Wawili kizimbani kwa kughushi cheti cha kifo

Muktasari:

Yazidu Mwakibe na Gerald Mapunda wakazi wa jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Temeke wakikabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kughushi cheti cha kifo kinachoonesha kuwa kimetolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Uthamini (Rita).

Dar es Salaam. Yazidu Mwakibe na Gerald Mapunda wakazi wa jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Temeke wakikabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kughushi cheti cha kifo kinachoonesha kuwa kimetolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Uthamini (Rita).

Akisoma hati ya mashtaka ya kesi hiyo  namba 38 ya mwaka 2019 leo Jumanne Januari 27, 2021 wakili wa Serikali, Salome Assey amedai  washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kula njama kufanya uhalifu, kughushi na kuwasilisha cheti cha kughushi.

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo,  Karim Mushi mwendesha mashtaka huyo amedai  katika shtaka la kwanza kati ya Agosti 14,2019 eneo lisilojulikana washtakiwa wote kwa pamoja walifanya kosa la kufanya uhalifu.

Katika shtaka la pili, inadaiwa Agosti 14 eneo lisilojulikana wote kwa pamoja walighushi cheti cha kifo kinachoonyesha kilitolewa na Rita Septemba 14,2019.

Shtaka la mwisho imeelezwa kuwa tarehe isiyojulikana mwaka 2019 katika mahakama ya mwanzo ya Temeke kwa nia ovu waliwasilisha cheti cha kughushi kwa Jesephita  Kinyondo ambaye ni hakimu wa mahakama ya mwanzo Temeke.

"Shtaka la kula nyama kufanya uhalifu kifungu cha 384 Sheria ya kanuni ya adhabu Sura ya 16 rejeo mwaka 2019 adhabu yake kifungo cha miaka  saba jela, shtaka la kughushi kifungu cha  333,335(a) na 338 ya Sheria  ya kanuni ya adhabu sura 16 rejeo mwaka 2019 adhabu yake jela miaka saba.”

“Na kuwasilisha cheti cha kughushi kifungu cha 342 cha sheria ya kanuni adhabu yake kifungo cha miaka saba jela," amedai Assey.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo walikana kutenda makosa hayo huku Assey akidai upelelezi umekamilika na kuiomba  mahakama hiyo ipange tarehe ya kusoma maelezo ya awali huku washtakiwa wakirudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 4, 2021