Zitto akomaa na Sh52 bilioni katika akaunti ya DPP

Zitto akomaa na Sh52 bilioni katika akaunti ya DPP

Muktasari:

  • Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume ya majaji kupitia malalamiko ya watu ambao walilipishwa fedha kwa mtindo wa kukiri makosa na kulipa fedha serikalini.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume ya majaji kupitia malalamiko ya watu ambao walilipishwa fedha kwa mtindo wa kukiri makosa na kulipa fedha serikalini.

Kafuatia hatua hiyo, Zitto aliyekuwa anachambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amesema wote watakaobainika kuwa katika makubaliano hayo na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) walionewa, warejeshewe fedha zao na rekodi zao za jinai zifutwe kisheria.

CAG amebainisha katika ripoti yake ya mwaka 2019/2020 kwamba amekuta fedha Sh51.52 bilioni kwenye akaunti ya DPP ambazo zilipatikana kutokana na kesi zilizomalizika katika mahakama mbalimbali kwa kipindi cha miaka sita iliyopita.

Kutokana na fedha hizo, Zitto alieleza kwamba, fedha hizo hazikutumika kwa sababu ya kukosekana kwa sheria na kanuni zinazoelekeza matumizi yake.

Alisema fedha hizo zilipatikana baada ya DPP kutaifisha fedha za watu kabla ya kuwepo kwa sheria ya ‘plea bargain.’

Matumizi nje ya mfuko wa hazina

Zitto alibainisha kuwa hoja zenye mashaka zilizoibuliwa na CAG zina thamani ya Sh3.6 trilioni na Dola za Marekani 596 milioni (Sh1.375 trilioni), ambacho kati yake Sh2.2 trilioni hazikupita mfuko mkuu wa hazina.

Katika ripoti yake CAG Charles Kichere anasema “Nilibaini kuendelea kuwapo kwa makusanyo yasiyohesabiwa Mfuko Mkuu. Hii ni pamoja na Makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya Sh 132.08 bilioni na Sh 2,025.67 bilioni zilizopelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo. Hali hii inasababishwa na kutotambuliwa kwa makusanyo na matumizi yasiyo taslimu (Dummy transaction) katika Mfuko Mkuu wa Serikali.”

Akichambua ripoti hiyo Dar es Salaam jana, Zitto alisema kwa kutopita mfuko mkuu wa hazina, matumizi hayo hayakuidhinishwa na CAG ambaye Katiba inampa mamlaka ya kufanya hivyo.

Zitto alisema katika uchambuzi waliofanya mwaka jana pia walionye

sha kuna fedha za Serikali ambazo zilitumika bila kupitia mfumo mkuu wa hazina kama Katiba inavyotaka.

Alisema mwaka 2018/19 Serikali ilitumia Sh1.7 trilioni bila kupita kwenye mfuko huo.

Alisema baadhi ya fedha hizo zinatokana na mikopo kutoka nje (Sh1.2 trilioni) ambapo CAG alisema zilikwenda kulipia miradi ya maendeleo moja kwa moja. Alisema mwaka 2019/2020 jumla ya Sh2.2 trilioni pia hazikuhesabiwa katika mfuko mkuu.

“Katiba ya nchi imevunjwa kwa Serikali kupokea fedha na kuzitumia bila kwanza kupita kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali,” alisema Zitto huku akinukuu ibara ya 135(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema ibara ya 136(3) inamtaka CAG kuidhinisha kutolewa kwa fedha kutoka mfuko mkuu wa hazina. Aliongeza kuwa fedha ambazo zinatumika bila kupita mfumo mkuu zinakosa idhini ya CAG na hivyo zinaweza kuwa zinatumika kinyume cha bajeti na kinyume cha sheria.

Alisema jambo hilo limekuwa likijirudia kwa miaka mitatu ambapo mwaka 2017/18, Sh800 bilioni hazikupitia mfuko mkuu wakati mwaka 2018/19 zikiwa ni Sh1.7 trilioni na mwaka 2019/20 zikiwa ni Sh2.2 trilioni.


Hasara ya TPDC

Zitto alifafanua kwamba CAG ameonyesha kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) lina mtaji hasi wa Sh332 bilioni ambao umesababishwa na mkopo ambao Serikali ilichukua kutoka China kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

“Tunapendekeza pia Serikali iliache shirika la TPDC lifanye kazi yake kibiashara na kurudi katika mpango kabambe wa kuzalisha na kusambaza umeme ili uwekezaji uliofanywa katika bomba la gesi uwe na manufaa kwa Taifa letu,” alisema Zitto.


Upungufu wa dawa

Kuhusu hoja ya upungufu wa dawa, Zitto alisema CAG amebainisha kuwa Bohari ya Madawa nchini (MSD) ambayo ndio shirika lenye jukumu la manunuzi yote ya dawa hapa Tanzania, inaidai Serikali jumla ya Sh257 bilioni.

“Tunapendekeza Serikali ilipe deni lote la MSD, na pia Serikali itoe mtaji kamilifu kwa MSD ili iweze kujitegemea kibiashara katika shughuli ya usambazaji wa dawa kwa wananchi wetu,” alisema Zitto.


Hoja nyingine

Hoja nyingine alizozijadili Zitto katika uchambuzi wake ni pamoja na hasara kwa shirika la ndege la ATCL ambapo alisema CAG hakueleza katika ripoti yake ilikuwaje shirika ambalo linapata hasara licha ya ruzuku ya Serikali, liliweza kulipa gawio kwa Serikali.

Pia, alisema uchambuzi wao umebaini kwamba, mwaka 2019/2020 madai dhidi ya Serikali yalikuwa Sh3.1 trilioni kutoka Sh2.7 trilioni mwaka 2018/19. Alisema madai ya wazabuni dhidi ya Serikali yaliongezeka kwa asilimia 15 kutoka mwaka uliopita.

Mwanasiasa huyo alisema makusanyo yamepungua ambapo kwa mujibu wa CAG katika ripoti yake, uwiano wa makusanyo ya kodi kwa Pato la Taifa ulikuwa asilimia 12.1 tu ikiwa ni ongezeko dogo kutoka asilimia 11.6 mwaka 2018/19. Alisema kiwango hicho bado kiko chini.

Kwa upande wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Zitto alishauri CAG afanye ukaguzi maalumu wa miradi yote mikubwa inayotekelezwa na TPA ili kupata uhalisia wa ubadhirifu katika mamlaka hiyo. Wakati wa ukaguzi huo, alipendekeza Bodi ya Bandari ivunjwe na kuundwa upya.