Mapambano dhidi ya saratani changamoto, matumaini kwa jamii

Unafahamu kama huu ni mwezi wa saratani? Usichokijua ni kwamba wanaougua ugonjwa huu kipindi chote cha tiba hupitia hatua ndefu zenye changamoto za kijamii, kibaiolojia na za kiuchumi.

Saratani huathiri watu wa rika na jinsia zote, lakini katika makundi hayo wanawake wametajwa kuathirika zaidi, huku saratani ya tezi dume ikiongoza kushambulia wanaume kwa asilimia 23, ikilinganishwa na saratani nyingine.

Kila miezi miwili ya mwanzo wa mwaka ni kipindi cha kutoa uelewa kuhusu magonjwa hayo na Februari 4 dunia huadhimisha siku ya saratani.

Kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, kati ya wagonjwa wapya 8,000 na wale wa marudio 68,000 waliopokelewa hospitalini hapo mwaka 2021, asilimia 70 ni wanawake na asilimia 30 ni wanaume.

Hali ya ugonjwa wa saratani nchini inakadiriwa takribani watu 42,000 hugundulika kila mwaka. Zaidi ya asilimia 35 hufika hospitalini, sawa na wagonjwa 16,000 na wengine hupotea wakifuata matibabu mbadala na kufariki huko.

Takwimu zinaonyesha asilimia 60 hufika kufuata huduma katika vituo vya afya wakiwa katika hatua ya tatu na nne ya ugonjwa ambayo ni ngumu kutibika na kupona kabisa.

Wanaougua ugonjwa huo, wanapitia shida, taabu na maumivu makali yanayoambatana na gharama za kifedha na maisha, ambayo yanapitiwa pia na ndugu wanaowauguza, marafiki.

Huu ni ugonjwa hatari duniani, wapo ndugu na jamaa ambao wamepoteza wapendwa wao. Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo, mwigizaji mwongozaji na mwandishi wa filamu nchini, Leah Mwendamseke, maarufu kama Lamata ameamua kutumia sanaa kufikisha ujumbe kwa jamii.

Lamata anasema uwepo wa tawi ‘scene’ katika tamthilia anayoiongoza ya Juakali, ilikuwa kutoa uelewa ili kuihamasisha jamii kupima mapema na kujikinga na ugonjwa huo.

Tawi hilo ambalo limeambatana na mwigizaji Femi (mwenye saratani ya damu) kunyoa nywele zake, familia ya mchumba wake ‘Luka’ nayo imenyoa nywele, huku baadhi ya waigizaji, wapenzi wa tamthilia hiyo wakinyoa nywele zao ili kumuunga mkono Femi.

Kwa mujibu wa Lamata, stori ya Femi ni uhalisia wa maisha na tangu tamthilia hiyo inaanza ilishaanndaliwa.

“Kuhusu Femi kuna mtu amepita kwenye hayo maisha si ya kufikirika wala ya kutunga, imeshamkuta mtu na matukio mengi ndani ya Juakali ni ya kweli.

“Niliipata kutoka kwa mtu wa karibu, ilinigusa sana. Niliamua kuisimulia kutumia tamthilia, mimi si mtaalamu, lakini ni mhanga, ugonjwa wa saratani kuna hatua ikifika nywele huwa zinanyonyoka na huwa wanashauriwa wanyoe kabisa na kuna wengine zinaweza kuota na wengine zisiote kulingana na hali ya ugonjwa wenyewe,” anasema.

Staa huyo katika uandishi wa filamu anayemiliki tuzo kadhaa, anasema ilipofikia hatua ya kunyoa nywele waliona wamuunge mkono Femi.
“Kumwonyesha tuko pamoja kwa maana kuna saratani ikishafika mwisho haiwezi kupona unafariki na wataalamu wa afya wanasema hapa tulipofika haiwezekani.

“Tunanyoa nywele kuunga mkono wagonjwa hawa na kutoa uelewa wa kupima mapema, maana huu ugonjwa unajitengeneza na ukianza kuona dalili umefika hatua za juu,” anasema Lamata.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Crispin Kahesa anasema mapambano dhidi ya saratani ni mtambuka na eneo linalohusisha sekta zaidi ya moja; habari na michezo, afya, elimu.

“Juakali imeamsha kile jamii inachopaswa kufanya, sekta hizi zote zikiungana tunaweza kupambana na saratani. Ukiangalia sekta ya utamaduni, michezo na sanaa na jamii yetu ni njia inayoweza kutumika kuifikia jamii kwenye rika tofauti.

“Tunaweza kuitumia kuhusisha walimu mashuleni katika kila eneo na sekta ya afya nayo itaendelea kutoa huduma kuelimisha jamii na wote wakishirikiana hili litaleta matokeo chanya,” anasema Dk Kahesa.


Changamoto kwa wagonjwa wa saratani

Lamata anasema, dada yake ameugua saratani na amepitia changamoto nyingi, hivyo aliandika tamthilia hiyo akiwa anafahamu nini wagonjwa hao hupitia, lengo kuipa uelewa jamii ijue namna ya kuishi nao, kuwatia moyo na umuhimu wa kupima afya mapema.

“Tanzania watu wengi wamefariki na saratani, ukipita nyumba mbili kuna watu wanafariki na saratani. Sasa hivi ndiyo nimegundua hili tatizo ni kubwa, tangu tawi ‘scene’ ya Femi na Luka watu wamenitumia video, picha na meseji namna ndugu zao wanavyopitia changamoto, wengi ni wahanga,” anasema Lamata.

