Kwa nini hushauriwi kunywa maji kupita kiasi

Hivi sasa maeneo ya ukanda wa pwani kama Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Zanzibar kuna hali ya hewa ya joto ambayo inawalazimu watu wa maeneo haya kunywa maji mengi.

Hali ya kupata kiu katika mazingira ya joto huwa ni kawaida, sababu hutokana na mwili kupoteza maji na chumvi-chumvi, yaani jasho kwa njia ya ngozi.

Kwa kawaida inashauriwa kwa mtu mzima kunywa maji kiasi cha glasi 8 hadi 10 kwa saa 24 au lita 1.5 hadi 2 kwa siku. Lakini bado hata anayekunywa lita tatu hadi nne si tatizo.

Kituo maarufu cha tafiti za magonjwa cha CDC cha Marekani kinahimiza kwa wanawake watu wazima kunywa lita 2.7 kwa saa 24 na wanaume lita 3 kwa saa 24.

Pamoja na maji kuwa ni muhimu kwa uhai wa mwili, mara chache hutokea maji yakawa ni sumu kwa mwili, tatizo lijulikanalo kitabibu kama ‘water intoxication’.

Wapo wagonjwa wanaoweza kushauriwa kutokunywa maji kupita kiasi, ikiwamo wagonjwa wa tatizo la moyo kufanya kazi, magonjwa sugu ya figo na tatizo la kiwango kidogo cha madini.

Mwili huwa na viashiria muhimu pale unapokuwa na upungufu wa maji, ikiwamo kuhisi kiu na vilevile mwili huwa na njia za kupunguza kiwango kilichozidi cha maji, ikiwamo kukojoa na kutoka jasho.

Pia, mwanadamu anaweza kupoteza maji mwilini kwa kupata haja kubwa na kupumua au wakati wa kuongea.

Tatizo la maji kuleta madhara mwilini linawapata zaidi wanariadha, wanajeshi, wafungwa na wanaofanya kazi ngumu. Tatizo hilo ni la nadra kuwapata watu na lisipodhibitiwa linaweza kusababisha kifo.

Kunywa maji kupita kiasi kunaweza kusababisha kuchujuliwa kwa madini ya sodiamu katika damu na hatimaye kupungua, hali hii kitabibu hujulikana kama “Hyponatremia”.

Madini haya yanapopungua, msukumo wa damu huyumba na kuleta athari za kiwango cha maji ndani ya seli na maji yanayozunguka mwilini.

Hali hii inapojitokeza kiwango cha maji cha mwili hupanda na kusababisha seli kujaa maji na kuvimba, hali hii inaweza kuleta athari mbalimbali, ikiwamo kichwa kuuma, kichefuchefu na kutapika.

Baadaye hali hii husababisha kuchanganyikiwa, kushindwa kuweka kumbukumbu, kukosa nguvu, kuweweseka, mchoko, kukosa utulivu, misuli kuuma na kukakamaa, degedege na kupoteza fahamu.

Tafiti za kitabibu zinaonyesha kuwa uwezo wa figo kuchuja ni lita 20-28 kwa saa 24 na uwezo wa kuchuja si zaidi ya lita 0.8-1 kwa saa moja.

Hivyo, ni hatari kwa mtu kunywa maji kwa ghafla kiasi cha lita 4-5 ndani ya saa moja, kwani uwezo wa figo kuchuja lita hizo kwa saa moja ni mzigo kwake.

Tafiti nyingi zinaonyesha wale waliofariki kwa kunywa maji mengi ni wale waliokunywa zaidi ya lita 4 kwa ghafla.

Kunywa maji mengi pia kunaweza kuleta athari kubwa kwa wale wenye matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu, moyo kushindwa kufanya kazi, matatizo ya figo na wenye umri mkubwa wasioweza kutembea.

Athari nyingine ni kupata hali ya kukujoa mara kwa mara, ikiwamo kila baada ya dakika 5-10. Kwa kawaida mwanadamu anatakiwa kwenda haja ndogo angalau mara 6-8 kwa saa 24.

Umuhimu wa kunywa maji unashinda zile athari chache zinazojitokeza, kwani yanahitajika na seli kwa ajili ya kazi zake mbalimbali.