Waziri Bashungwa ataka uadilifu, kutunza siri za Serikali

Friday June 24 2022
uadilifuupiic
By Mwandishi Wetu

Dodoma . Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tanisemi), Innocent Bashungwa amewataka watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa  Wizara hiyo imabeba taswira  ya nchi.

Pia, amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatunza  siri za Serikali na kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma kwa kuwa Tamisemi imebeba maisha ya watanzania.

Waziri Bashungwa amesema hayo kwenye Kikao kazi na watumishi wa Tamisemi ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma ambapo kila mwaka huadhimishwa kuanzia Juni 16 hadi 23.

Taarifa iliyotolewa leo Tamisemi imesema kuwa Waziri Bashungwa ameendelea kuwataka watumishi hao kufanyakazi kwa weledi na  kujitoa katika kuwahudumia wananchi na kutojihusisha na rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tamisemi tuna jukumu kubwa la kutoa huduma kwa wananchi niwatake watumishi suala la utoaji wa huduma ni ibada tusimamie katika utendaji wa haki pasina kujihusisha na rushwa. Wizara hii ni kubwa ujue ukiwa humu unatakiwa ufuate maadili ya utumishi wa Umma na imani tuwe nayo sababu sisi tunatoa huduma moja kwa moja kwa wananchi wetu” amesema Waziri Bashungwa

Amesema kuwa baadhi ya  vitendo vinatokea ambavyo  ni kinyume na maadili ya utumishi wa Umma ambapo baadhi ya watu wanaharibu taswira ya ofisi hiyo kwa kushiriki kwenye vitendo ikiwamo kugushi barua za uhamisho wa watumishi  hivyo, amemuelekeza  Katibu Mkuu Profesa Riziki Shemdoe  kulishughulikia kwa haraka suala hilo.

Advertisement

“Ninaelekeza wale wote ambao waliopata barua za uhamisho ambazo tumeshafanya uchunguzi na sio halali warudishwe kwenye vituo vyao vya awali na kama kuna stahiki zozote walipatiwa ambapo ni fedha za Serikali zirudishwa na wachukuliwe hatua” amesisitiza Waziri Bashungwa

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Tamisemi, David Silinde  amewashukuru watumishi hao kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi hao  kuweza kutekeleza majukumu yao ikiwa wao ni moja kwa moja wanawajibika na wananchi huku akiwataka kuendelea kuwahudumia wananchi kwani wana imani na Wizara hiyo.

“Imani ya wananchi ni pamoja na kuwa na imani ya Rais Samia Suluhu Hassan na sisi Tamisemi tunawajibika moja kwa moja kwa wananchi nitoe rai kwa watumishi wote kufanyakazi kwa weledi kwa kuwa  tumeaminiwa hivyo tuaminike” amesema Silinde

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Tamisemi, Profesa  Riziki Shemdoe amemuhakikishia Waziri Bashungwa kuwa maelekezo yote aliyoyatoa anaenda kuyasimamia ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma.

Amesema wao kama watendaji watahakikisha wanaendelea kushirikiana na viongozi wa ngazi zote za Wizara hiyo ili kuendelea kuwahudumia wananchi

Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Namsifu Maduhu ambaye ni ofisa Utumishi Mkuu, ameushukuru uongozi na kuahidi kutekeleza yale yote yaliyoagizwa kwa lengo la kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

Advertisement