Waziri Ummy ataja vipaumbele 13 Wizara ya Afya

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya feda ya Wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Muktasari:

Makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yamewasilishwa yakigusia vipaumbele 13 ili kuboresha huduma za afya nchini.

Dar es Salaam. Makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yamewasilishwa yakigusia vipaumbele 13 ili kuboresha huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Mei 16, 2022 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya feda ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya zikiwemo Hospitali za Rufaa za Mikoa, Kanda, Maalum na Taifa.

“Tutaimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya na huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi,” amesema.

Amesema Wizara itaimarisha huduma za afya nchini zikiwemo huduma za mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, utoaji wa huduma za chanjo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini;

Maeneo mengi yaliyotajwa ni pamoja na utoaji wa mafunzo ya wataalam katika sekta ya afya, kusimamia ubora, usalama na ufanisi pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za afya na Kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika utoaji huduma za afya.

“Tutaimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, kudhibiti magonjwa ya mlipuko, kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza na kuimarisha mifumo ya tehama na matumizi ya takwimu,” amesema Waziri Ummy.