Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaweka mikakati kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza

Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye kikao cha kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukizwa Jijini Dodoma leo Juni 9, 2026

Muktasari:

  • Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali zimeanza kuandaa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), huku Kamati ya Kisekta Mtambuka ikitarajiwa kuratibu juhudi za sekta zote katika kuzuia na kudhibiti magonjwa hayo.

Dodoma. Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali zimeungana kuandaa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), kufuatia tahadhari ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu udhibiti wake.

WHO imeeleza kuwa  magonjwa hayo yanahatarisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030.

Hatua hiyo imekuja baada ya wawakilishi wa wizara mbalimbali kukutana jijini Dodoma kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo, ambapo moja ya ajenda kuu ilikuwa kuunda Kamati ya Kisekta Mtambuka ya Magonjwa Yasiyoambukiza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 9, 2026 kuhusu kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Tiba katika Wizara ya Afya, Dk Mwinyikondo Amir, amesema mkutano huo umefanyika kwa maelekezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu na dhamira ya Serikali ya kushughulikia tatizo la magonjwa yasiyoambukiza katika ngazi zote.

Amesema uundwaji wa kamati hiyo ni miongoni mwa maazimio muhimu yaliyofikiwa, huku ikitarajiwa kuratibu utekelezaji wa majukumu ya kila sekta katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye kikao cha kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukizwa Jijini Dodoma leo Juni 9, 2026

“Tupo hapa kujadili kwa kina suala hili na kuandaa mikakati ya taasisi zetu katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza. Pia tunafafanua wajibu wa kila wizara katika mapambano haya,” amesema Dk Amir.

Ameongeza kuwa wadau wanatarajiwa kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu magonjwa yasiyoambukiza na kusaini mwongozo wa ushirikiano utakaoratibu utekelezaji wa mikakati hiyo.

Kwa upande wake, mjumbe wa bodi wa Muungano wa Mashirika Yanayopambana na Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (Tancda), Waziri Ndonde, amesema kikao hicho ni hatua muhimu kwa Tanzania katika kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Amesema tayari wadau wameandaa mwongozo wa utekelezaji na mpango mkakati unaolenga kujenga mazingira yanayochochea wananchi kuishi maisha yenye afya, ikiwemo kushiriki mazoezi ya mwili.

“Changamoto ya mazoezi ya mwili inahusisha sekta nyingi. Unahitaji usalama barabarani, sheria na sera zinazowezesha wananchi, wakiwemo watu wenye ulemavu, wanawake na watoto, kufanya mazoezi kwa usalama. Haya yote yanahitaji uratibu wa Serikali kwa ujumla,” amesema Ndonde.

Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye kikao cha kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukizwa Jijini Dodoma leo Juni 9, 2026

Amesema ana matumaini kuwa kupitia ushirikiano huo, Tanzania itaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza kama ilivyofanikiwa kudhibiti baadhi ya magonjwa ya kuambukiza yakiwemo kifua kikuu pamoja na Virusi vya Ukimwi (VVU).

Kwa mujibu wa WHO, ongezeko la kasi la magonjwa yasiyoambukiza linaweza kudhoofisha juhudi za kupunguza umaskini katika nchi zenye kipato cha chini kutokana na kuongezeka kwa gharama za matibabu.

Shirika hilo linaeleza kuwa watu walio katika mazingira magumu na wenye hali duni ya kiuchumi huathirika zaidi na magonjwa hayo kutokana na upatikanaji mdogo wa huduma za afya, hali inayochangia kuugua na kufariki mapema ikilinganishwa na makundi yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi.

WHO inapendekeza serikali kuendelea kuwekeza katika mifumo ya afya inayojibu kwa ufanisi mahitaji na matarajio ya wananchi, ili kupunguza tofauti hizo na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.