Zitto ataka wananchi wasilazimishwe kuchagua kiongozi wasiyemtaka

Zitto ataka wananchi wasilazimishwe kuchagua kiongozi wasiyemtaka

Muktasari:

  • Zitto amewataka wananchi wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma kumchagua mgombeaanayejua kero zao ili iwe rahisi kuzitatua.

Buhigwe. Wananchi jimboni Buhigwe mkoani Kigoma wametakiwa kuwachagua viongozi watakaotatua kero zao ili wapate maendeleo wanayokusudiwa.

Hayo yamesemwa jana Mei 9, 2021na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye ni ameyasema hayo wakati akimnadi mgombea ubunge katika jimbo la Buhigwe, Garula Kudra katika Kata ya Mwayaya, ambapo amewataka wananchi kutolazimishwa kuchagua kiongozi wasiyemtaka.

Amesema wanachi wanatakiwa kutambua kuwa dunia inabadilika kila kukicha na inahitaji watu wanaoweza kushirikiana wao, huku wakifahamu maendeleo ya Jimbo lao ni yao wenyewe.

“Wapo watu wanaowatisha na kuwalazimisha wananchi kutowapigia kura viongozi wa vyama vya upinzani kwa madai hawezi kuleta maendeleo, sasa nataka niwambie kuwa maendeleo hayawezi kuletwa na chama bali viongozi bora wanapatika kwenye vyama hivyo.

“Mtu bora anaweza kupatikana kwenye chama hata kama ni kidogo sana hivyo Wananchi amkeni, jitambueni zipimeni  kauli za watu na vyama vyao,” amesema Zitto.


Jimbo hilo linafanya uchaguzi Mei 16, 2021 baada ya aliyekuwa mbunge, Dk Philip Mpango kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.


Kwa upande wake mgombea ubunge, Kudra amesema iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo atapambana kutatua kero za jimbo hilo akisema kuwa anazijua.


“Kuna Vituo vya afya, lakini zipo kata nyingi ambazo wananchi wanatembea mwendo mrefu kufuata huduma hizo, kutokana na hali hiyo nitahakikisha kero ya kutembea mwendo mrefu inakwisha,” amesema Kudra.


Ameongeza: “Ninatambua zipo kero kama upatikanaji wa maji safi, elimu masoko ya bidhaa za kilimo kukosa masoko. Nataka kuona wakulima wapate tija katika kilimo kulingana na gharama wanazozitumia.”