Jinsi upandikizaji wa uume unavyofanyika

Dar es Salaam. Huduma ya upandikizaji uume iliyotangazwa hivi karibuni na Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma ilizua mjadala, huku wengi wakipiga simu kuulizia huduma hiyo.

Hospitali hiyo ilifanya upasuaji huo wa kwanza kwa kushirikiana na chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo nchini (TAUS) pamoja na daktari bingwa kutoka nchini na walipandikiza uume kwa watu wawili waliokuwa na matatizo ya nguvu za kiume.

Huduma hiyo hutolewa kwa mgonjwa kuwekewa vipandikizi vya plastiki vinavyoitwa silicone kwenye uume, hivyo kuwa na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kama kawaida.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na uzazi wa Hospitali ya MDM Specialized, Deogratius Mahenda anasema vipandikizi hivyo vinasaidia misuli ya uume kuwa imara.

Vipandikizi hivyo ambavyo ni plastiki vinaingizwa kwenye misuli ya uume na vitaendelea kuwapo kwa maisha yote ya mhusika. Upasuaji hufanyika kwa muda wa saa moja na nusu.

Anaeleza baada ya upasuaji huo, siku saba za awali zinakuwa za uponyaji na mhusika anatakiwa asubiri kwa mwezi mmoja ndipo aanze kushiriki tendo la ndoa.

“Mwanamume aliyewekwa vipandikizi, hisia zake zitabaki palepale…kama atahitaji kupata watoto ataweza kwa kuwa utoaji wa mbegu hauathiriwi.”

Anaeleza kuwa mwanamume aliyewekewa vipandikizi hategemei mtu amvutie hisia au kuguswaguswa ndipo uume usimame.

"Mwanamume aliyewekwa vipandikizi akitaka kufanya tendo la ndoa anainyoosha, akikubaliana na mwenza wake inatosha, uume anaupindisha.

“Vipandikizi havisababishi maumivu, mhusika anaweza kushiriki tendo hilo kadiri anavyotaka kwa sababu vinauwezesha uume usimame wakati wote,” anasema na kuongeza kuwa akimaliza tendo kuna namna ya kuuweka uume usionekane kama umesimama.


Upatikanaji vipandikizi

Anasema vipandikizi vinaagizwa nje ya nchi na gharama yake inategemea na bei ya soko kwa wakati husika.

“Kulingana na uhitaji wa wagonjwa wanaopata matatizo ya nguvu za kiume, Serikali iondoe kodi kwa vipandikizi hivyo.

“Vipandikizi hivi jozi moja inauzwa kwa Euro 2,500, sasa ikiletwa hapa kwetu ikawekewa VAT asilimia 18, bado maandalizi ya upasuaji mgonjwa anaweza akajikuta akigharamia hadi kufikia Euro 5,000,” anasema Dk Mahenda. Mkurugenzi wa Kampuni ya Zephyr Surginal Implants inayosambaza vipandikizi kutoka nchini Swizerland, Raphael Llorens anasema kaka yake ambaye ni daktari amejenga kiwanda hicho baada ya kukutana na wagonjwa wenye tatizo la kukosa nguvu za kiume.

Llorena anasema vipandikizi hivyo vipo vya aina tatu; Inflatable Penile Implant, Malleable Penile Implant na Soft Penile Implant.

Anasema mwanamume anayewekewa vipandikizi hivyo anakaa navyo maisha yake yote, hufanyika baada ya sindano na dawa kushindwa kufanya kazi.

Anasema wanatarajia kuwa na maabara Tanzania ambayo itatengeneza dawa na sindano zitakazokuwa zinachomwa kwenye uume wa mwanamume, ili imsaidie kusimamisha.

Llorens alitolea mfano kwa Serikali za Ulaya huwa wananunua vipandikizi kwa ajili ya hospitali za Serikali, ili upasuaji ufanyike kwa wenye matatizo ya nguvu za kiume.

Anasema kama Serikali ya Tanzania itanunua vipandikizi hivyo kwa wingi, kampuni hiyo itapunguza gharama ili wananchi wenye matatizo hayo waweze kuwekewa.


Chanzo kukosa nguvu za kiume

Dk Mahenda anasema wengi wameathirika na msongo wa mawazo na matatizo ya kisaikolojia kutokana na kazi za kila siku, ugumu wa maisha na kutokuwa na maelewano mazuri na wenza wao.

Sababu nyingine ni magonjwa, mfano kisukari ambacho kinaathiri mishipa ya damu na mifumo ya fahamu pamoja na baadhi ya dawa na daktari hakuwa tayari kutaja aina hizo za dawa.

“Shinikizo la damu nayo inaharibu mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye uume, hivyo kuchangia changamoto hiyo,” anasema.

Pia waliopata ajali na kuvunjika uti wa mgongo na wenye matatizo ya mfumo wa fahamu kwa waliopata kiharusi, wanaweza kupata shida ya nguvu za kiume.

Wenye matatizo ya kisaikolojia, daktari anasema wanatakiwa kupatiwa ushauri nasaha pamoja na dawa, ili waondokane na tatizo hilo.

Anasema wenye matatizo ya ufahamu, magonjwa ya shinikizo la damu na sukari zipo dawa za vidonge ambazo wakitumia zitasaidia kurudisha usimamishaji wa uume katika hali ya kawaida, sindano pamoja na dawa za kupaka.

“Kwa wale ambao tiba hizo zimeshindikana wana nafasi ya kuwekewa vipandikizi kwenye uume visaidie katika usimamishaji wa kawaida wa uume,” anasema.