Sababu shambulizi katika tezi dume

Mara nyingi tumezoea kusikia saratani au kuvimba kwa tezi dume kwa wanaume, lakini kumbe pia tezi hiyo inaweza kupata shambulizi na kuleta maumivu ya kushtua kwa watu wazima.

Inaweza ikiwa ni shambulizi bila ya uvamizi wa bakteria au kuvamiwa na kushambuliwa na vimelea mbalimbali. Leo nitawapa ufahamu wa shambulizi la vimelea katika tezi hii muhimu kwa wanaume.

Tezi hii ndiyo inayohusika kutengeneza majimaji yanayofifisha tindikali na takasumu za mkojo ambazo vikichanganyika na mbegu za kiume zinapotoka huweza kuziharibu.

Vilevile inahusika na kuubana mrija wa njia ya kuleta mkojo, ili kuruhusu kupita kwa mbegu za kiume pekee.

Tezi hii inaweza kupata maambukizi ya vimelea na kushambuliwa, hivyo kuathiri utendaji wake.

Uambukizi unaweza kuwa wa ghafla wa kawaida unaodumu kwa kipindi kifupi au unaweza ukawa ni uambukizi sugu unaodumu kwa kipindi kirefu.

Pia shambulizi linaweza likawepo bila kusababishwa na uambukizi wa vimelea. Ni kawaida pia shambulizi kuwapo bila kujitokeza kwa dalili zozote.

Vimelea ambao wanasababisha tatizo hili mara nyingi ni wale wanaosababisha magonjwa yanayoenea kwa kujamiiana, ikiwamo vimelea wanaosababisha kisonono na klamidia.

Vilevile bakteria rafiki wa mwilini walio katika ngozi kama vile staphylococcus na maeneo ya haja kubwa (utumbo mpana) ikiwamo E.coli ambao wanapohama kutoka eneo lake kwenda eneo lingine wanaweza kuleta tatizo hili.

Maambukizi haya yanaweza kusababishwa na uambukizi wa moja kwa moja katika damu na kuifikia tezi dume au kwa uambukizi wa tishu zilizo jirani na tezi dume, ikiwamo uambukizi wa mrija wa mkojo. Maambukizi hayo yanaweza pia kumpata mtu wakati wa kufanyiwa vipimo vya uchunguzi katika njia ya mkojo au wakati wa unyofozi wa tishu za tezi dume kwa ajili ya vipimo ili kubaini uwapo wa saratani.

Dalili na viashiria vya awali ni pamoja na kuwa na homa, kuhisi maumivu au kukereketwa au wakati wa kutoa haja ndogo, kuhisi baridi na maumivu chini ya mgongo na kiunoni. Vilevile kukojoa mara kwa mara, kupata hisia ya kukojoa tena mara baada ya kutoka kukojoa, kuhisi mkojo mkali usiovumilika nyakati za usiku hivyo kumfanya mgonjwa kuwahi haraka kwenda haja ndogo.

Pia kuhisi vitu kuchoma choma wakati wa kukojoa na hali ya mwili kuuma na uchovu.

Tatizo hilo linatibika kwa dawa za maumivu na homa pamoja na antibiotiki dhidi ya vimelea wa bakteria na dawa za kufubaza virusi, lakini uchunguzi wa kimwili na vipimo mbalimbali vya uchunguzi hufanyika.

Daktari atafanya uchunguzi rahisi muhimu kwa wale wenye umri ulio katika hatari ya kupata tezi dume au saratani kwa kutumia kidole cha shahada kupitia njia ya haja kubwa. Ieleweke kuwa njia hiyo hufanyika kwa kuzingatia maadili na mgonjwa huelimishwa juu ya umuhimu wake. Upande wa maabara uchunguzi wa sampuli ya damu na mkojo hufanyika, ili kubaini aina ya vimelea. Pia picha ya xray, ultrasound ya kiuno na tumbo vitafanyika kutazama hali ya mifupa ya kiuno na tezi dume.