Wenye mashamba ya zabibu Dodoma wapata tumaini

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabil Shekimweri amesema Serikali haiwezi kuruhusu upimaji mashamba ya zabibu yawe viwanja.

Dodoma. Mkuu wa Eilaya ya Dodoma, Jabil Shekimweri amesema mashamba ya zabibu katika jiji hilo hayatapimwa viwanja hivyo wakulima waendelee kuchapa kazi.

Shekimweri ametoa kauli hiyo leo ofisini kwake wakati akizungumza na Taasisi ya PASS Trust ambao ni wadau wa kilimo waliokuja na mkakati wa kuinua zao la zabibu mkoani hapa.

Ardhi ya Jiji la Dodoma imepimwa kwa sehemu kubwa na kumekuwa na kelele kuhusu mashamba ya zabibu ambalo ni zao pekee linalolimwa kwa wingi mkoani hapa.

Shekimweri amesema mkakati wa PASS Trust unaendana na mipango iliyowekwa na wilaya hiyo hivyo watafanya kazi kwa ushirikiano katika kufufua zao hilo ambalo linalimwa katika kata 27 kati ya 41 zinazounda wilaya.

Amesema Serikali haitaruhusu kupimwa mashamba hayo kama viwanja wakati uhitaji wa zabibu ni mkubwa kwa kuwa ndiyo dhahabu ya watu wa Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi wa Tanzania Agriculture Sector Trust (PASS Trust), Anna Shanalingigwa amesema taasisi yao inalenga kufanya maonyesho makubwa kuanzia kesho na mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ambaye ni mkulima wa zabibu.

Shanalingigwa amesema katika wiki ya PASS Trust watakuwa na vitu vingi vya maonyesho ambavyo vinalenga kuwaweka pamoja vijana katika kuwapa mbinu na mitaji.

Amesema taasisi hiyo imejipambanua katika kuwainua wajasiriamali wadogo na wakulima katika kuwapatia mikopo ya kujiendeleza kiuchumi.