Zombe, wenzake wanane wanaswa, wanne waponyoka (61)

Zombe, wenzake wanane wanaswa, wanne waponyoka (61)

Muktasari:

  • Katika sehemu ya 60 ya simulizi hii ya Kesi ya Zombe, tuliona waendesha mashtaka walivyojibu hoja za mawakili wa utetezi, ambapo waliieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa kwa ushahidi waliouwasilisha mahakamani, washtakiwa wakinyamaza au wakijitetea wana kesi ya kujibu.
  • Pia upande wa mashtaka ulichanganua ushahidi huo kuonesha jinsi ulivyomgusa kila mshtakiwa kiasi cha kumfanya alazimike kujitetea kwa mashtaka hayo.
  • Leo katika simulizi hii tataangalia uamuzi wa mahakama na je, nini ambacho mahakama ilikiamua na ilifikiaje uamuzi huo? Endelea na sehemu ya 61 ya simulizi hii.

Katika sehemu ya 60 ya simulizi hii ya Kesi ya Zombe, tuliona waendesha mashtaka walivyojibu hoja za mawakili wa utetezi, ambapo waliieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa kwa ushahidi waliouwasilisha mahakamani, washtakiwa wakinyamaza au wakijitetea wana kesi ya kujibu.

Pia upande wa mashtaka ulichanganua ushahidi huo kuonesha jinsi ulivyomgusa kila mshtakiwa kiasi cha kumfanya alazimike kujitetea kwa mashtaka hayo.

Leo katika simulizi hii tataangalia uamuzi wa mahakama na je, nini ambacho mahakama ilikiamua na ilifikiaje uamuzi huo? Endelea na sehemu ya 61 ya simulizi hii.

Uamuzi wa mahakama

Baada ya malumbano ya hoja za awali kutoka kwa mawakili wa pande zote, hatimaye mahakama ilitoa uamuzi wake uliokuwa ukisubiriwa sana na wadau wote wa kesi hiyo.

Ilikuwa ni Jumatatu ya Februari 9, 2009 wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilipotoa uamuzi uliotegua kitendawili cha kwanza cha hatima ya washtakiwa katika kesi hiyo.

Huo ulikuwa ni uamuzi wa kama washtakiwa wote au baadhi yao katika kesi hiyo hawana au wana kesi ya kujibu kutegemeana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.

Siku hiyo Jaji Massati aliingia mahakamani saa 4.26 ambapo baada ya kimya cha dakika takribani sita huku akipekuapekua jalada la kesi hiyo alianza kusoma uamuzi.

Kwanza alianza kufanya rejea ya hoja za upande wa utetezi walizoziwasilisha kuishawishi mahakama kuwa washtakiwa hawakuwa na kesi ya kujibu na kisha akafanya rejea ya majibu ya hoja hizo kutoka upande wa mashtaka.

Katika uamuzi wake, Jaji Massati aliwaachia huru washtakiwa watatu baada ya kujiridhisha kuwa hawana kesi ya kujibu, kwani hakukuwa na ushahidi wa kuwashtaki.

Walioachiwa huru katika hatua hiyo ni PC Noel Leonard, aliyekuwa mshtakiwa wa nne, CP Moris Nyangelela, mshtakiwa wa sita na CPL Felix Cedrick, mshtakiwa wa nane.

Zombe na wengine tisa walinaswa, baada ya mahakama kuridhika kuwa walikuwa na kesi ya kujibu. Kutokana na uamuzi huo, Zombe alitaka aanze kujitetea siku hiyohiyo, lakini Jaji Massati alimgomea.


Sababu za Zombe kunaswa

Katika uamuzi wake, Jaji Massati alisema kuwa Zombe kwa nafasi aliyokuwa nayo ya kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) alikuwa katika nafasi nzuri ya kujua kila tukio la uhalifu lililokuwa likiendelea jijini na hata kutoa maelekezo au maagizo ambayo ni sahihi.

Sababu nyingine aliyoibainisha Jaji Massati kumfanya Zombe awe na kesi ya kujibu ni kitendo cha kuwaita ofisini kwake washtakiwa wengine walioshiriki katika tukio hilo la kuwakamata marehemu ili kuwapongeza.

“Kitendo hiki kinaonesha kuwa alikuwa akijua kilichotendeka kwa marehemu. Kwa mazingira kama haya ni muhimu apewe nafasi ya kuieleza mahakama kilichotokea,” alisema Jaji Massati.

Jaji Massati alisema kitendo cha Zombe kufika katika kituo cha Polisi Urafiki usiku wa tukio hilo na kuulizia pesa zilizochukuliwa na washtakiwa kutoka kwa marehemu, ambapo alikasirika baada ya kuambiwa kuwa zilikuwa zimepungua, inaonesha kuwa alikuwa na mawasiliano na washtakiwa wengine waliowakamata marehemu.

Kitendo cha kuwaweka ndani ndugu wa marehemu waliokwenda kutambua miili ya marehemu katika Hospitali ya Muhimbili, Venance Mchami ambaye ni shahidi wa nne katika kesi hiyo na Emmanuel Likonga, huku akiwatishia kuwaua na kuwataka wampelekee Benadetha Ngonyani (shahidi wa pili), ni sababu nyingine iliyomfanya awe na kesi ya kujibu.

Kwa upande wa Bageni, Jaji Massati alisema kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuwa ndiye alikuwa kiongozi wa msafara uliokwenda kuwakamata marehemu huko Sinza, anapaswa aieleze mahakama juu ya majibizano ya risasi kati yao (Polisi) na marehemu, jinsi yalivyotokea.

