Zingatia matumizi sahihi ya taulo kuepuka magonjwa

Zingatia matumizi sahihi ya taulo kuepuka magonjwa

Muktasari:

  • Unajua madhara unayoweza kuyapata endapo utachangia taulo mmoja na mtu mwingine? Usikubali kutumia taulo moja na mtu mwingine hata kama ni familia yako, ni hatari kwa afya, wataalamu wa afya wanaeleza.


Unajua madhara unayoweza kuyapata endapo utachangia taulo mmoja na mtu mwingine? Usikubali kutumia taulo moja na mtu mwingine hata kama ni familia yako, ni hatari kwa afya, wataalamu wa afya wanaeleza.

Pia wanasema kama taulo halitahifadhiwa katika mazingira safi na kutotumika kwa umakini, linaweza kusababisha magonjwa ambayo ni hatari kwa afya yako.

Taulo linabeba fangasi na bakteria hatari ambao husababisha magonjwa, yakiwemo ya ngozi, maambukizi kwenye mfumo wa njia ya mkojo (UTI) na muwasho sehemu za siri.

Bakteria hao na fangasi wanaweza kusababisha mwili kuwasha na ngozi kuwa na magamba, malengelenge, ngozi kubadilika na kuwa nyekundu na wakati mwingine mtu anatokewa na uvimbe na vipele vilivyojaa maji, hali inayosababisha kupata homa kali hadi kuishiwa nguvu.

Dk Warles Lwabukuna kutoka hospitali ya Hubert Kairuki Memorial (HKMH) anasema kuna magonjwa mengi yanayoweza kuenezwa kwa kutumia taulo.

“Hatuwezi kusema eti tuache kutumia taulo, la hasha! Tunatakiwa tutumie taulo vizuri kwa kuzingatia usafi,” anasema.

Dk Lwabukuna anaeleza ili taulo litumike kwa usalama zaidi, kuna mambo yanatakiwa kufanyika kwa mtu anayetumia.

Mtaalamu huyo ambaye amebobea katika magonjwa yasiyoambukiza anasema suala la usafi ni muhumu kuzingatiwa, kwa sababu taulo inaweza kueneza magonjwa.

“Magonjwa hayo yanaenea kutoka katika taulo ambalo mtu amejifutia mwenye ugonjwa fulani labda wa ngozi, viini vyake vitabaki katika taulo hilo na muda mwingine akijifutia anaweza kupata ugonjwa huo,” anafafanua.

Anasema kutokana na taulo lenyewe na sehemu linapowekwa, inawezekana viini vya magonjwa vikazaliana katika taulo hilo.

Usafi wa taulo

Dk Lwabukuna ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Hubert Kairuki Memorial anasema taulo linatakiwa kufuliwa na maji ya moto kila baada ya siku tatu au siku tatu kwa wiki.

“Tunasisitiza utumiaji wa taulo lazima uendane na usafi na ni vizuri taulo liwe linafuliwa kwa maji ya moto walau kila baada vya siku tatu, kwa sababu kuna watu wengine wanafua taulo kwa wiki mara moja, lakini kila siku analitumia kwa kujifutia na kuliweka bafuni likiwa bichi hivyo hivyo.

“Mtu anajifutia taulo asubuhi analiacha bafuni likiwa bichi, akirudi tena jioni akioga anajifutia. Hii ni hatari kwa afya,” anasema.

Anabainisha kuwa taulo linapofuliwa na kukaushwa vizuri juani, linapokauka linapaswa kupigwa pasi ili kuua vijidudu mbalimbali, ikiwemo hao bakteria.

“Ubichibichi wa taulo unavutia vimelea vya vijidudu vya magonjwa, mfano bakteria na fangasi ambao ndio viini vya magonjwa ambayo yamekuwa ni sababu ya kutokea kwa matatizo ya kiafya, ikiwemo ugonjwa wa UTI,” anafafanua.

Pia anasema jambo la msingi ni kuhakikisha taulo halina unyevunyevu kabla ya kutumika na baada ya kutumika lianike juani.

Mtaalamu huyo wa magonjwa ya ndani anasema mfano wa bakteria na fangasi wanaoleta madhara kwa binadamu ni staphylococcus aureus, streptococcus na E.coli.

