Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zitto: Natamani kuwa Rais Tanzania

Muktasari:

  • “Natamani siku moja nipate nafasi ya kuiongoza nchi yangu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”


Mwanza. “Natamani siku moja nipate nafasi ya kuiongoza nchi yangu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Hiyo ni kauli ya Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe wakati wa mahojiano maalum na Mwananchi yaliyofanyika jijini Mwanza ambako viongozi wakuu wa chama hicho wamepiga kambi ya kampeni ya kuimarisha uhai wa chama, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka minane ya chama hicho.

Akijibu swali kuhusu tetesi za yeye kuhusishwa na harakati za kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025, Zitto alisema ni imani yake kuwa anao uwezo wa kuliongoza Taifa katika nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi nchini kutokana na uwezo, maarifa na uzoefu alioupata katika ulingo wa siasa alioingia tangu akiwa mwanafunzi.

“Nimesema siku zote kwamba urais nautaka. Siwezi kusema moja kwa moja kwamba nitagombea mwaka 2025, kwa sababu uamuzi huo unatokana na kwanza kudra za Mungu na pia chama na wananchi ambao ndio lazima watoe ridhaa na dhamana ya kuiongoza nchi katika nafasi hiyo,” alisema Zitto.


Vyama vya upinzani kuungana

Pamoja na kupata ridhaa ya chama chake, kiongozi huyo aliyeanzia harakati za siasa akiwa Chadema, alisema kuna haja ya vyama vya upinzani nchini, kuunganisha nguvu kukabiliana na chama tawala (CCM).

“Kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha Watanzania kuvitaka vyama vya upinzani kushirikiana ili kuweza kupambana dhidi ya CCM; yawezekana tukakubaliana kushirikiana (kusimamisha mgombea mmoja) na nisiwe mimi; au tukakubaliana niwe mimi. Yote haya ni mambo ya kimjadala huwezi kupata majibu yake sasa hivi,” alisema

Alisema kutokana na ukweli kwamba ushindi kwenye sanduku la kura unahitaji uungwaji mkono wa umma wa wapigakura, viongozi wa ACT-Wazalendo wameweka kambi ya karibu mwezi mzima mkoani Mwanza kuongeza nguvu na ushawishi wa kisiasa katika makundi na rika zote mkoani humo na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa yenye wapigakura wengi.

“Lengo ni kujijenga kama taasisi katika matawi, kata na majimbo yote mkoani Mwanza kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025,” alisema


Tume huru ya uchaguzi na Katiba Mpya

Akizungumzia msimamo wa chama chake wa kupigania kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya Katiba Mpya, Zitto alisema uamuzi huo haukusudii kupingana na vyama vingine vya upinzani, bali umezingatia kile kinachoweza kupatikana kwa haraka.

Alivisihi vyama vingine vya upinzani, wanaharakati na wapenda demokrasia nchini kudai kwanza tume huru kwa kuanza kushinikiza mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ili iwezeshe Taifa kuwa na chaguzi huru zitakazowapa fursa wananchi siyo tu kuwachagua viongozi wanaowataka, bali pia tume kuwa na uhuru wa kutangaza waliochaguliwa na kushinda kwa kura za wananchi.

Alisema bila kuwa na tume huru inayosimamia chaguzi huru, itakuwa ndoto kudai na kupata Katiba Mpya.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mbunge katika majimbo ya mkoani Kigoma, aliwaomba wadau wa siasa nchini kuunga mkono majadiliano yanaoendelea kuhusu maboresho ya siasa, kwa sababu ni moja ya njia muhimu ya kuondoa changamoto na matatizo ya kisiasa yaliyopo nchini ikiwemo madai ya tume huru ya uchaguzi na katiba mpya.

“Hatuandiki katiba ya chama kimoja, tuaandika ya Watanzania wote, kwa hiyo lazima katiba iendane na mazingira ambayo watu wanakuja pamoja. Lazima tukae kwenye meza ya maridhiano, vyama vya siasa, viongozi, wanasiasa na wasio wanasiasa wakae wajadiliane na kukubaliana,” alisema.

Alisema ACT-Wazalendo inatarajia kuandaa kongamano la kitaifa jijini Mwanza Mei 7 ikiwa ni utekelezaji wa lengo la kupata tume huru ya uchaguzi.


Matarajio 2025

“ACT-Wazalendo tuna matarajio makubwa katika nafasi zote za uongozi kwa kuanza na uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunaendesha kampeni hizi kwa ajili ya kujiimarisha; ni matumaini yetu kwamba tutakifikisha chama kila kona ya Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema.

Alisema chama hicho kinatekeleza mikakati ya miaka mitatu ya kujitanua na kukita mizizi kila kona ya nchi.


Wachambuzi watoa neno

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu mikakati ya ACT-Wazalendo ya kujiimarisha kisiasa na ndoto ya Zitto ya urais, wachambuzi wa masuala ya kisiasa walisema kila chama chenye usajili wa kudumu kina fursa ya kusimamisha wagombea.

Akimzungumzia Zitto katika nafasi ya urais, wakili Majid Kangile wa jijini Mwanza alisema; “Ni haki yake kikatiba kugombea; anazo sifa za kuwania nafasi hiyo. Jambo muhimu ni wapigakura kumpima kwa kuangalia sera ya chama chake, utendaji wake katika nafasi alizowahi kushika ikiwemo ubunge na vipaumbele vya wapigakura.”

Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema mwanasiasa huyo na vijana wengine walioko kwenye ulingo wa siasa, wanaweza kuongoza Taifa wakipewa nafasi kutokana na uzoefu wao kisiasa.