Wawili wafa ajalini 16 wajeruhiwa Mafinga

Gari ambalo limepata ajali na kusababisha vifo vya watu wawili  katika eneo la Majinja-Changalawe Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Picha na Mary Sanyiwa

Muktasari:

  • Ajali hiyo imetokea katika barabara kuu ya Makambako – Iringa, imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso mali ya Shirika la Umeme Tanzania lililokuwa likiendeshwa na Zakaria Yona (44), mkazi wa Mafinga ambaye amemgonga mwendesha baiskeli kabla ya gari hilo kuacha njia na kupinduka.

Mafinga. Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa akiwemo mtumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Evance Lusinde (37).

Ajali hiyo imetokea leo Jumapili Juni 16, 2024 baada ya gari kuacha njia na kupinduka eneo la Majinja Changarawe katika Halmashauri ya Mji Mafinga mkoani Iringa.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, Alfred Mbena amesema ajali hiyo imetokea katika barabara kuu ya Makambako – Iringa, imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso mali ya Shirika la Umeme Tanzania lililokuwa likiendeshwa na Zakaria Yona (44), mkazi wa Mafinga ambaye amemgonga mwendesha baiskeli kabla ya gari hilo kuacha njia na kupinduka.

Amewataja waliopoteza maisha ni Valentino Msogoya (70), mkazi wa Changarawe na Evance Lusinde (37), mfanyakazi wa Tanesco aliyekuwa abiria kwenye gari hilo.

Majeruhi wa ajali hiyo ni Zakaria Yona (dereva wa gari hilo), Tamsi Gerald (28), Peter Mbepwa (35), Alamu Mgaya (41), Emmanuel Ngaga (21), Nicolaus Malile (30), mkazi wa Mtili Mufindi, Chedinyo Kanyika (22), Tamim Leonar Mgetwa (16), Martin Ponda (35), Ibrahim Lupola (31), Paschal Leonard (18), Mary Nyagawa (41), Paulo (28), jina la pili  halijulikani), Zefania Chumi (26), Juma Mwakalenga (26), na Aizack Mwaigonile (25), mfanyakazi wa Tanesco.

Wote wamepatiwa matibabu katika Hospitali ya Mji Mafinga na hali zao zinaendelea vizuri.

Kamanda huyo amesema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva aliyeshindwa kulimudu gari lake alipokuwa akimkwepa mwendesha baiskeli ambaye pia alimgonga na gari likapinduka.

“Niwaombe sana madereva, muwe makini mnapokuwa barabarani na kuepuka kubeba watu kwenye magari yasiyo ya abiria,” amesema kaimu kamanda huyo.

Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Mafinga, Amata Haule amesema amepokea miili ya watu wawili na majeruhi 16 kutokana na ajali hiyo.

Amesema majeruhi wanne wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa kwa matibabu zaidi, lakini wengine waliobaki hali zao zinaendelea vizuri na wameruhusiwa kutoka hospitali.

Meneja wa Tanesco Mafinga, Modest Mahururu amesema gari lililopata ajali ni mali ya Tanesco lilikuwa na wafanyakazi wawili waliokuwa wanatokea kazini eneo la Igowole.

Amesema walipokuwa njiani maeneo ya mashamba ya miti, walisimamishwa na wakata miti wa Sao Hill wakaomba lifti wakawapakia.

"Watumishi wangu walikuwa Igowole kwa shughuli zao za kila siku. Waliporudi walipita katika shamba la Sao Hill na kukutana na wakata miti. Kwa kuwa walikuwa porini na waliomba lifti, ilikuwa vigumu kuwaacha, hivyo waliwasaidia. Walipofika eneo hilo ndipo walipopata ajali hiyo," amesema Mhururu.