Kauli ya mwandishi huyo inaungwa mkono na Mkufunzi wa Kitaifa wa saratani ya mlango wa kizazi, Dk Amina Yusufu anayesema Januari ni mwezi wa ufahamu kuhusiana na saratani ya mlango wa kizazi, lakini wagonjwa hao wanakabiliwa na changamoto nyingi.

Dk Amina, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama kutoka Hospitali ya Bugando anasema hiyo ni miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake na wamekuwa wakifanya uchunguzi kubaini mapema, hata hivyo bado hakuna mwamko kwa walio wengi kupima.

Anasema miongoni mwa wanaobainika na ugonjwa huo wamekuwa wakikata tamaa kwa kuwa hawana uelewa, hivyo elimu inahitajika.

“Wengi hupokea kwa mshtuko kwa kuwa ugonjwa huo unaambatana na gharama za matibabu, lakini nje ya matibabu zinaenda moja kwa moja, mtu anapopata huduma ya tiba kuna changamoto pia za matokeo hasi ya dawa,” anasema.

Dk Amina anasema tiba ya saratani ni mtambuka, inaambatana na dawa sambamba za upasuaji na tiba nyingine anazopewa ili kuzuia madhara mengine, pamoja na kwamba zina manufaa, lakini zina adha ndogondogo mgonjwa anazopata, zipo za karibu mgonjwa akakosa hamu ya kula.

“Mgonjwa kupata kichefuchefu inajumuisha mabadiliko kwenye baadhi ya mifumo, ikiwemo kucha kubadilika rangi, nywele zinaanza kuisha/kunyonyoka au rangi yake ya mwili inabadilika, wenye rangi nyeupe ya muda mrefu baada ya kutibiwa anapata aina ya makovu mbalimbali,” anasema.

Dk Amina anasema mgonjwa hupitia changamoto nyingi za kijamii na kibaolojia na hasa wanawake wanaopata saratani ya kizazi na matiti hupitia changamoto ya kutoa harufu.

Dk Kahesa anasema saratani ya mlango wa kizazi inaathiri wanawake wengi, changamoto zinaanzia nyumbani kwa mgonjwa mwenyewe na familia inapata changamoto.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni ugonjwa unaweza kusambaa kwenye viungo vingine.

Anasema wapo wanaoshindwa kwenda kutibiwa kutokana na ukubwa wa gharama za huduma na vipimo vya kufanya kabla ya kuanza matibabu, hivyo kama hana uwezo huo hawezi kuanza matibabu.

Dk Kahesa anasema wanawake wana hatari zaidi ya kupata saratani ikilinganishwa na wanaume, hasa kutokana na vihatarishi mbalimbali.

Anasema saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kwa asilimia 33, ikifuatiwa na asilimia 16 ya matiti inayoathiri shingo, kichwa na kinywa ni asilimia 11, tezi dume asilimia 9 na saratani ya njia ya chakula asilimia 8.

Dk Kahesa anasema licha ya saratani zinazoongozwa kuwa zinazoathiri wanawake, kundi hilo wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa katika saratani nyingine, zikiwemo za utumbo mpana, njia ya chakula, ngozi na hata saratani ya damu.

“Ukiangalia kwa wanaume wao tezi dume ndiyo inawaumiza zaidi, lakini hizi saratani nyingine wanashea makundi yote.

Ukiangalia saratani ya kichwa, utumbo mkubwa, wanaoathirika ni kinamama na kinababa pia, ila mlango wa kizazi na matiti ni wanawake, ndiyo maana idadi kwao huongezeka,” anasema Dk Kahesa ambaye pia ni Mkurugenzi wa huduma za kinga hospitalini hapo.

Miongoni mwa vitu vinavyowaumiza wagonjwa wenyewe na ndugu zao ni gharama kama anavyosema Jacqueline Chammafwa (45) ambaye miaka mitano iliyopita aligundulika na saratani ya matiti.

Jacqueline anasema alitumia zaidi ya Sh4.8 milioni kujitibu kwa dawa za mionzi hivyo kutoa wito kwa Serikali kuangalia namna ya kusaidia punguzo kwa wagonjwa.

Esha Stima (77) anasema matibabu ya Saratani ni gharama hivyo kuiomba Serikali kupunguza gharama ya ugonjwa huo ili kuvutia watu wengi wajitokeza kupima ugonjwa huo.
“Ninaomba Serikali iweke ruzuku kwenye idara za Saratani.
 

Kirusi cha HPV

Kirusi cha HPV ‘human papilloma virus’ ndicho hatari kwa kusababisha saratani za aina mbili tofauti zinazokua kwa kasi, ikiwemo inayoathiri koo la hewa.

Sayansi inaonyesha asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi hupata maambukizi kwa njia ya ngono, huku saratani ya koo la hewa ikishika nafasi ya saba na chanzo kikitajwa kuwa ngono ya kinywa.

Pamoja na visababishi vingine, saratani ya shingo ya kizazi inatokana na aina 40 ya virusi, aina mbili ikiwa ni vinavyosambaa kwa njia ya ngono, ikiwemo ‘Squamos cell carcinoma’, kirusi namba 16 na ‘Adenocarcinoma’ namba 18.