katika mji mdogo wa Isaka halmashauri ya Msalala ambapo alisema kuwa wanaume nao wanapaswa kuongoza na wenza wao pasipo shaka kwenda kupima Ukimwi.
Dkt Ndungile amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi Mkoa wa Shinyanga kiko juu kwa asilimia 5.9 ukilinganisha na kiwango cha kitaifa 4.7
"Wanaume wapendeni wenza wenu wanapopata ujauzito muwasindikize kliniki mkapime afya kwa pamoja msiwaache pekee yao wakapime mshuhudie wote na kupewa ushauri nasaha wa namna ya kuishi"amesema dkt Ndungile.
Dkt Ndungile amesema kuwa maambukizi ya virusi vya ukimwi yameongezeka kutoka asilimia 3.9 mwaka jana hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka huu huku watu zaidi ya 6000 wamebainika kuwa na maambukizi mapya.
Ofisa maendeleo ya jamii mkoa wa Shinyanga Tedson Ngwale amesema kuwa siku hizi wajawazito nao wamekuwa na mtindo wa kuchukua mwanaume yoyote ambaye siye mume wake nakwenda naye kliniki Ili mradi akapate huduma ikiwemo kupima ukimwi jambo ambapo ni hatari.
Kaimu meneja wa Shirika la Uheso linalojishughulisha na jamii inayoishi na virusi vya Ukimwi wilayani Kahama David Edson amesema kuwa wamekuwa wakihamasisha kundi la vijana wasichana katika suala la kupima VVU na kuwapa ushauri nasaha.
Scholastika Kapera mwenyekiti wa mtandao wa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi (WAVIU) amésema kumekuwa na malalamiko kwa wajawazito wanapokwenda kliniki wanaelezwa kwenda na wenza lakini wanaume wamekuwa hawapo tayari , badala yake yake wamekuwa wakikodi wanaume kuwasindikiza kliniki na ndio hao wanaopimwa virusi vya Ukimwi.