Wawili mbaroni wakidaiwa kusafirisha mifugo 514 bila vibali
Muktasari:
- Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kutorosha mifugo 514 kwenda nchi jirani kwa kutumia kampuni bandia.
Arusha. Jeshi la Polisi kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo nchini, linawashikilia watuhumiwa wawili wakidaiwa kutorosha mifugo 514 kwenda nchi jirani wakitumia kampuni bandia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa kikosi hicho nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Simon Pasua, watuhumiwa hao wamekamatwa juzi Aprili 6, 2024 wilayani Longido, Mkoa wa Arusha.
Amesema watuhumiwa hao ambao majina yao kwa sasa yanahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi, walikamatwa baada ya kikosi hicho kupewa taarifa na wananchi.
“Kwa kushirikiana na raia, tumewakamata watuhumiwa wawili wakiwatorosha mbuzi na kondoo 514 kwenda nchi jirani wakitumia leseni ya biashara ambayo siyo yao,” amedai kamanda huyo.
Kutokana na hilo, ametoa wito kwa wafanyabiashara kufuata utaratibu wa uuzaji wa mifugo kuepuka kadhia za kuvunja sheria.
Paseua amesema wataendelea kutoa elimu na kuwachukulia hatua wote wanaokiuka utaratibu.
"Tunatoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi kwa kutoa taarifa za utoroshwaji au wizi wa mifugo, kuhakikisha kwamba wanapofanya biashara za mifugo wanakuwa na leseni zao wao wenyewe na wafuate taratibu za usafirishaji wasitumie leseni au kampuni za watu wengine ambazo hazihusiani na wao na tutaendelea kutoa elimu kwa wafanyabishara wa mifugo na watakaoendelea kukiuka itawachukulia hatua," amesema kamanda huyo.
Daktari wa mifugo katika mnada wa mpaka wa Tanzania na Kenya (Namanga) wilayani Longido, Ally Hamka amewataka wafanyabiashara kufuata utaratibu, wasikurupuke wala wasipende kupita njia za mkato.