‘Rubani’ aliyetumia muziki kupata maokoto ya kilimo

“Baba siku moja alirudi kutoka kazini na kutuita na kuhoji, huko mtaani naitwa baba Skwiza! Huyu Skwiza ni nani?, hakuwa anafahamu kama nafanya muziki na tayari nilishajibadilisha jina,” anaanza kusimulia George, maarufu Skwiza.

Mwanamuziki huyo ambaye pia alimuingiza, dada yake Dataz kwenye gemu, anasema wakati huo alikuwa kidato cha pili na familia nyingi ikiwamo ya kwao ziliamini muziki ni uhuni.

“Sikuwa na namna nyingine zaidi ya kusema ukweli, mimi ndiye nilikuwa kijana mkubwa, nikaambiwa fanya madudu yako, lakini kwenye shule tutagombana.

“Wazazi hawakunielewa, lakini niliamua kusimamia kile ninachokipenda, kitu cha ajabu sasa, Dataz alikuwa akisoma Mtwara Tech, hivyo alikuwa akipitia Dar es Salaam kupanda meli kwenda Mtwara wakati huo tunaishi Morogoro.

“Akawa wa kwanza kuingia studio kurekodi, ule muda wa kupita Dar es Salaam anakaa siku kadhaa akisubiri meli, aliutumia kama fursa kurekodi kabla yangu,” anasema.
 

Alivyomuingiza dada yake kwenye muziki

Anasema, Dataz alikuwa akimuona akiimba na marafiki zake, ambao walikuwa wakienda nyumbani kwao kufanyia mazoezi, akapenda.

“Mimi ndiyo ilikuwa nimeingia kwenye muziki, wakati huo tuko home (kwa wazazi) ilikuwa ni rahisi kunikopi, nikamuelekeza akawa anafanya vizuri.

“Alijikuta anaimba tu sehemu ya verse (mistari) zangu, nikaanza kumuelekeza hadi akajikita kwenye muziki, wazazi wetu hawakujua kama tunaimba, tulifanya kwa siri sana, Dataz akapata fursa ya kurekodi mapema kabla yangu,” anasema.

Anasema baada ya wazazi wao kufahamu kuwa ni wasanii, walichukia, lakini wao wakaendelea kusimamia msimamo wa vipaji vyao kwenye muziki.

“Msimamo huu ilikuwa ni njia rahisi wao kuona kumbe hawa wote wako hivi, jamii ilivyotupokea na nyimbo tulizokuwa tukiimba wakaamua kutuacha tuendelee, baadaye wakaja kutusapoti ilifikia wakati wakawa wanatupa hadi nauli kwenda kufanya muziki, ingawa maneno ya watu na ndugu wengine yaliibuka kutokana na taswira iliyokuwepo kwenye jamii kuhusu muziki wakati ule kuwa ni uhuni.

“Kuna watu kwenye jamii huwa wanakuwaga hasi tu siku zote na wengine ni kinyume chake, lakini tulikuja kuwaonyesha hawakuwa sahihi, wakaona ile ni kama karama yetu ikatuweka salama zaidi kwenye familia katika kufanya muziki,” anasema.

Anasema, shuleni alikuwa akitafutwa kama Skwiza, walimu hawakulifahamu hilo jina, lakini walipokuja kujua, walipokea kwa mtazamo chanya.

“Stori zilikuwa mtaani, shule wakawa wanakataa hakuna mwanafunzi kwao anaitwa Skwiza, walikuja kugundua kwenye mashindano ya shule kwa shule ambapo alipafomu, walilipokea vizuri kutokana na maendeleo yangu darasani hayakuwa mabaya na kwenye kipaji nilifanya vizuri.
 

Alitamani kuwa rubani

“Nilikuwa nafanya vizuri darasani, wazazi walitamani niwe daktari, lakini mimi nilikuwa na ndoto ya kuwa rubani, niliamini kwenye fani hiyo. Lakini muziki uliponiingia, nikajikuta nakuwa kama ‘chizi muziki’, sikutaka kufanya kitu kingine tena,” anasema.

Anasema aliingia kwenye mziki mwaka 1997, alipofuata nyayo za binamu yake (Jico Man) aliyekuwa anaimba miondoko la rege, ambaye aliishi naye wakati.

