Waziri Ummy alia na wakurugenzi

Waziri Ummy alia na wakurugenzi

Muktasari:

  • Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu amesema wakurugenzi na watumishi wazembe vichwa vyao ni halali yake.

Dodoma. Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu amesema wakurugenzi na watumishi wazembe vichwa vyao ni halali yake.

Amebainisha kuwa kama ingeruhusiwa awe kwenye mkutano wa hadhara alitamani kuwaita mbele wakurugenzi wa halmashauri za Uvinza, Bumbuli na Same ili wazomewe na wananchi.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Aprili 23, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya mapato kwa robo ya tatu ya halmashauri za wilaya, miji na majiji nchini.

Amesema hayupo tayari kuvumilia uzembe na ubadhirifu wala kumuonea haya mtu ambaye si mwajibikaji.

Amebainisha kuwa haivumiliki wala kukubalika mbele ya kadamnasi kuona watu hawabadiliki na wanaendelea kufanya kazi za mazoea kila wakati.

Kuhusu mapato amesema ziko halmashauri ambazo lazima zitazamwe kwani ziko kwenye hali mbaya kimapato wakati hakuna sababu ya msingi kuwa hivyo.