Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye ulemavu walia utekelezaji hafifu wa sera

Mwenyekiti wa chama Cha viziwi wasioona Tanzania David Shaba (mwenye fimbo) akiandikiwa maswali kwenye kiganja kwa kutumia kidole cha mtoto wake, Godwin Shaba alipokuwa akihojiwa na Mwananchi kuhusu changamoto wanazozipata watu wenye ulemavu wa aina hiyo. Picha Hamida Shariff



Muktasari:

  • Watu wenye ulemavu wamesema kutotekelezwa kwa sera inayowahusu, kumewafanya wakose haki zao ikiwemo ya kupata elimu, huduma za afya, ajira na mazingira bora ya miundombinu.

Morogoro. Kutotekelezwa kwa Sera ya Watu Wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya kijiji na mtaa ni moja changamoto inayolifanya kundi hilo kushindwa kupata huduma na haki zao mbalimbali ikiwemo kupata matibabu bure, elimu na ajira.

Hayo yamebainishwa Mei 22, 2025 mjini Morogoro na Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi na Wasioona Tanzania, David Shabani wakati wa mafunzo ya utoaji huduma, matunzo na usaidizi kwa watu wenye ulemavu, yaliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP).

Amesema licha ya jitihada na Serikali kutoa ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu, watendaji ngazi ya mitaa na vijiji wameshindwa kutekeleza sera hiyo, badala yake wamekuwa wakihudumia kundi hilo kwa kufuata miongozo ya wizara.

Shabani amesema kuwa changamoto kubwa inatokana na sera kutofafanua vizuri nini kifanyike hasa kwa viongozi wa serikali za mitaa, vijiji katika kutoa huduma, matunzo na usaidizi kwa watu wenye ulemavu, hivyo watendaji au watekelezaji wa sera wamekuwa hawazielewi namna ya kusimamia.

“Natoa mfano kwenye eneo la afya, sera inasema wazi kwamba watu wenye ulemavu watapata huduma za afya bure, hata hivyo watu hao wanapokwenda hospitali wamekuwa wakilipia baadhi ya vipimo na dawa kwenye magonjwa mbalimbali,” amesema Shabani.

Mjumbe wa Jumuiya ya wanawake na watoto wenye ulemavu Tanzania, Linda Macha akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo ya huduma na usaidizi wa watu wenye ulemavu yaliyoendelea mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff

Katika kutatua changamoto hiyo ameshauri kuwepo na miongozo kuanzia ngazi za chini ambayo ni serikali za mitaa na vijiji ili kuimarisha ushirikishwaji wa kutoa uamuzi na huduma za watu wenye ulemavu.

“Kukosekana kwa miongozo kumesababisha mambo yetu mengi kukwama, hata masuala ya ajira kuna vikwazo, mambo ya ajira sera inasema lazima kila mwajiri asilimia 3 ya wafanyakazi wake wawe ni wenye ulemavu, hata hivyo wapo baadhi ya waajiri hawatekelezi sera hiyo,” amesema Shabani.

Ameongeza: “Kuna walemavu wengine ambao hawawezi kuajiriwa kutokana na hali ya ulemavu wao, mfano mimi ulemavu wangu sioni wala sisikii, sasa nani ataniajiri, hata hivyo walemavu wa aina hiyo inawezekana wakawa na watoto wenye elimu na sifa za kuajiriwa, nadhani Serikali ingeweka sera ya kuwapa watoto hao ajira ili wawasaidie wazazi wao,” amesema Shaba.

Mjumbe kutoka Jumuiya ya wanawake na watoto wenye ulemavu Tanzania, Linda Macha amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kupatiwa usalama wa kimaisha ingawa haki hiyo ipo lakini bado haijafanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji yao msingi.

Amesema haki za watu wenye ulemavu zinapaswa kuboreshwa katika nyanja zote ikiwemo miundombinu ya majengo kwa kuweka maeneo ya kupitia watu wenye ulemavu, vyoo vitakavyowawezesha kujihudumia.

“Vijijini wapo akina mama walioathiriwa na mila kandamizi kuwafungia watoto wenye ulemavu ndani na kushindwa kuwapeleka shule kwa kuhofia gharama na kubanwa na shughuli za familia,” amesema Macha.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Ussy Khamis Debe amesema kwa mujibu wa sheria namba 8 ya mwaka 2022 ya watu wenye ulemavu, imewapa mamlaka ya kusimamia na kuratibu masuala yote ya wenye ulemavu hasa katika masuala ya haki na fursa kwa kundi hilo.

Debe amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha kwamba huduma za msingi zinapatikana hasa huduma za afya, elimu na miundombinu ili kuhakikisha wanapata huduma na kwamba Serikali imeweka vipaumbele vingi kwa mujibu wa bajeti.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022, watu wenye ulemavu ni wale wote wenye changamoto za muda mrefu za kimaumbile, kiakili na katika mfumo wa fahamu, hivyo nao wana haki ya kushiriki sawa na makundi mengine ya kijamii katika kuzifikia fursa mbalimbali.