Kumbe mtoto anasikia, kuhisi upendo au hasira akiwa tumboni
Muktasari:
- Wataalamu wa afya wameshauri mama anapaswa kuzungumza na mtoto pindi ujauzito unapofikisha miezi mitatu, wakibainisha mafanikio, furaha au huzuni kwa mtoto hutegemeana na mama alivyokuwa wakati wa ujauzito.
Dar es Salaam. Mtoto ambaye hajazaliwa anaweza kusikia sauti, kuhisi upendo na hasira, hivyo wanasayansi wanashauri ni vyema mama kuwa katika hali nzuri katika kipindi cha ujauzito.Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mimba inapofikisha umri wa miezi mitatu masikio ya mtoto huchomoza na mara hiyo huwa na uwezo wa kusikia.“Mtoto anasikia mazungumzo, ukiimba anakusikia naa hata mama akiwa na hasira mtoto huhisi na wakati mwingine kama hiyo hali itamtawala nyakati nyingi, mtoto anazaliwa na hasira na kulia sana,” amesema Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Aga Khan, Jane Muzo.Dk Muzo anasema mimba inapofikisha umri wa miezi mitatu, mtoto huota masikio na mara hiyo huanza kusikia kila kitu.Mwanaharakati wa kike wa Mumbai na Daktari wa magonjwa ya wanawake, Suchitra Delvi amesema kwamba mtoto ambaye hajazaliwa, anaweza kusikia sauti lakini hawezi kuelewa lugha yoyote, ijapokuwa ana hisia kwa kiwango cha juu.“Kadiri mwili wa mtoto unavyokua tumboni, masikio yake pia hukua. Katika hali hiyo, mawimbi ya sauti pia humfikia,” amesema.Hata hivyo, wanasayansi wanasema mtoto anayekua tumboni anaweza kujifunza hadi maneno 500, hata hivyo ulimwengu wa sayansi umegawanyika katika suala hili.Akitoa elimu kwa wajawazito kupitia Mradi wa Safiri Salama katika Zahanati ya Kambangwa iliyopo Mwananyamala, Dk Muzo amesema kuna haja kwa kinamama kuzungumza maneno mazuri wanapokuwa wajawazito.“Unatakiwa kuongea na mtoto kwani anasikia. Pia tunashauri mama usiwe na hasira au msongo wa mawazo kwani hali hiyo inampata mtoto, hivyo anakosa furaha,” amesema.Akitaja mambo mengine muhimu, Dk Muzo amesema mama anatakiwa kula lishe bora kwani mtoto hufikisha uzito wa kilog moja anapofikisha umri wa miezi saba, kabla ya kuanza kukua kwa kasi kufikia miezi tisa kabla hajazaliwa.Amesema mtoto hukua taratibu mwanzoni kwa kuwa hatua za awali kuna mabadiliko mengi hutokea kabla ya miezi mitatu ya ujauzito, hivyo mtoto hushindwa kuongezeka uzito na mama pia.“Miezi mitatu mama anaanza kupata hamu ya kula muda huo mtoto anakua ameumbika vizuri, siku zinavyokwenda kuna sehemu pia za viungo vya uzazi zinakua mpaka miezi saba. Watoto wengi hawakui kwa haraka kutokana na yale mabadiliko yanayotokea kwenye placenta ya uzazi,” amesema na kuongeza:“Ndiyo maana miezi mitano misuli ya mtoto inakua imekomaa akicheza mama anasikia mtoto wake anazunguka, tangu mwanzoni anakua anacheza lakini misuli yake haijakomaa mama hawezi kusikia.”Pamoja na hilo, Dk Muzo ameonya kinamama kuacha kufuatilia ushauri wa mitandaoni na badala yake waende kliniki.Amesema wataalamu wanaoibuka mitandaoni wanatoa mafunzo ambayo ni kinyume na uhalisia.“Wanaibuka na kujiita wauguzi lakini wengi wanatoa taarifa sizo, wanaeneza kwenye jamii. Kinamama wapewe mafunzo kuhusu dalili za hatari na nini cha kufanya angalau mara mbili kwa mwezi waendelee kupata elimu,” amesema.Mmoja wa kinamama waliopata elimu hiyo, Zainab Mkungwa amesema inawasaidia wao pamoja na watu wengine wa karibu yao kwa kuwaeleza yale waliyojifunza.Mganga Mfawidhi wa Zahanati Kambangwa, Dk Dora Ntemo amesema changamoto wanayokumbana nayo kinamama wanachelewa kuhudhuria kliniki na wengine wanasubiri mpaka tumbo likue.“Mtu anaweza kuja na mimba ya miezi mitano au saba. Pia kinababa hawawaleti kinamama kliniki wengi wanasema wao watafutaji mpaka atoke ndiyo apate hela ya kula. Tunaendelea kuwapa elimu wapate vipimo pamoja,’’ amesema Dk Ntemo.