Matumizi sahihi ya sindano za insulin
Tiba ya sindano za insulin mara nyingi hutumiwa na wenye aina ya kwanza ya kisukari, wanawake wajawazito wenye kisukari cha mimba na wakati mwingine mwenye aina ya pili ya kisukari anaweza kutumia tiba ya sindano za insulin kama vidonge vimeshindikana kudhibiti kiwango cha sukari.
Mgonjwa anaweza kutumia aina moja ya insulin au aina tofauti kwa siku kulingana na mtindo wake wa maisha, kila anachokula na viwango vyake vya sukari kwenye damu.
Ili insulin ifanye kazi mwilini kama inavyopaswa, ni lazima ufuate sheria zote za uhifadhi wake na tarehe za kumalizika muda wa matumizi. Sindano za insulin ni lazima zihifadhiwe kwenye sehemu ya ubaridi kama jokofu, ila haitakiwi kuganda.
Kama kuna ulazima wa kusafiri, ni muhimu mgonjwa kuhakikisha anaweka kwenye kifaa cha kutunza ubaridi na akifika anapokwenda ni lazima akumbuke kuweka kwenye sakafu sehemu ya mlango.
Kwa wagonjwa ambao hawana jokofu, wanaweza kuhifadhi sindano zao kwenye mtungi wenye maji au kwenye kopo la bati lenye maji.
Kabla mgonjwa hajachoma insulin, ni lazima aoshe mikono kwa sabuni na maji na kuhakikisha mikono imekuwa safi. Angalia lebo ya chupa ya insulin, ili kuhakikisha ni dawa sahihi. Pia hakikisha muda wake wa matumizi haujaisha. Kabla mgonjwa hajachoma insulin, anatakiwa kufuta sehemu anayochoma kwa kutumia spirit.
Mgonjwa anayetumia sindano za insulin anaweza kupata madhara au athari za kawaida kama tatizo la sukari kushuka sana, hasa wakati wa usiku, hivyo mgonjwa anatakiwa asikae muda mrefu bila kula, lakini pia anatakiwa kupima sukari kabla ya kwenda kulala, kama itakuwa ipo chini ya 5 ni lazima ale chakula au matunda, ili sukari isishuke akiwa katika usingizi.
Hypoglycemia ni athari nyingine ya kuchukua sindano za insulin. Insulin nyingi mwilini hupunguza shinikizo la damu. Hii inasababisha maumivu ya kichwa, kusinzia, udhaifu na kasi ya moyo. Kadiri sukari ya damu inavyopungua, jasho, kichefuchefu au kupumua haraka pia kunaweza kuonekana. Mgonjwa anayetumia insulin anatakiwa kupata elimu na maelezo kutoka kwa daktari ili kuepuka athari au madhara madogo madogo yanayoletwa na sindano hizo. Mgonjwa hatakiwi kuacha kutumia sindano mpaka daktari amshauri vinginevyo.