Yanayowasubiri ma RC Arusha, Mwanza, Mara

Paul Makonda

Muktasari:

Miongoni mwa kero zilizopo ni migogoro ya ardhi, uvuvi haramu, kufungwa viwanda vya samaki, ubadhirifu kwenye halmashauri na migogoro baina ya bajaji na daladala

Mikoani. Zikiwa zimepita siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan afanye uhamisho na uteuzi wa wakuu wa mikoa ya Arusha, Mwanza na Mara, wadau wa maendeleo kwenye mikoa hiyo wametaja kero zinazowasubiri wanaoenda kuiongoza mikoa hiyo wazitatue.

Miongoni mwa kero hizo ni migogoro ya ardhi, uvuvi haramu, kufungwa viwanda vya samaki, ubadhirifu kwenye halmashauri na migogoro baina ya bajaji na daladala.

Machi 31, 2024 Rais Samia aliendelea kupanga safu ya wasaidizi wake kwa kuteua, kuhamisha vituo vya kazi na kutengua huku aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha nafasi aliyokuwa akiihudumu John Mongella ambaye iliripotiwa atapangiwa kazi nyingine.

Katika mabadiliko hayo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda amehamishiwa Mwanza akichukua nafasi ya Amos Makalla ambaye taarifa ilisema atapangiwa kazi nyingine huku, Kanali Evans Alfred Mtambi akipandishwa kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga hadi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi na wadau wa maendeleo wa mikoa hiyo wamesema usafi wa mazingira, miundombinu mibovu sokoni ni kero zingine zinazotakiwa kushugulikiwa.

Yanayomsubiri Makonda Arusha

Mkoani Arusha ubadhirifu kwenye halmashauri, ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani, usafi wa mazingira, vitendo vya kihalifu ukiwamo ‘tatu mzuka’, migogoro baina ya daladala na bajaji ni vitu ambavyo Makonda anatarajiwa kwenda kuongoza safu ya viongozi kuvitokomeza.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Locken Masawe amesema wanaamini Makonda anajua matatizo yaliyopo mkoani humo kwa sababu akiwa katibu wa NEC alifanya ziara kujionea jinsi umati wa watu ulivyokuwa ukihangaika ili apate taarifa za maumivu wanayopitia.

“Kimsingi anajua matatizo mengi yalizikwa zikwa yakanyamaziwa. anapokuja haji kama mgeni. Kwa mfano sisi wafanyabiashara shida zetu ni kubwa sana sitaki kusema viongozi wengine hawajafanya ila shida zetu ni nyingi,”amesema.

Said Mtanda

 “Wafanyabiashara wanadidimia kwa kiwango kikubwa sana, tunadidimizwa na wanasiasa bila kujali tukifilisika kodi itapatikana wapi, tunaamini alikuwepo Dar es Salaam ambapo ni mji mkubwa wa kibiashara hapa patakuwa padogo kwake na tunatarajia mabadiliko makubwa.”

Masawe amesema ni matamanio yao baada ya Makonda kukabidhiwa rasmi ofisi aite makundi ya  wafanyabiashara, wakulima, wafugaji ili wamueleze yanayowasibu ikiwamo kudidimia kwa biashara, tozo kali za huduma (service levy) na  kuvunjwa maduka.

“Kwenye usafirishaji hilo ni tezi dume,haiwezekani uache daladala uweke bajaji barabarani, Mongella aliunda hadi kamati na utaratibu ukawekwa ila hautekelezwi kwa kuwa hauna faida kwa wengine, kiukweli kuna shida kwenye usafirishaji wa mjini, tunaamini Dar alipanyoosha  tunatarajia na hapa ataanyoosha,”amesema Masawe

Mkazi wa jijini Arusha, Salim Abdallah amesema wanatamani mkuu huyo mpya wa mkoa akomeshe vitendo vya ubadhirifu vinavyodaiwa kufanyika kila mara pamoja na kutatua kero ya uchafu.

“ Jiji la Arusha linunue magari ya kisasa lakini tunashangaa kuna magari ya kizamani na mji wa kitalii, tunaamini ni mfuatiliaji wa kila jambo na ana tabia ya kuingia mitaani, ataingia na akomeshe uchafu kwenye jiji letu,”amesema. 

Kassim Hamis amesema wanatamani akomeshe vitendo vya uvunjifu wa amani ikiwamo tatu mzuka na kuweka sawa makubaliano baina ya bajaji na daladala ili kila mmoja afanye kazi kwenye eneo alilopangiwa.

Mwanza wanayotarajia kwa Mtanda

Licha ya kusifia siku 382 za utendaji kazi mzuri wa Makalla ikiwamo kutembea kila kijiji cha Mkoa wa Mwanza, kusikiliza na kutatua kero tangu alipoteuliwa kwenye nyadhifa ya ukuu wa mkoa Mei 15, 2023, wakazi wanatarajia Mtanda kuboresha makusanyo ya kodi na kutatua changamoto ya machinga.

Pia, wanatarajia kutatua ujenzi holela, uvuvi haramu, viwanda vya samaki kurejea kufanya kazi, ubovu wa miundombinu na kuimarisha uchumi wa wananchi.

