Wazazi wakumbushwa wajibu wa kuwalea watoto kimaadili

Tuesday October 05 2021
wazazi pic1
By Florah Temba

Moshi. Wazazi kukosa muda wa kukaa na watoto wao na kuacha jukumu la malezi kwa wasaidizi wa kazi za nyumbani, kumetajwa kuwa chanzo cha ongezeko la matukio ya ukatili, unyanyasaji na mauaji kwa watoto.

Hayo yamebainishwa jana Septemba 25, 2021 na Mkurugenzi wa Shule ya msingi ya Little Acorns iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Julieth Sopiato, wakati wa mahafali ya kwanza ya darasa la saba, akiwataka wazazi kuwalea watoto katika njia iwapasayo ili wawe na maadili mema katika jamii.

Amesema wazazi wanapaswa kutenga muda wa kuwa na watoto wao toka wakiwa wadogo na kuwafanya marafiki, ili kuwawezesha kuwa wajasiri na kueleza changamoto na madhila wanayokutana nayo pindi wazazi hawapo nyumbani.

wazazi pic2

"Wazazi tubadilike, tuwafanye watoto kuwa marafiki zetu, na tunaporudi jioni kutoka kazini tuwe na tabia ya kukaa nao kuzungumza nao na kuwauliza siku yao ilikuwaje na changamoto zipi walizipitia, lakini pia tuwajengee ujasiri na kujiamini ili waweze kuwa wazi kutueleza chochote.

"Tuwalee watoto katika uwazi, tusiache jukumu la malezi ya watoto kwa wasichana wa kazi, bibi au shangazi. Tusimame kama wazazi kwenye nafasi zetu,” amesema.

Advertisement

Amesema uwazi ndiyo utamwezesha mtoto kumweleza mwalimu jambo lolote na hata mambo ya ajabu anayofanyiwa lakini si mzazi.

Akizungumza kwenye mahafali hayo, Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo amesema nafasi ya malezi kwa wazazi katika jamii leo imepotea kutokana na changamoto za kimaisha, jambo ambalo ni hatari katika makuzi kwa watoto.

"Hali hii inasababisha watoto kukuzwa katika tabia na mienendo isiyofaa, leo walimu wanapelekewa watoto kitabia na mienendo ni tofauti na wanavyoonekana wazazi wao, kwa sababu mtoto anakuwa analelewa na mfanyakazi na mzazi hajui wala hajawahi kukaa nae, ni changamoto kubwa kwa jamii na nchi ambazo uchumi unakua kwa sasa," amesema Tarimo.

Advertisement