Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Chana aonya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana (kulia) akimkabidhi bendera, Brigedia Jeneral Salum Mnumbe (kushoto)ambaye ni kiongozi wa wapanda mlima kwa ajili ya kupandisha bendera ya Taifa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Picha ba Florah Temba

Muktasari:

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana amewataka wananchi kufuata sheria na kujiepusha na uendeshaji wa shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, ili kuunga mkono jitihada za Serikali za uhifadhi wa mlima huo, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Moshi. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana amewataka wananchi kufuata sheria na kujiepusha na uendeshaji wa shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo katika hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.


Dk Chana ametoa rai hiyo leo Jumatatu Desemba 5, 2022, wakati wa hafla ya uzinduzi wa upandaji mlima Kilimanjaro kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru wa Tanzania Bara, ambapo wapanda mlima zaidi ya 200 wameanza safari ya kuupanda mlima Kilimanjaro, kupandisha bendera ya Taifa, ambapo Desemba 9, wataiweka katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.


Wapanda mlima hao ambao wanaongozwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ), pia wamo mabalozi 11, wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali, Waandishi wa Habari, Wasanii, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Bohari ya Dawa (MSD) pamoja na wadau wengine wa utalii na Taasisi mbalimbali.


Dk Chana amesema Mlima Kilimanjaro unakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu zinazoleta uharibifu wa mazingira, na kwamba ili kuweza kukabiliana na changamoto hizo ni jukumu la kila mwananchi kuwa wazalendo na kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu ili kulinda na kutunza mazingira ya mlima huo.


“Miongoni mwa changamoto zinazoukabili uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro ni pamoja na  ukataji wa miti usiozingatia kanuni za uhifadhi, uingizaji wa mifugo katika maeneo ya Hifadhi, shughuli za kilimo karibu na vyanzo vya maji, uwashaji holela wa mioto hifadhini na ujangili.


“Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia madhara ya mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame uliokithiri, kukauka kwa baadhi ya mito na kupungua kwa mitiririko ya maji, migogoro ya matumizi ya maji, ongezeko la joto, mvua zisizotabirika na mafuriko, hivyo nichukue nafasi hii kutoa rai kwa wananchi kufuata sheria kwa kujiepusha na uendeshaji wa shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa".


Pia, amesema Mlima Kilimanjaro ni nembo muhimu ya Taifa la Tanzania na umebeba historia kubwa ya nchi ambapo amesema pia umekuwa ukichangia kuongeza pato la Taifa na kuwataka watanzania kujitokeza kuupanda na kuutangaza.


Amesema utalii unachangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa, na unatoa ajira zisizopungua milioni 1.5 na kwamba mikakati iliyopo ni kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 5 na pato la Taifa litokanalo na utalii lisipungue Dola za kimarekani 6 Bilioni ifikapo mwaka 2025.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Shirika ka Hifadhi za Taifa (TANAPA) Jenerali Mstafu, George Waitara amesema upandaji Mlima Kilimanjaro kupandisha bendera kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru, imeanza mwaka 2008, hatua ambayo imekuwa ikivuta hamasa kwa watu wengi kujitokeza kuupanda na kuutangaza mlima huo mrefu barani Afrika.


Waitara ametoa wito kwa mabalozi 11 wanaopanda Mlima Kilimanjaro, baada ya kushuka kwenda kuutangaza vyema katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania na kuchochea ongezeko la watalii nchini na pia pato la Taifa.


“Tumeboresha mambo mengi ya huduma katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, ikiwemo malazi, vyoo, Mawasiliano na uokoaji  na maboresho yataendelea kufanyika, nitoe rai kwa watanzania, kujitokeza kwa wingi kuupanda Mlima huu, ili kuweza kujionea yaliyomo na kuutangaza ndani na nje ya nchi,” amesema.


Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi – Tanapa, Asteria Ndaga amesema hifadhi ya Kilimanjaro ni miongoni mwa hifadhi tano zinazoongoza kwa kupokea wageni wengi kutoka mataifa ya nje na hivyo kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hifadhi ilipokea wageni 32,834 na kuliingizia Taifa Sh39 bilioni.


“Utalii wa ndani ni asilimia 5 tu ya wageni hao, hivyo Tanapa tunahamasisha watanzania kujitokeza kupanda mlima Kilimanjaro ili kukuza utalii wa ndani na kuchochea ukuaji wa pato la Taifa,” amesema