“Fangasi aina staphylococcus wanapoathiri sehemu ya ngozi, huifanya ngozi kubadilika rangi na kuwa nyekundu, kuwa na vipele, malengelenge, kuwashwa na wakati mwingine ngozi ya mgonjwa inakuwa imelika kwa sababu ya ugonjwa huo.

“Ili kuepuka na ugonjwa huu wa staphylococcus, unatakiwa kufua taulo yako kwa maji ya moto, halafu ikishakauka unaipiga pasi” anasema.

Bakteria mwingine anayeeneza magonjwa ni streptococcus ambaye husababisha ugonjwa wa ngozi na mara nyingi ugonjwa huo unafanana na majipu kwenye ngozi.

Kwa upande wa bakteria aina ya E.coli, wao hueneza ugonjwa wa UTI, kama mtu atatumia taulo mbichi ambayo ina vijidudu ya ugonjwa huo.

Anasema si bakteria aina ya E.coli wanaweza kukaa kwenye taulo, pia hata kwenye sabuni iliyopo bafuni wanaweza kukaa na hivyo kusababisha madhara kwa binadamu.

“Huyu bakteria aina ya E.coli anaishi katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa binadamu na hana shida akiwa ndani kwa sababu anasaidia kuzalisha baadhi ya vitamini B12, lakini akihama kutoka katika mazingira yake huleta madhara na hutoka kwa njia ya haja kubwa.

“Akiwa katika mfumo wa njia ya mkojo kusababisha ugonjwa wa UTI na hiyo ni kutokana na watu kujifutia taulo mwili mzima hadi katika sehemu za siri,” anafafanua Dk Lwabukuna. Pia matumizi ya taulo bichi yanaweza kusababisha fangasi kama vile dermatophytes (ringworm). Baadhi ya fangasi kwa ujumla ni trichophyton, microsporum, epidermophyton na candida, ambao husababisha fangasi.

“Mfano wa magonjwa yanayosababishwa na fangasi ambao huenezwa kwa njia ya taulo ni aina ya candida,” anasema.

Anasema fangasi aina ya candida huharibu ngozi na wakati mwingine aina hiyo ya fangasi hujitokeza pale kinga ya mwili inaposhuka na kueleza kuwa watu walio katika hatari ya kupata fangasi hao ni wajawazito, watu wenye umri mkubwa, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wenye magonjwa yasiyoambukizwa kama kisukari, watu wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Nini kifanyike

Dk Lwabukuna anasisitiza watu waepuke kuchangia taulo na mtu mwingine na kila mtu awe na taulo lake.

Pia anasema jamii ina wajibu wa kuzingatia usafi wa taulo, kwani kila unapotumia hakikisha unalianika juani likauke, ili kuepusha bakteria na fangasi ambao hujihifadhi katika taulo bichi. Pia watu wawe na utamaduni wa kufua taulo kila baada ya siku tatu au kwa wiki mara tatu kwa maji ya moto na likikauka lipigwe pasi kabla ya kutumika.

Wakati Dk Lwabukuna akieleza hayo, Profesa John Oxford kutoka chuo kikuu cha Queen Mary University nchini Uingereza ananukuliwa na mtandao wa BBC akisema hashauri mtu kuchangia taulo moja na mtu mwingine kwa sababu taulo ni kitu chenye utata.

Profesa Oxford anasema taulo lililokaushwa vizuri na kupigwa pasi ni salama kwa mtumiaji.

“Unyevunyevu uliopo katika taulo ni mazingira mazuri kwa viini vya magonjwa kuzaliana, hivyo hata kama kila mtu atakuwa na anatumia taulo lake, msisitizo uliopo ni kulifua kila baada ya siku mbili au tatu na anapomaliza kujifutia maji alianike juani,” anasema Profesa Oxford.

Mtaalamu huyo anaeleza hata sabuni ya kipande inayowekwa bafuni nayo si salama, kwani inabeba vimelea vya maambukizi ya bakteria.

“Bakteria wanaweza kukaa kwenye sabuni ya kuogea na kuhama kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, kwa mfano bakteria aina ya E.coli huishi maeneo hayo.

Anashauri matumizi ya sabuni ya maji iliyohifadhiwa katika chupa ni bora zaidi kuliko sabuni ya kipande kwa matumizi ya kifamilia.