Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wezi wavunja makanisa KKKT, Sabato na kuiba

Dar es Salaam. Watu wasiojulikana wameingia katika nyumba za ibada wilayani Kibiti, mkoani Pwani na kuiba vifaa mbalimbali pamoja na chakula. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Protas Mutayoba amethibitisha.

Kamanda Mutayoba akizungumza na Mwananchi jana, alisema Jeshi la Polisi linaendelea na msako kuwanasa wahusika wote wa matukio hayo.

Tukio la kwanza alilotaja Kamanda Mutayoba, lilitokea usiku wa kuamkia jana likihusisha wizi wa mali za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kibiti.

“KKKT Kibiti wezi waliiba mixer moja, amplifaya, mishumaa mitatu, microphone, sasa wakati askari wa Rufiji wakiwa kwenye msako wa kuwatafuta waliotenda uhalifu huu ndio wakakumbana na hao walioiba chakula,” alisema.

Taarifa za kuibiwa kanisa hilo, zilienezwa kupitia ujumbe mfupi wa maandishi wenye jina na Mchungaji wa Kanisa hilo, Kaunda Kense na kusambaa mitandaoni.

“Wapendwa watumishi, hapa kwetu Kibiti tumeibiwa jana Power Mixsa, Mic 3 na risza zake, Stablaisa, Mishumaa 2 ya Madhabahuni, Feni ya Madhabahuni. Tumetoa taarifa Polisi toka jana, Rev Kaunda Kense,” ulisomeka ujumbe huo.

Hata hivyo, alipotafutwa Mchungaji Kense alikanusha kuandika ujumbe huo akisema tukio hilo halijatokea, akisema ujumbe huo huenda umeandikwa na watu wenye nia ovu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Upendo Media Network, Neng'ida Johannes ambaye ni Msemaji wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani alisema: “Hatuna taarifa ya tukio hilo, tutalifuatilia."

Tukio la pili la wizi uliohusisha chakula, Kamanda Mutayoba alisema limetokea ndani ya Kanisa la Adventisti Sabato Kibiti usiku wa kuamkia jana.

"Walichoiba ni mahindi ya kande kilo 50, mafuta lita moja na nusu na maharage kilo tano, ndani ya kanisa kulikuwa na vifaa vingi havikuchukuliwa, maana yake huyu aliyeiba lengo lake lilikuwa chakula, hivyo wahalifu bado tunawatafuta."

Mapema mwaka huu, tukio la wizi kwenye nyumba ya ibada lilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Nronga, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, ambapo wezi walivunja ofisi ya mhasibu na kuiba zaidi ya Sh3 milioni za sadaka na kompyuta mpakato.

Mwaka jana mkoani Njombe, Polisi walikamata vitu mbalimbali vilivyokuwa vimeibwa baada ya wezi kuvunja nyumba mbalimbali za ibada na kuiba.

Januari 4, 2022, watu wanne walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na shtaka la wizi wa Sh480.5 milioni ambazo ni mali ya msikiti wa Shree Sanatan Dharma.

Mwaka huo huo, Aprili 18, kamera za ulinzi ‘CCTV’ zilimnasa kijana mmoja akimwibia simu mmoja wa waumini aliyekuwa akiswali katika Masjid Mindhir (msikiti wa Baghani, visiwani Zanzibar) kisha akaondoka pasi na kukamatwa.

Matukio hayo yaliendelea kuripotiwa ambapo Machi 9, 2021, watu wasiojulikana waliingia Kanisa la Parokia ya Mt. Augustino Wanging’ombe Jimbo Katoliki la Njombe kupitia dirishani (kwa kulivunja) na kuiba vitu mbalimbali vinavyotumika kwa ajili ya maadhimisho ya misa takatifu.

Juni 2018, watu wasiofahamika, walivunja mlango mdogo wa mimbari katika Msikiti Mkuu wa Igunga, Mkoa wa Tabora na kuiba Sh720,000 za sadaka.

Mbali na tukio hilo, Aprili 5, 2018, watu wanaodaiwa kuwa majambazi walivamia Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu-Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam na kupora fedha na baadhi ya vifaa vya kuendeshea misa kanisani hapo.