Pera linavyoimarisha kinga ya mwili

Tunafahamu matunda yenye vitamini C husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuharakisha uponaji kwa haraka.

Lakini ulishawahi kujiuliza siku ukikosa machungwa ambayo wataalamu wa masuala ya afya wanatueleza kuwa yamesheheni vitamini C, unaweza kutumia matunda gani yatakayokusaidia kupata vitamini C kwa wingi?

Jibu hili hapa, matunda kama mapera, maembe, mananasi, ukwaju, mabungo, ubuyu na zabibu, machenza, limao na ndimu yatakupa vitamini C ya kutosha.

Ofisa Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Medina Wandella anasema mojawapo ya faida ya kula matunda yenye vitamini C ni kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali, likiwamo Uviko-19.

“Japokuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa matumizi ya matunda yenye vitamini C kwa wingi kuzuia au kutibu Uviko-19, lakini matunda hayo yanaweza kutumika kuboresha kinga ya mwili na kupunguza baadhi ya dalili zinazotokana na maambukizi ya Uviko-19,” anasema Wandella.

Anasema faida nyingine ya ulaji wa matunda yenye vitamini C, yana virutubishi vingi muhimu, likiwamo, vitamini A, D na madini ya calcium na manganese ambayo ni muhimu katika kuimarisha kinga ya mwili.


Matumizi

Wandella anasema kutumia matunda halisi ni bora zaidi kuliko kutengeneza juisi kwa kuwa mtumiaji atapata faida nyingine zilizopo katika tunda husika kama vile nyuzi nyuzi.

Anasema endapo matunda hayo yatachemshwa kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza vitamini C iliyopo, hivyo inashauriwa kula matunda au kunywa juisi bila kuchemsha.

“Inashauriwa kula matunda hayo (mapera) mara kwa mara kwa kuwa vitamini C ni kati ya vitamini ambazo huyeyushwa na maji na haihifadhiwi mwilini kwa muda mrefu,” anasema Wandella.

Hata hivyo, anashauri watu kutumia matunda hayo kiasi, kwa kuwa yana tindikali ambayo huweza kuleta madhara mwilini.