Yaleyale ndani ya CUF

Naibu katibu wa CUF, Magdalena Sakaya

Muktasari:

  • Uamuzi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini kuisajili bodi mpya ya upande wa Profesa Lipumba umepokelewa na upande wa Maalim Seif kama hatua nyingine ya kukoleza mgogoro unaoendelea na chama hicho

Dar es Salaam. Kama ni kidonda, bado ni kibichi na kinahitaji dawa kali ili kikauke. Mzozo mpya unafukuta ndani ya CUF baada ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), kusajili bodi ya wadhamini upande unaomuunga mkono mwenyekiti anayeungwa mkono na ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Hatua hiyo ya Rita haijaungwa mkono na upande wa katibu mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad uliosema uamuzi huo unakirudisha chama chao kulekule walikotoka hadi kufikishana mahakamani.

Uamuzi wa Rita kuisajili bodi hiyo umefanyika zikiwa zimepita siku 18 tangu Mahakama Kuu kutengua wajumbe wa bodi walioteuliwa na upande wa Lipumba.

Februari 18, Mahakama hiyo ilitangaza kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo na kutowatambua wajumbe wa upande wa Maalim Seif.

Baada ya uamuzi huo kila upande ulitangaza kufanya mkutano wa kujaza nafasi hizo, kisha wakasema watapeleka majina hayo Rita ili yaweze kusajiliwa.

Jana, naibu katibu wa CUF, Magdalena Sakaya alisema usajili wao umefanikiwa baada ya kurekebisha dosari zilizoelezwa na Mahakama na kufuata maelekezo waliyopewa ili kuirasimisha bodi yao.

Alisema hatua inayofuata ni bodi hiyo kukaa na kuchagua mwenyekiti ili kuanza kazi ya kuendesha chama na kushughulikia kesi zilizopo mahakamani.

“Niwasihi wanachama wa CUF na Watanzania kwa ujumla waache kusikiliza habari zisizoeleweka zinazozungumzwa huko mitaani na kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Sakaya.

“Chama kipo imara chini ya Profesa Lipumba na tunasubiri bodi ianze kazi mara moja kukipeleka mbele zaidi.”

Wakati Sakaya akieleza hayo, Nassor Ahmed Mazrui, naibu katibu mkuu wa CUF (Zanzibar) upande wa Maalim Seif aliliambia Mwananchi kwamba, Rita inawarudisha nyuma walikotoka kwa kusajili bodi ya upande wa Profesa Lipumba.

“Awali tulipowauliza (Rita) mnasajili lini (bodi) walitujibu wanasubiri hukumu ya Machi 18 kuhusu uhalali wa Lipumba,” alisema.

“Lakini leo (jana), tunasikia Rita imekubali kuisajili bodi ya Lipumba. Hii siyo dalili nzuri ina lengo la kukivuruga na kuisambaratisha CUF, sisi tulikuwa wa kwanza kupeleka majina ya wajumbe lakini waliojibiwa ni wale waliopeleka mwisho.”

Alisema kwa sasa hawawezi kuzungumza au kufanya lolote badala yake wanasubiri uamuzi wa kesi yao Machi 18 utakaowapa mwelekeo wa hatua za kuchukua kuhusu mwenendo wa chama hicho.

Uamuzi huo unatarajiwa kuamua kama Profesa Lipumba ni mwenyekiti halali wa chama hicho au la, baada ya mwaka 2015 kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo kisha baadaye kurejea jambo ambalo linapingwa na upande wa Maalim Seif. Kutokana na mivutano pande hizo mbili zimefikishana mahakamani ambako kuna kesi kadhaa zinazotokana na mgogoro ndani ya chama hicho.