Kwa mshtakiwa wa tatu, ASP Makelle aliridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani kuwa aliwakamata marehemu wakiwa hai na kuwafunga pingu na kisha kumtaarifu mkuu wake wa kituo kuwa wamewakamata majambazi wakiwa na pesa na silaha kabla ya vifo vyao.

Kwa sababu hiyo, Makelle amepatikana na kesi ya kujibu kuieleza mahakama kuwa ilikuwaje wachimba madini na dereva teksi wakakutwe maiti wakati waliwakamata wakiwa hai.

Kwa washtakiwa wengine, Jaji Massati alisema kwa kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo unadhihirisha kuwa walihusika katika kuwakamata marehemu na kwamba walikuwepo katika eneo la mauaji, basi wanayo kesi ya kujibu kuielezea mahakama jinsi marehemu walivyouawa.

Akijibu hoja za wakili wa washtakiwa wa 11 (Koplo Rashid Lema) na mshtakiwa wa 12 (Koplo Rajabu Bakari), Jaji Massati alisema ingawa katika maelezo yao waliyoyatoa katika timu ya polisi ya upelelezi wa tukio hilo washtakiwa hao hawakubali kuwa walihusika, lakini kuna baadhi ya vigezo vinavyowahusisha na tuhuma hizo.

Washtakiwa hao ndio walioieleza timu hiyo kuwa marehemu waliuawa katika Msitu wa Pande na kwamba wao hawakuhusika kuwaua bali walikuwa wakiangalia tu na kwamba baada ya kuuawa wao walihusika kubeba maiti hizo na kuziingiza kwenye gari kwa ajili ya kuzipeleka Hospitali ya Muhimbili.

Alisema kwa ushahidi huo ambao pia uliungwa mkono na mashahidi watatu, namba 30,31 na 36, hafikirii ni kwa nini nao wasikutwe na kesi ya kujibu.

Akielezea sababu za kuwaachia huru washtakiwa watatu, Jaji Massati alisema kuwa ingawa kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamanai hapo walifika katika eneo la tukio wakati wa kuwakamata kule Sinza, lakini hakuna ushahidi kuwa walikwenda katika eneo la mauaji katika msitu wa Pande.

Noel, ambaye alikuwa dereva wa gari la polisi lililotoka kituo cha Chuo Kikuu, gari lake liliishiwa mafuta na hivyo akalazimika kurudi nalo kituoni akiwa na Cedrick, huku Nyangelela yeye aliendesha gari la marehemu kulipeleka katika kituo cha Polisi Urafiki.

“Mshtakiwa wa nne, sita na wa nane simameni. Ninyi hamna kesi ya kujibu hivyo mko huru ondokeni,” alisema Jaji Massati.

Mara baada ya kuelezwa kuwa hawana kesi ya kujibu, Noel alionekana akifuta chozi la furaha kwa kitambaa chake cheupe huku Nyangelela naye machozi ya furaha yakimlengalenga na kujifuta kwa viganja vyake.

Wote kwa pamoja waliondoka kizimbani saa 5.40 huku wakifuatwa na ndugu zao walioonyesha furaha isiyokuwa na kifani.

Kwa upande wa watuhumiwa waliopatikana na kesi ya kujibu, Jaji Massati aliwaamuru kusimama na kisha akawaeleza: “Ninyi mahakama imeona kuwa mna kesi ya kujibu na mnatakiwa kujieleza, lakini mnazo haki tatu”.

Alizitaja haki hizo kuwa ni haki ya kukaa kimya kusubiri uamuzi wa mahakama, lakini akawatahadharisha kuwa athari yake mahakama inaweza kuwaona kuwa wameidharau.

Haki ya pili alisema kuwa wanaweza kutoa ushahidi bila kiapo ambapo hawataulizwa maswali na haki ya tatu alisema ni kutoa ushahidi kwa kiapo ambapo wataulizwa maswali na hata kuleta mashahidi kama wanao.

Zombe baada ya maelezo hayo kupitia kwa wakili wake Msemwa alisema alikuwa yuko tayari kuanza kujitetea muda ule, ombi ambalo hata hivyo Jaji hakulikubali.

Pia alisema anao mashahidi wapatao saba ambao ni pamoja na Sajenti Arifa kutoka Kituo Kikuu cha Polisi, Mkuu wa Gereza la Ukonga, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Matage, Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam ACP Mkumbo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala ACP Masindoki Masindoki na Mkuu wa Upelelezi Central SP Andrew.

Washtakiwa wengine nao walidai watasimama kujitetea na wanao mashahidi isipokuwa mshtakiwa wa 11 ambaye yeye mwenyewe ndiye atakuwa shahidi.

Jaji Massati alitumia zaidi ya saa moja na nusu ambapo aliahirisha kesi hiyo hadi kesho yake kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea

Zombe baada ya kutoka mahabusu alionekana kuwa mpole tofauti na siku ambayo mawakili wake waliwasilisha hoja ambapo alitamba kuwa hakuwa na kesi kabla ya hoja zake kuvunjwa siku ya pili na upande wa mashtaka.

Waandishi wa habari waliokuwa wakimsubiri kwa hamu nje ya mahakama hiyo walimzongazonga kwa maswali ili kusikia lolote kutoka kwake, ingawa awali hakuwa tayari lakini hatimaye alijikuta akitamka.

“Tuonane kesho jamani tuonane kesho. Tuonane kesho ili tujifunze, tuonane kesho tujifunze sheria,” alisema Zombe na kuingia ndani ya basi kwa ajili ya kuondoka kurejea mahabusu.

Nini utetezi wa Zombe na wenzake? Kesho usikose kununua nakala yako ya Mwananchi, kujua hatima ya kesi hii iliyovuta hisia za wengi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.