Wawili wateuliwa kuchuana kumrithi Profesa Hosea TLS

Profesa Edward Hosea.

What you need to know:

  • Mawakili Sungusia, Shirima wateuliwa kuchuana kumrithi Profesa Hosea TLS katika uchaguzi utakaofanyika Mei mwaka huu.

Dar es Salaam. Mawakili Harold Sungusia na Regnald Shirima wa wameteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika uchaguzi utakaofanyika Mei mwaka huu.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya Rais aliyepo Profesa Edward Hosea kumaliza muda wake ambapo ameongoza kwa kipimdi cha miaka miwili.

Akizungumza leo Ijumaa Machi 24, 2023 mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi Wakili Mwandamizi Charles Rwechungura amesema, uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za mwaka 2022.

“Kamati ya uchaguzi TLS imepitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za iuongozi kwa ajili ya uchaguzi wa chama wa mwaka 2023, waliojitokeza nafasi ya urais ni watatu na baada ya kupitia vigezo tulijiridhisha wawili ndio wenye sifa,”amesema Wakili Rwechungura.

Kwa upande wa umakamu kamati hiyo imepitisha majina manne ambayo Wakili Revocatus Kuuli, Emmanueli Augustino, Aisha Sinda na Fredrick Mtei.

Meneja huduma kwa wanachama, Ana Muro amesema uchaguzi huo utatanguliwa na mkutano mkuu utakaofanyika kuanzia Mei 11 jijini Arusha.

Amesema pamoja na uchaguzi huo na mkutano mkuu pia kutakuwa na semina ya kuwajengea uwezo mawakili na baadaye kutembelea mbuga za wanyama.