YouTube yashusha wimbo wa rapa aliyeuawa

Muktasari:

  •  Mtandao wa video wa YouTube umeshusha video iliyosambaa ya wimbo uliotolewa baada ya kuuawa kwa rapa wa Sikh nchini India, Sidhu Moose Wala kutokana na malalamiko ya serikali.


New Delhi, India (AFP). Mtandao wa video wa YouTube umeshusha video iliyosambaa ya wimbo uliotolewa baada ya kuuawa kwa rapa wa Sikh nchini India, Sidhu Moose Wala kutokana na malalamiko ya serikali.

Wimbo huo unaoitwa "SYL" unazungumzia mfereji wa Sutlej-Yamuna Link (SYL) ambao umekuwa kiini cha mgogoro wa muda mrefu kuhusu maji kati ya jimbo analotoka rapa huyo wa Sikh la Punjab na jimbo jirani la Haryana.

Wimbo huo ulioachiwa Alhamisi baada ya kifo chake, pia unagusia mambo mengine nyeti kama vile vurugu zinazoilenga jamii ya Sikh zilizolipuka mwaka 1984 na jeshi kushambulia msikiti muhimu wa Sikh uliopo Amritsar mwaka huohuo.

Video hiyo ilitazamwaka mara milioni 30 na kupata 'like' milioni 3.3 katika akaunti ya mwimbaji huyo ya YouTube kabla ya kuondolewa mwishoni mwa wiki.

"Maudhui haya hayapatikani katika eneo hili la nchi kutokana na malalamiko ya kisheria kutoka serikalini," unasema ujumbe uliowekwa katika linki ya wimbo huo.

Wimbo huo unaweza kufunguka katika nchi nyingine.

Katika baruapepe iliyotumwa AFP, msemaji wa YouTube anasema waliuondoa wimbo huo kwa sababu tu "kuheshimu sheria za ndani za nchi na masharti yetu ya huduma baada ya kuuangalia kwa makini".

Serikali haikueleza lolote licha ya kupokea maswali.

Familia ya Moose Wala imeelezea kushushwa kwa wimbo huo kuwa "si haki" na kuiomba serikali kuondoa malalamiko yake, vyombo vya habari vya India vimeripoti.

"Wanaweza kuupiga marufu wimbo, lakini hawawezi kumuondoa Sidhu mioyoni mwa watu. Tutajadili uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria na wanasheria," alisema mjomba wake, Chamkaur Singh alipoongea na gazeti la Hindustan Times.

Moose Wala -- ambaye pia anajulikana kwa jina la kuzaliwa la Shubhdeep Singh Sidhu -- aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya gari lake katika jimbo la kaskazini la Punjab mwezi uliopita.

Msanii huyo mwenye miaka 28 alikuwa maarufu nchini India na katika jamii ya Punjabi nje ya nchi, hasa Canada na Uingereza.