“Nilianza kupenda muziki na kujikuta naingia huko, lakini ni eneo gani nitafiti? Nikaona ni kwenye Hiphop wakati huo ndipo kina Snoppy Doggy wanafanya vizuri, nikajitosa nikiwa kidato cha pili Morogoro Sekondari.

Anasema mwaka 1997 ndipo alianza kujulikana kwenye muziki, akiwa mjini Morogoro ambapo kulikuwa na eneo ambako yalifanyika mashindano ya nani mkali kwa Morogoro na Dar es Salaam.

“Nakumbuka kulikuwa na kundi la kina Sallam na wenzake wakijita Watukutu, kina Boy G (sasa ni marehemu) na wengine wengi.
 

Kutoka kuzomewa hadi kuwa staa

Anasema siku ya kwanza aliposhiriki mashindano hayo, alifanya vibaya sana, alikuwa na verse moja tu.

“Nilizomewa ukumbini, ile hali ikanipa hamu ya kubadilika na kupambana, tulikuwa wawili kwenye kundi langu, mwenzangu alifika stejini kasahau verse na mimi ninayo moja tu, niliaibika.

“Nikajikuta nairudia muda wote, nikaanza kuzomewa, nikapaniki na kupoteza mwelekeo iliniumiza sana, nikiwa pale sielewi, akanifuata O-Ten na jamaa mwingine, wao walikuwa kwenye crew ya ma-brother (kaka) hivyo wakawa hawapati fursa ya kupewa kipaza sauti, wakataka niungane nao.

“Nikaona ile ni fursa, nitapata japo nyimbo mbili tatu, nikawa na hamu ya kufanya vizuri, nikaungana nao tukajiita Killing boys, tukawa wanne kwenye mashindano, kutoka kuzomewa na kuaibika na kuingia kwenye tano bora, nikaona naweza kuwa hata wa kwanza.

Anasema baada ya pale, kuna kundi ambalo lilikuwa na upinzani na lile la Watukutu, wakaomba ajiunge nao, akafanya hivyo yakawa na ushindani Morogoro na Dar es Salaam na huo ukawa mwanzo wa kujulikana na wasanii wengine.

“Wigo mkubwa niliutengeneza pale, wakati huo hata ndoto za urubani tena zikawa zimeyeyuka, akili yangu ilikuwa ni muziki muda wote, nikawa chizi muziki,” anasema.
 

Kolabo bora

Skwiza ambaye alitambulishwa na wimbo wa ‘Naja’ ambao alimshirikisha Juma Nature, anasema kolabo yake kali kuifanya ilikuwa ya ‘Uvumilivu’ alioimba na Keysha.

“Nature alikuwa rafiki yangu, nilipomshirikisha kuhusu kufanya naye kazi hakuwa na tatizo na wimbo ukafanya vizuri, lakini kolabo ambayo ilibamba na ninaikubali zaidi ni ya ‘Uvumilivu’ uliokuwa wazo la Keysha ile kazi alinipa Babu Tale na Master Jay ambaye nilikuwa kwenye lebo yake.

“Tayari Keysha alikuwa ameshafanya upande wake, akanitumia kazi nikawa najaribu kuandika verse zangu, wakati ule nimebobea kwenye Hiphop, ila ikawa inahitaji vionjo vingine ilinipa tabu kidogo nikaifanya ikatoka na kuwa bora,” anasema.
 

Muziki ulivyompa chaneli kwenye kilimo

Skwiza ambaye hivi karibuni ameachia ngoma ya ‘Freeky’ akiwa na nyota mwingine wa zamani Makamua. Alikuwa kimya kwenye gemu kwa muda mrefu mwenyewe akifichua kwamba alijikita kwenye kilimo.

“Majukumu ya familia yaliniweka kando kidogo, ingawa pia nimejikita kwenye kilimo kwa sasa, nalima vitunguu na viazi mviringo,” anasema.

Anasema pesa ya muziki ilimuwezesha kununua shamba huko Ruaha Mbuyuni mpakani mwa Morogoro na Iringa ambako ana zaidi ya ekari mbili akilima vitunguu.
“Pia nalima viazi mviringo Njombe, ambako huku huwa nakodisha mashamba, ni zaidi ya ekari nne ambazo nalima viazi,” anasema.

