Wenye ulemavu kuwezeshwa kupata fursa, kushiriki uongozi

Mkuu wa Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Finland nchini Dk Timo Voipio akizungumza wilayani Tarime baada ya kutembelea eneo la utekelezaji wa mradi wa chaguo langu haki yangu.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Afya ya Uzazi ( UNFPA) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Finland na Asasi ya Kupinga Ukatili ya Masanga wamezindua mradi wa kuhudumia watu wenye ulemavu ili kuwajengea uwezo na kupata fursa ya kushiriki katika masula mbalimbali ya kijamii ikiwemo uongozi.

Tarime.  Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Afya ya Uzazi ( UNFPA) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Finland na Asasi ya Kupinga Ukatili ya Masanga wamezindua mradi wa kuhudumia watu wenye ulemavu ili kuwajengea uwezo na kupata fursa ya kushiriki katika masula mbalimbali ya kijamii ikiwemo uongozi.

Mradi huo unaojulikana kama chaguo langu haki yangu utakagharimu zaidi ya Dola za kimarekani 6.2 milioni na  utatakelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika mikoa ya Mara, Shinyanga na Zanzibar lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa kushiriki katika ujenzi na ustawi wa nchi na jamii.

Akizungumza wilayani hapa leo Jumatano Mei 25, 2022, Mkuu wa Ushirikiano kutika ubalozi wa Finland nchini, Dk Timo Voipio amesema kuwa wameamua kufadhili mradi huo ili kusaidia kupaza sauti hasa kwa jamii ambazo bado zinaendeleza mila zinazomkandamiza mwanamke ambazo kwa namna moja ama nyingine zinapeleka kuwepo kwa ulemavu.

"Zamani watu hawakufikiria kama Tanzania inaweza kupata Rais mwanamke na sasa tunaye Rais Samia sasa inabidi tubadilike ili tuwe na akina Samia wengi siku zijazo bila kujali kama ni mlemavu au mzima na uwezo huo tunao" amesema

Amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vikiwemo vitendo vya ukeketaji vina madhara makubwa ukiwemo ulemavu hivyo ni wajibu wa wadau kuungana kwa pamoja kupambana navyo ili viweze kuisha katika jamii.

Dk Voipio mesema kuwa mradi utawapa nafasi walengwa wote wakiwepo wasichana kupata haki yao ikiwa ni pamoja na kupanga maisha wanavyotaka badala ya kupangiwa au kunyimwa fursa.

Meneja wa Mawasiliano kutoka UNFPA, Warren Bright amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na ubaguzi katika jamii.

"Mradi huu unalenga kuina kuwa hakuna mtu anaachwa nyuma kutokana na hali yake hivyo walemgwa watapata elimu juu ya mambo mbalimbali ikiwemo haki zao na hivyo wanakuwa na maamuzi sahihi juu ya mustakabali wa maisha yao" amesema

Amefafanua kuwa watu wenye ulemavu ulemavu wakizijua haki zao watakuwa na uwezo wa kuzidai pale ambapo wanazikosa na kwamba mradi huo pia uatatoa fursa kuwawezesha kiuchumi walengwa ili waweze kujitegemea tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wao wamekuwa tegemezi.

Meneja wa miradi kutoka asasi ya Masanga, Valerian Mgani amesema kuwa mkoani Mara mradi huo utatakelezwa katika wilaya za Tarime na Butiama.

Amesema kuwa tayari maandalizi ya awali yameanza ikiwa ni pamoja na kufanya utafii ili kujua idadi ya walemavu katika wilaya hizo sambamba na kubaini aina za ulemavu wao ili kujua ni huduma zipi wanatakiwa kupata kupitia mradi huo.