Wawili walioshitakiwa pamoja wakili Mwale waachiwa huru

Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha hukumu iliyowatia hatiani na kuamriwa kulipa faini ya Sh100 milioni kila mmoja, na kuwaachia huru waliokuwa mameneja wa Benki ya CRDB, waliotiwa hatiani kwa kosa la utakatishaji wa fedha.

Boniface Mwimba aliyekuwa meneja wa benki ya CRDB tawi la Meru na Elias Ndejembi aliyekuwa meneja wa huduma kwa wateja wa benki hiyo, wameachiwa huru baada ya kushinda rufaa yao iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu.

Katika kesi ya awali, Mwimba aliyekuwa mshitakiwa wa tatu na Ndejembi mshitakiwa wa nne, walikuwa wameshitakiwa pamoja na wakili maarufu nchini, Median Mwale na mfanyabiashara tajiri wa nchini Kenya, Don Ooga Gichana.

Wanne hao walikuwa wanakabiliwa na mashitaka mbalimbali ya utakatishaji wa fedha Dola 5.4 milioni, ambazo ni karibu Sh12 bilioni za Tanzania, ambazo ziliingizwa na kutolewa katika akaunti zilizokuwa zimefunguliwa benki ya CRDB. Makosa hayo yalidaiwa kutendeka kati ya Novemba 2009 na Februari 2015.

Gichana anayetajwa kuwa ni mfanyabiashara tajiri na mwanasiasa mashuhuri Kenya, aliachiwa mwaka 2013 baada ya kukiri makosa na kutakiwa kulipa faini ya Sh300 milioni na Mwale naye akakiri makosa 2018 na kulipishwa faini ya Sh200 milioni.

Mwaka 2019, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wa wakati huo ambaye sasa ni Jaji, Biswalo Mganga akatangaza Serikali kutaifisha mali za Mwale ambazo ni magari sita ya kifahari, nyumba mbili na shamba vyote vikiwa na thamani ya Sh1.1 bilioni.

Gichana alishawahi kugombea ubunge jimbo la Kitutu Chache Kusini nchini humo mwaka 2013 na mwaka 2007 alipata umaarufu baada ya kumzawadia mwanasiasa mashuhuri nchini humo, Raila Odinga, gari la kifahari aina ya Hammer.
 

Kesi ya waliokuwa mameneja

Baada ya Mwale na Gichana kukiri makosa yao, Mwimba na Ndejembi aliendelea kushikilia msimamo wa kukanusha tuhuma hizo, lakini mahakama iliwatia hatiani na kuwaamuru kulipa faini ya Sh100 milioni kila mmoja.

Endapo wangeshindwa kulipa wangetumikia kifungo cha miaka mitano jela.
Hawakuridhishwa na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa kupitia kwa mawakili wao, Moses Mahuna na Hellen Mahuna na moja ya sababu ni si sahihi kuwashitaki kwa kula njama na hapo hapo kosa halisi la utakatishaji.

Pia walidai kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika uendeshaji wa shauri hilo na kwamba, kulikuwa na kupishana kati ya maelezo ya kosa na ushahidi uliopokelewa mahakamani na baadaye ukatumika kuwatia hatiani kwa makosa ya utakatishaji.

Ilielezwa kuwa katika ushahidi kulikuwa na hundi 17 zenye thamani ya Dola 5,296,327.25 tofauti na Dola 5,468,699.25 zinazoonekana kwenye maelezo ya kosa hilo na hivyo kufanya tofauti ya Dola 172,372 za Marekani.
 

Hukumu ya Majaji

Katika hukumu yao iliyotolewa Aprili 18,2023 na kupakuliwa katika mtandao wa Mahakama wa Tanzill, majaji wa mahakama ya Rufani Tanzania, Shaban Lila, Lugano Mwandambo na Patricia Fikirini, waliwaona hawana hatia.

Majaji walizingatia kuwa ni msimamo wa kisheria kuwa kunapojitokeza tofauti kati ya maelezo ya hati ya mashitaka na ushahidi, hiyo husababisha upande wa mashitaka uonekane umeshindwa kuthibitisha shitaka bila kuacha shaka.

Kulingana na majaji hao, walisema kumbukumbu zinaonyesha upande wa utetezi uliibua hoja kwamba ushahidi wa Jamhuri unaweza kuthibitisha tu miamala ya hundi 15 kati ya 17 inayoonekana katika maelezo ya kosa hilo.

“Ushahidi uko wazi kwamba kosa la kugushi lilianzia sehemu nyingine na mtu ambaye hana mahusiano na benki ya CRDB,” alisema majaji hao.

Majaji hao katika hukumu hiyo, walisema jaji aliyesikiliza kesi hiyo hakufanyia kazi hoja ya utofauti wa kiwango cha fedha na idadi ya hundi na badala yake akaegema ushahidi huo na kuwatia hatiani warufani hao na kuwahukumu.

“Tunaelewa kuwa mahakama iliegemea maungamo ya mshitakiwa wa kwanza (Gichana) kama sehemu ya ushahidi wa kuwatia hatiani warufani lakini, ukitizama maungamo hayo yalihusu utendaji kosa la kugushi,” alieleza majaji hao.

“Kama ilivyobainika, kulikuwa na ombwe la kupiga miayo katika ungamo kuhusiana na idadi ya hundi na kiwango cha fedha kilichohusika. Katika mazingira hayo huwezi kusema upande wa mashitaka ulithibitisha mashitaka hayo”

Majaji hao walisema dosari hizo zinatosha kuamua rufaa hiyo kwa manufaa ya warufani hivyo wakabatilisha kutiwa kwao hatiani na adhabu waliyopewa na kuamuru waachiliwe huru labda kama wanashikiliwa kwa maosa mengine.

Pia majaji hao wamamuru kama kuna faini yoyote walilipa warejeshewe fedha hizo.