Wazazi CCM kuchaguana, Kinana awapa mambo matatu

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Abdulrahman Kinana.

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abrahaman  Kinana ameutaka uongozi ujao wa Jumuiya ya Wazazi Taifa  kusimamia mambo matatu.

Dodoma. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Abdulrahman Kinana ameutaka uongozi ujao wa Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho kusimamia mambo matatu.

Mambo hayo ni mmonyoko wa maadili, kujenga uchumi wa chama na kuendelea kupunguza madeni.

Kinana ameyataja mambo hayo leo Alhamisi Novemba 24, 2022 wakati akifungua mkutano wa 10 wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ambao unaenda pamoja na uchaguzi wa kuwapata viongozi wa juu wa jumuiya hiyo.

Viongozi watakaochaguliwa ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti, wajumbe watano wa Halmashauri Kuu (NEC), wajumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa na Uwakilishi Jumuiya zingine ngazi ya Taifa.

Kinana amesema wale ambao watapata nafasi ya kuchaguliwa ni lazima wafanye kazi kwa bidii ikiwemo kusimamia suala la mmonyoko wa maadili.

"Msingi wa kuundwa kwa Jumuiya ya Wazazi iliundwa kwa ajili ya kusimamia malezi na maadili hasa kuanzia kwa watoto.

"Taifa letu linakabiliwa na mmonyoko wa maadili hadi kuhatarisha usalama, kuna vitendo vya ukiukwaji wa maadili," amesema Kinana.

Pia, amewataka kusimamia suala la kuimarisha uchumi wa jumuiya kwani haujakaa vizuri.

"Chama kimetoa maelekezo kutekeleza sera ya miradi na uwekezaji ili kuondokana na ruzuku. Nimpongeze Rais na Mwenyekiti (Samia Suluhu Hassan) kwa kuongeza na kujali maslahi ya wafanyakazi.

"Hatuwezi kuendelea kutegemea fedha kutoka kwa wasamaria kufanya hivyo ni kuhatarisha uhuru," amesema Kinana

Vilevile ameutaka uongozi ujao kuendelea kupunguza madeni ambayo inadaiwa Jumuiya hiyo.

Kuhusiana na uchaguzi, Kinana amesema waliojitokeza kugombea ni wengi lakini nafasi ni chache hivyo anaamini hata watakaochaguliwa watakuwa ni wachache.

"Niwaombe kwa wale ambao mtachaguliwa kujituma na kufanya kazi ya kufikia matarajio.

"Mwenyekiti amenituma niwafikishie salamu, anawatakia kila la kheri, anawapongeza sana kwa hatua hii kwa kufanikisha chaguzi zote na kwa kuzingatia kanuni za chama chetu," amesema.

Aidha, ameipongeza Jumuiya kwa kujenga ofisi makao makuu pamoja na kuendesha shule na kuongeza ufaulu.

"Kwa watendaji wa chama chetu, nimpongeze Rais na Mwenyekiti wetu (Samia Suluhu Hassan), Katibu Mkuu (Daniel Chongolo) anafanya kazi vizuri hata mimi kwenye ukatibu wangu sikuwa na uwezo kama huu wako unafanya kazi nzuri ya kutazama maslahi,” amesema Kinana.

Katika uchaguzi huo ambao msimamizi wake mkuu, Maalim Kombo Hassan, wanaochuana nafasi ya uenyekiti wako nane, akiwemo Dk Edmund Mndolwa, anayetetea nafasi hiyo.

Wengine ni, Fadhili Maganya, Bakari Kalembo, Said Mohamed Mohamed (Dimwa), Mwanamanga Mwaduga, Ally Maulid Othman, Ali Khamis Masudi na Hassan Haji Zahara.


Endelea kufuatilia mitandao yetu kwa habari zaidi