“Bado hatujawa na mfumo mzuri wa wafanyabiashara wadogo ndio maana ikikaribia sikukuu wanarudi mjini na masoko yaliyopo nje hayana mifumo mizuri, kwa hiyo anatakiwa kutengeneza mifumo mizuri ya ufanyaji biashara lakini pia miundombinu ya barabara ni mibovu hili nalo lipo kwake," amesema Katibu Mwenezi Mstaafu wa Chadema Wilaya ya Nyamagana, Godfrey Misana 

Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Saidi Tembo amesema wanatarajia Mtanda kutatua changamoto ya machinga kukosa maeneo ya kufanyia biashara yenye mzunguko mkubwa wa watu.
"Yapo mambo ambayo tutafikisha kwenye meza yake jambo la kwanza wafanyabiashara wadogo hatuna maeneo ambayo yapo karibu na mkusanyiko wa watu.

“Lakini mkuu wa mkoa atukubalie ombi la baadhi ya barabara kufungwa nyakati za usiku au mara moja kwa wiki kuruhusu wamachinga kufanya biashara mpaka usiku," amesema Tembo.

Mfanyabiashara wa mbogamboga na Mwenyekiti wa Soko la Igogo jijini Mwanza, Hawa Nyampangula amesema miundombinu mibovu masokoni ikiwamo kukosekana mitaro ya kupitishia maji yanayosambaa mvua zinaponyesha, kuwekwa mageti ni miongoni mwa changamoto zinazomsubiri Mtanda.

Waziri Kivuli wa Nishati na Katibu Mwenezi wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Filbert Macheyeki amesema shauku kubwa ya wananchi ni kuona changamoto ya maji, ukosefu wa ajira, ukosefu wa soko la uhakika la uvuvi na changamoto ya uchumi wa mwananchi una imarishwa.
“Sisi kama wanasiasa tunaona uteuzi huu ni maandalizi kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu lakini mambo ambayo yanamsubiri ni pamoja na changamoto ya uhaba wa,”amesema

Mdau wa uvuvi nchini, Bakari Kadabi amesema wavuvi wanahitaji mkuu wa mkoa ashughulikie changamoto ya uvuvi haramu na kufufua viwanda vya samaki ambavyo havifanyi kazi kutokana na uhaba wa samaki.
Mkazi wa Kata ya Bulyaheke, Rafael Bituro amesema jitihada za haraka zinatakiwa ili kukabiliana na uvuvi haramu ndani ya ziwa Victoria na kuoka mazalia ya samaki.

“Changamoto nyingine ni kusuasua kwa ukamilishaji wa kivuko kipya cha Kome hapa Sengerema ambacho kilikuwa kimilike Aprili lakini hakijamilika ili kuwaondolea adha wananchi wa kome wanaotumia kivuko kidogo ambacho hakikidhi mahitaji,” amesema.

Mkazi wa Kisiwa cha Kome, Amoni John amesema kingine kinachomsubiri Mtanda ni migogoro ya ardhi inayowatesa wananchi wa Sengerema ambao wanadai kudhurumiwa viwanja na mashamba yao na baadhi ya watu wenye uwezo.


Yanayomsubiri Kanali Evans Alfred Mtambi

Makamu wa Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Kilimo (TCCIA), Boniface Ndengo amesema licha ya Mkoa wa Mara kuwa na fursa nyingi za kiuchumi lakini fursa hizo hazijatumika vema kuinua uchumi wa wakazi wa mkoa huo.
"Hakuna viwanda, hakuna miradi mikubwa ukiondoa migodi lakini tuna fursa nyingi, kuna ziwa, utalii, mifugo na zingine nyingi zikitumika vema tunaweza kupata miradi ya viwanda kwenye sekta za maziwa, nyama, samaki na kuinua uchumi wa mkoa kwa ujumla,” amesema.

“Kinachonisikitisha mkoa huu umekuwa kama sehemu ya majaribio kila anayekuja akishindwa anapumzishwa, akifanya vizuri anapelekwa kwingine, ninachoweza kusema huyu mkuu wetu mpya sisi sekta binafsi tuko tayari kumpa ushirikiano tusaidiane kujenga uchumi wetu," amesema.

Abida Modest amesema suala la ukosefu wa ajira kwa vijana ndani ya mkoa huo ni jambo jingine linalomsubiria mkuu huyo wa mkoa.
"Kama unavyoona hatuna viwanda ambavyo ndivyo vingekuwa sehemu kubwa ya kutoa ajira kwa vijana, kwa vile fursa zipo naamini atatumia fursa hizo kwa ajili ya vijana na mkoa kwa jumla," amesema Abida.
Naye mkazi wa Musoma, Frank Manyama amesema suala la usalama hasa katika sekta ya uvuvi ni ajenda nyingine inayomsubiri mkuu huyo wa mkoa kwa maelezo kuwa kufungwa kwa viwanda vya samaki ndani ya mkoa huo kumetokana na uvuvi usiokuwa salama ndani ya Ziwa Victoria.