Prime
Hatari iliyojificha katika nguo nyekundu kwa mtoto mchanga

Muktasari:
- Nguo nyekundu hazimdhuru mtoto moja kwa moja, lakini zinaweza kuficha hatari kubwa siku chache za mwanzo baada ya kuzaliwa.
Dar es Salaam. Kama umewahi kujiuliza kwa nini maduka mbalimbali huuza nguo za watoto wachanga zenye rangi angavu kama nyeupe, pinki, bluu bahari au njano! Leo una cha kujifunza.
Wataalamu wa afya za watoto wachanga wametaja hatari iliyojificha katika nguo nyekundu kwa mtoto mchanga, ambazo wanawake wengi hawaijui.
Hata hivyo, wazee wa zamani, hasa bibi zetu wa makabila mbalimbali, wamekuwa na utamaduni wa kuwashauri wanawake wanaotarajia kupata watoto kwa mara ya kwanza, wakiwausia kuwa ni mwiko kumvalisha mtoto nguo nyekundu. Hata hivyo, wengi hawaweki wazi sababu.
Neema Shetui (27), mkazi wa Tanga, amesema wakati anapata mtoto wake wa kwanza, mama yake alimshauri mara kwa mara ahakikishe hamvalishi mtoto nguo nyekundu, wala kumfunika kwa kitenge, khanga au taulo jekundu.
"Mama alianza kuniambia kabla. Baada ya kujifungua, bibi yangu alikuja kuniona. Baada ya mazungumzo na mtoto kulala baada ya kumnyonyesha, nikamlaza pembeni yangu tukiwa sebuleni na kumfunika na mtandio wangu mwekundu.
"Bibi alinikanya na kuufunua haraka, akisema ni mwiko kufanya hivyo. Nilishangaa, nikauliza kwa nini. Akasema hata yeye alihusiwa na bibi yake. Nikajua labda mambo ya kimila," amesema Neema.
Neema ni miongoni mwa wanawake wengi hapa nchini wanaoamini kuwa kufanya hivyo haitakiwi, bila kujua sababu.
Mtaalamu wa afya ya mama na mtoto kutoka kituo cha Waridi Fertility Solutions kinachojihusisha na afya ya uzazi, Dk Rose Masonda, amesema nguo nyekundu hazimdhuru mtoto moja kwa moja, lakini zinaweza kuficha hatari kubwa siku chache za mwanzo baada ya kuzaliwa.
Dk Rose amesema nguo nyekundu inaweza kuficha hatari ya utokaji wa damu katika kitovu cha mtoto.
"Ni siku ya tatu zilikuwa zimepita tangu mtoto azaliwe. Alionekana mtulivu, analala vizuri, hana homa, hana kilio cha ajabu. Mama anafurahia. Alivaa vitenge vizuri vya rangi nyekundu kali, akamfunika. Mtoto alionekana mtulivu.
"Lakini, katika hali ya kawaida kabisa, bila kelele wala ishara, damu ilikuwa inatoka kwenye kitovu taratibu, lakini mama hakuiona kwa sababu nguo aliyomfunika mtot o ilikuwa nyekundu," amesema.
Dk Rose amesema kwa bahati mbaya, alikuja kugundua hali hiyo mtoto akiwa tayari amepoteza kiasi kikubwa cha damu.
"Na hapo ndipo aliponitafuta kama daktari. Nikakutana na mama aliyechanganyikiwa, aliyejilaumu. Alikuja kwangu ana uchungu mwingi, akiniuliza: 'Kwa nini hakuna aliyeniambia mapema?'" amesema.
Amesema hali hiyo huwakuta madaktari wa watoto, lakini mara nyingi mama anakuwa amechelewa kugundua, na wengi wanawapoteza watoto wachanga kwa njia hiyo.
Amesema mjamzito au mama anayejiandaa kujifungua, nguo nyekundu si mbaya kwa hali ya kawaida na kiimani.
"Lakini, kisayansi, zinaweza kuficha damu au majeraha ya mtoto, hasa katika wiki ya kwanza ya maisha ambapo mwili wake bado ni dhaifu sana.
"Uamuzi wa rangi unavyomvika mtoto wako unaweza kuwa tofauti kati ya kuona mapema au kuchelewa kusaidia," amesema Dk Rose.
Ameshauri wazazi kutumia nguo za rangi nyepesi — kama vile nyeupe, pinki angavu, bluu bahari angavu au zenye kuonyesha uchafu au doa kwa haraka — katika siku za mwanzo, ili chochote kidogo kitakachoibuka kiweze kuonekana mapema kabla hakijawa tatizo kubwa.