Zitto: Uchaguzi mdogo majimbo ya Kigoma kupima joto la Rais Samia

Zitto: Uchaguzi mdogo majimbo ya Kigoma kupima joto la Rais Samia

Muktasari:

  • Wakati baadhi ya vyama vya upinzani, kikiwamo Chadema vikitangaza kutoshiriki uchaguzi mdogo wa majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma, chama cha ACT - Wazalendo kimejitosa kukabiliana na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wakati baadhi ya vyama vya upinzani, kikiwamo Chadema vikitangaza kutoshiriki uchaguzi mdogo wa majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma, chama cha ACT - Wazalendo kimejitosa kukabiliana na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Chadema kwa upande wao wametoa sababu ya kutoshiriki uchaguzi huo kuwa ni pamoja na kutokuwa na imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Hata hivyo, akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi wiki iliyopita, Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe alisema wameamua kushiriki ili kupima kama Rais mpya, Samia Suluhu Hassan ni muumini wa demokrasia.

“ACT Wazalendo tumeona nafasi ya uchaguzi wa Muhambwe ni ya kumjaribu Rais Samia kama ni muumini wa demokrasia au atakuwa kama mtangulizi wake,” amesema Zitto.

Amesema sababu ya kutokuwa na imani na NEC haina mashiko kwa sababu vyama vya upinzani vimeshiriki chaguzi na tume hiyohiyo ikiwepo.

“Ni hoja nzuri, lakini turudi nyuma, tangu mwaka 1995 kwani tume ilikuwa tofauti? 2000 pia, ilikuwa tofauti? 2005, 2010, 2015 miaka yote hiyo, tume ilikuwa tofauti? 2020 tena Rais alikuwa John Magufuli na tulishiriki uchaguzi. Kwa hiyo sioni kama ni hoja ya kutoshiriki uchaguzi. Inawezekana kuna suala la kujiandaa, inawezekana ni fedha, inawezekana ni eneo ambalo sisi hatuna nguvu na sababu nyingine. Siwezi kuingilia uamuzi wa vyama vingine, lakini sisi tumeona kuna mabadiliko makubwa,” amesema Zitto.

Akitoa mifano kushibisha hoja yake, kiongozi huyo anasema ameshiriki chaguzi mara nne na kutangazwa mshindi mara tatu na tume hiyohiyo.

“Katika hizi mara tatu kulikuwa na marais wawili, mwaka 2005 alikuwepo Rais Benjamin Mkapa na mwaka 2010 na 2015 alikuwa Rais Jakaya Kikwete. Tumekwenda na nimeshinda kirahisi kabisa na sikuwa peke yangu, walikuwepo wengine.

“Mtakumbuka tumeshinda uchaguzi mdogo mwaka 2013, Mzee John Cheyo alishinda uchaguzi mdogo mwaka 1997, Augustine Mrema alishinda uchaguzi mdogo wa mwaka 1998, uchaguzi ambao ulikuwa na matatizo makubwa kabisa, akagombea Temeke na akatangazwa mshindi na tume hiyohiyo na akaenda bungeni. “Kwa hiyo nadhani kwetu ACT, Muhambwe na Buhigwe ni maeneo ambayo nchi na jumuiya ya kimataifa wataona kama Tanzania chini ya Rais Samia itaheshimu misingi ya demokrasia au itaendelea na yaleyale?” amesema. Amesisitiza kuwa haiwezekani kutambua ubaya na uzuri wa uchaguzi huo kama vyama havitashiriki.

“Usiposhiriki na mgombea wa CCM akatangazwa mshindi utasema nini? Lakini mkishiriki halafu mkaenguliwa mna cha kusema. Mkishiriki mambo yakaenda shwari hadi siku ya kupiga kura fujo zikatotokea, mna cha kusema, mkishiriki mkashinda na mkatangazwa, mtasema tunaona kuna mabadiliko.”

Alipoulizwa sababu ya viongozi na makada wa vyama vya upinzani kuongoza kwa kumsifia Rais Samia, Zitto amesema baadhi ya watu ndani ya CCM na Serikali hawakuwa tayari kumwambia ukweli Rais aliyekuwepo. “Siasa nzuri ni zile ambazo unaeleza kile unachokiamini na ukakubali gharama zake. Na hali hii haiko Tanzania tu, kwa sababu hata Rais Samia alikuwa Makamu wa Rais wa Magufuli, iweje leo aone vikosi kazi vya kukusanya kodi havifai? Kwa nini hakuviona wakati ule?” amehoji. Ameendelea kutoa mfano aliyekuwa Rais wa Urusi, Joseph Stalin alipofariki dunia, Nikita Khrushchev alishika nafasi yake, lakini alianza kukosoa sera za mtangulizi wake. Hivyo hili si la ajabu kwa watu kuona kama Rais Samia anajaribu kusawazisha pale palipokosewa na mtangulizi wake na kuimarisha pale alipofanya vema. “Stalin alikuwa Rais katili na aliua watu sana, sasa Nikita alianza kufanya mabadiliko. Mmoja wa wajumbe wa kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Urusi, akamwandikia ujumbe kwenye kikaratasi wakiwa kwenye kikao, akamwambia; “Wewe si ulikuwa namba mbili wa Stalin, sasa unataka kuyasema mambo yote aliyokuwa akifanya, unayakosoa.” Mjumbe huyo hakuandika jina lake.

