Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutokulala kwa muda mrefu na athari kwa mwanamume

Muktasari:

  • Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha wanaume wengi wanaolala kwa muda mfupi huwa na kiwango kidogo cha kichochezi hiki. Utafiti uliochapishwa mwaka 2006 katika jarida la Sleep and Sports Health uliohusisha wazee wa umri wa zaidi ya miaka 50 unashangaza.

Usingizi ni dawa ambayo inaweza kukutibu bila wewe kujua, kwa hiyo inafaa uitumie mara nyingi

Ni wengi katika jamii ambao hawafahamu umuhimu wa kupata muda mzuri wa kulala katika maisha yao.

Pia, wengi hawatambui jinsi ukosefu wa usingizi wa kutosha ulivyo na athari kwao na kuwa kulala kwa muda mfupi kunapunguza kichochezi dume kiitwacho testosterone

Mwonekano wa mwanamume yeyote duniani na kupata sifa ya kuitwa mwanamume husababishwa na kichochezi hiki testosterone.

Kichochezi hiki kiletacho tabia na maumbile ya kiume na kumpa mtu sifa ya kuitwa mwanamume kinaweza kuathiriwa na ukosefu wa usingizi wa kutosha.

Kichochezi hiki kinazalishwa katika sehemu za uzazi za mwanamume katika korodani na hutiririshwa kutoka korodani  na kusambaa kwenye sehemu mbalimbali za mwili kupitia njia ya damu.

Homoni hii ndiyo inayotoa maumbile na kazi za kimwili kwa wanaume na hufanya maumbile ya kiume kuwa na misuli  iliyo kakamavu, mifupa imara, kuota ndevu, kupata ndevu za kifua, kuongezeka maumbile ya viungo vya uzazi, kuwa na sauti nzito, kumfanya mtu apate hamu ya kujamiiana, kuwa na mikono iliyojitokeza kwa nje, kutembea kibabe.

Pia, kichochezi hiki hasa kwa wanaume hutokea kuwa na upara kichwani.

Nini athari ya kupungua kichochezihiki

Wanaume wengi wanapofikia umri wa miaka 30 au zaidi, wengi wao hudhani kuwa kupungua kwa uwezo wao wa kujamiiana kunasababishwa na umri mkubwa, kumbe sivyo.

Hilo si sahihi, bali ni kupungua kwa kichochezi hiki cha testosterone. Moja ya athari ya kupungua kwa kichochezi hiki ni kupungua kwa nguvu za kiume na kutofika kileleni, kukosa mwamko wa kujamiiana, kupata ugumba kwa wale walio katika umri wa uzazi.

Mambo haya yakitokea humwathiri mhusika kisaikolojia na kumfanya kuwa na sonono (depression), kuwa na tabia za ukali, msongo wa mawazo, unyongofu, kujitenga na jamii kwa kule kuhofia kunyanyapaliwa, misuli ya mwili kupungua uzito na uimara, huwa katika hatari ya kupata maradhi ya moyo.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wenye upungufu wa homoni hii hufa mapema kulinganisha na wale wasio na tatizo hili.

Nini kinatokea mtu akikosa usingizi?

Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha wanaume wengi wanaolala kwa muda mfupi huwa na kiwango kidogo cha kichochezi hiki. Utafiti uliochapishwa mwaka 2006 katika jarida la Sleep and Sports Health uliohusisha wazee wa umri wa zaidi ya miaka 50 unashangaza.

“Matokeo ya utafiti wetu yanaongeza uwezekano kuwa wanaume watu wazima na wazee ambao hupata muda mfupi sana wa kulala nyakati za usiku huwa na kiwango kidogo sana cha homoni ya testosterone wakati wa asubuhi,” anasema Plamen Penev kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, Marekani.

Wakati wa utafiti, wataalamu waliofanya uchunguzi huo walipima kiwango cha homoni ya testosterone katika damu kila asubuhi kwa wanaume watu wazima wenye umri kati ya miaka 64 na 74 waliojitolea kushiriki kwenye utafiti huo.

 Aidha, mtindo wao wa kulala pamoja na kupata usingizi pia vilichunguzwa kila siku kwa muda wa wiki nzima.

Matokeo ya uchunguzi huo yalionyesha kuwa kiasi cha usingizi walicholala kilikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiwango cha testosterone katika damu wakati wa asubuhi.

Wale waliopata usingizi mzuri na kwa muda mrefu (walau saa nane) walikuwa na kiwango kikubwa cha testosterone wakati wale waliopata usingizi wa kubabaisha (saa nne) walikutwa na kiwango cha chini cha homoni hiyo. Wastani wa muda wa kulala ulikuwa saa sita.

“Pamoja na kwamba matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa urefu wa muda wa kulala wa mtu waweza kuwa kiashiria cha mabadiliko ya homoni katika mwili yanayohusiana na umri, matokeo ya utafiti huu yanatoa picha ya nini kinachotokea mwilini mtu asipopata usingizi wa kutosha.

Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kuthibitisha umuhimu wa uhusiano kati ya usingizi na mabadiliko ya homoni katika mwili,” anasema Dk Penev.

Ushauri

Ili kuimarisha kiwango cha kichochezi hiki ni vyema kuepukana na mambo yanayoweza kuingilia usingizi wako.

Kwa mfano, kuzima kompyuta, simu, taa, runinga, redio na kuacha kulala na vikuza sauti masikioni. 

Tengeneza mazingira ya chumba chako yawe na joto la wastani na uende haja ndogo kabla ya kulala. Inafaa kuongeza muda wako wa kulala kwa saa kumi na muhimu kula lishe bora na mazoezi ya wastani.

Kadri unavyopata usingizi ndivyo kiwango chako cha testosterone huongezeka na kuipa uimara  misuli yako ya mwili.