Skwiza miongoni mwa wanamziki waliojikita kwenye kilimo, anasema alipoingia alipata changamoto ya kujua msimu wa kupanda na kuvuna.

“Kwenye kilimo nako kuna changamoto hasa ya hali ya hewa, huwezi kujua itakuwa vipi, na wakati wa mavuno bei itakuwaje, nilipoingia nilipata hasara, nililima vitunguu, wakati wa kuvuna ilikuwa ni kipindi ambacho vipo vingi sokoni na bei ni ya hasara.

“Tofauti na sasa, gunia ni zaidi ya Sh300,000 shambani, hivyo kwenye kilimo ni kuzingatia muda tu ya hali ya hewa na msimu utakavyokuwa, ukiupatia kinalipa sana,” anasema mwanamuziki huyo na baba wa mtoto mmoja.

Anasema kwake, kilimo na muziki vinategemeana vyote vinamuingizia kipato kwa nyakati tofauti, ingawa muziki ndiyo umempa chaneli za kuingia kwenye kilimo,.

“Nakodisha vibarua kulima, lakini kuna kazi ndogo ndogo mwenye huwa nazifanya nikiwa shambani, kama kupiga dawa au kuweka maji hizo nafanya lakini kushika jembe hapana, japo nimezaliwa kwenye familia ya wakulima na wafungaji.
 

Anusurika kuuwawa

Katika harakati za muziki, Skwiza anakumbuka alivyonusurika kifo akiwa kwenye mojaya shoo mjini Musoma ambapo shabiki alifyatua risasi.

“Ilitokea vurugu nikiwa stejini, kuna shabiki alitofautiana na mwenzake, kumbe mmoja ana bastola, akawa anapiga risasi hovyo, ilikuwa tafrani watu walikuwa wengi wakaanza kukimbia, nilitulia kwanza kuangalia nitakimbilia wapi, nilitoka lakini kwa tahadhari, hata hivyo baada ya muda mambo yalitulia, tukarudi kuendelea na shoo,” anasema.

Tukio jingine ambalo Skwiza analikumbuka ni siku anazindua albamu aliyoshirikiana na dada yake, Dataz ya ‘Wanadata’.

“Ilikuwa CCM Kirumba, Mwanza, tulienda na Afande Sele na Bushoke, mashabiki walifurika, ilikuwa ni shoo kubwa kwangu,”.

“Jingine ni kifo cha Complex na Vivian, ni wiki ambayo ndiyo nilitoa wimbo wa ‘Naja’, siku moja kabla ya kifo chao tulikuwa nao kwenye shoo Morogoro, kisha twende Tanga siku inayofuata.

“Akaniambia tukimaliza ziara tutakaporudi Dar es Salaam kuna kitu nimekifikiria kwenye wimbo wa Naja tukifanye, hakuniambia ni kitu gani, kesho yake nasikia amepata ajali amefariki, iliniumiza na ni tukio ambalo siwezi kulisahau,”.
 

Muziki ulivyompa mkwanja

Skwiza licha ya kupitia haso nyingi akitafuta nafasi ya kutoka kimuziki, anasema alipoanza kujulikana akapata shoo iliyomsahaulisha machungu yote ya muziki .

“Nililipwa Sh5 milioni, wakati ule ilikuwa ni pesa nyingi sana, ilinisahaulisha zile haso zote za kushinda studio huna hela, wakati mwingine unafika studio ratiba inapanguliwa, natembea kwa mguu kurudi nyumbani, umbali mrefu na changamoto nyingine nyingi ikiwamo za kudhulumiwa.

“Kuna siku promota mmoja alinipeleka kwenye kazi Mwanza, baada ya shoo, akanikimbia niko hotelini sijui narudije, nalipaje gharama za hoteli na nyinginezo, lakini shoo ya malipo haya ambayo ilikuwa katika mikoa mitatu ilinisahaulisha haso zote, pesa ile niliwapa kidogo wazazi na nyingine kufanya vitu vyangu ikiwamo kununua shamba, lakini kuna shoo nyingi ambazo zilinipa pesa nzuri baadaye,”anasema Skwiza.