“Khrushchev alikisoma kile kikaratasi kwenye kikao, kisha akasema; ‘Hicho kilichokufanya usiandike jina lako, ndicho na mimi kilinifanya nisikosoe’. Sisi tuangalie mbele. Kwa hiyo na mimi nashauri tuangalie mbele.”

Utawala wa Rais Samia

Akizungumzia utawala wa Rais Samia, Zitto anasema japo wamekuwa wakimsifia kwa kuleta matumaini makubwa, Watanzania hawapaswi kubweteka.

“Ninyi pia ni mashahidi, tangu tumempata Rais Samia kumekuwa na matumaini makubwa ya wananchi. Mimi nimetoka nje ya Dar es Salaam, juzi nilikuwa Mwanza, jana nilikuwa Kibondo, Kigoma (wiki iliyopita), unaona kuna mabadiliko makubwa. Matumaini kwa watu ni makubwa.

“Naamini kabisa Rais Samia hatawaangusha Watanzania, bali mabadiliko haya yatakuwa ya kiuchumi na mabadiliko ya kutenda haki. Kama mlivyosikia, amesema hataki dhuluma. Ina maana katika maisha yake yote anasema hataki dhuluma,” anasema Zitto.

Huku akitoa mfano wa wafanyabiashara wa fedha za kigeni jijini Arusha waliotakiwa kusalimisha fedha zao Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Zitto alisema Rais Samia amewatoa Watanzania kwenye enzi za kudhulumiwa na kunyimwa uhuru wa maoni.

“Inatia matumaini makubwa ya kuondokana na miaka ya watu kudhulumiwa bila kusema chochote. Yaani tulifikia wakati nchi hii unapigwa halafu unazuiwa usilie. Ukilia unaulizwa kwa nini unalia?” alisema Zitto.

Alisema kwa ujumla Rais Samia amependezesha makundi yote ya Watanzania wakiwamo wananchi waliokuwa wakilalamikia ukata wa fedha. “Alipokuwa akihutubia alisema watu wanalalamika hawana fedha mifukoni, kwa hiyo anakwenda kujibu kilio cha wananchi hao.” Akifafanua zaidi kuhusu matumaini yake, Zitto alisema katika uchaguzi mdogo wa Muhambwe mkoani Kigoma chama chake hakijapata misukosuko waliyozoea kuipata. “Zamani kuchukua fomu tu ya kugombea, utakuta msimamizi amefunga ofisi, lakini tumekwenda msimamizi wa uchaguzi anamsubiri mgombea. “Tumewekewa pingamizi na CCM, katika hali ya kawaida tulikuwa tunajua tumeshaenguliwa. CCM wanaweka pingamizi bila kuwa wameongea na Mkurugenzi? Tukajibu kwa taratibu zinazotakiwa, halafu Mkurugenzi akatupilia mbali pingamizi la CCM. Ni kitu ambacho unajiuliza kama kweli yanatokea? Kwa hiyo ni matumaini makubwa sana. Lakini haya matumaini yasituondoe kwenye hali kwamba mabadiliko haya si ya kimfumo bali sasa tunahitaji mabadiliko ya kimfumo,” amesema kiongozi huyo.

Aidha, alisema ni jambo la kujivunia kwa Watanzania kuona viongozi wakibadilisha madaraka kwa amani tofauti na nchi nyingine ambazo hukumbwa na misukosuko.

Lakini hata hivyo, ninarudia tena; “Tusibweteke, kwa sababu ni mapema mno. Huu ni mwanzo tu, hatujaona shughuli yoyote inayohusisha sheria ikiwa imefanyika.” Amesisitiza uwapo wa mabadiliko ya kimfumo na ametolea mfano wa kauli ya Rais Samia kuhusu kufunguliwa kwa vyombo vya habari ilivyochukuliwa na watendaji wa Serikali.

“Tulimsikia Rais akisema vyombo vya habari vifunguliwe, Katibu Mkuu wa Wizara akasema ni online (mitandao) peke yake, Mkurugenzi wa Habari Maelezo mpya naye akasema ni online peke yake, Waziri akaja akasema wenye magazeti waende ofisini kwake wakajadiliane.

“Yote haya yanaonyesha kuwa tunahitaji mfumo wa kisheria kwa sababu yanaweza kubadilika,” alimalizia kiongozi huyo.