Mchafuko wa damu, tatizo linalowaathiri wengi bila kujua

Muktasari:

  • WHO yasema vimelea vinavyosababisha maambukizi vimejenga usugu wa dawa kwa zaidi ya asilimia 50

Wakati kukiwa na ongezeko la wagonjwa wanaopimwa maabara na kukutwa na maambukizi kwenye damu ‘blood infection’, wataalamu wa afya wametaja hatari iliyopo kimatibabu wakitaka kuwepo kwa usimamizi wa sheria kupambana na changamoto hiyo.

Vituo vya afya vimetakiwa kuhakikisha vinawapima wagonjwa wanaobainika na tatizo hilo kubaini ugonjwa gani wanaumwa kabla ya kuwapatia dawa za antibaotiki, ili kudhibiti tatizo la usugu wa vimelea vya bakteria dhidi ya dawa hizo linalokua kwa kasi.

Sayansi inaeleza kuwa maambukizi kwenye damu si ugonjwa, bali ni matokeo ya ugonjwa uliopo mwilini.

Umewahi kujiuliza, unahisi homa hasa kupanda kwa joto kuliko kawaida, lakini ukifanyiwa vipimo majibu huonyesha hakuna tatizo, mara nyingi majibu ya daktari husema una mchafuko wa damu?

Hata hivyo, dawa zinazosaidia kutibu tatizo hilo, zimeelezwa kuanza kujenga usugu, hali hiyo inadaiwa kusababishwa na matumizi holela ya dawa kwa binadamu na mazao ya mimea pamoja na mifugo.

Utafiti uliofanyika nchini mwaka 2018 ulionyesha asilimia 90 ya wafugaji wanatumia dawa za antibiotiki kutibu wanyama badala ya chanjo, hivyo kusababisha ongezeko la usugu wa vimelea dhidi ya dawa hizo.

Desemba 9 mwaka jana, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilichapisha utafiti mpya uliofanyika nchi 87 ulioonyesha vimelea vinavyosababisha maambukizi kwenye damu vimejenga usugu wa dawa kwa zaidi ya asilimia 50, hali inayohatarisha maisha ya wagonjwa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus alisema usugu wa dawa katika kutibu magonjwa ni jambo hatari ambalo ni muhimu lidhibitiwe, tafiti nyingi zifanyike na mikakati ya kudhibiti inahitajika haraka.

Alitaja vimelea ambavyo usugu wake umeongezeka ni pamoja na vile vinavyosababisha magonjwa kama nimonia, maambukizi katika njia ya mkojo, kisonono, kaswende na vingine vingi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mtaalamu wa magonjwa ya maambukizi kutoka hospitali ya Aga Khan, Samina Somji alisema tatizo la maambukizi kwenye damu na usugu wa dawa katika matibabu yake linazidi kukua duniani kote.

“Usugu wa dawa unaweza kusababisha maambukizi katika mfumo wa damu unaotishia maisha (pia huitwa Sepsis) unaweza pia kusababisha upinzani dhidi ya matibabu ya maambukizi kadhaa ya bakteria,” alisema.

Dk Samina alisema takribani watu milioni 50 waliopata maambukizi ya damu yakawa sugu kutibika wameripotiwa duniani, “kwa hiyo unaweza kufikiria ukubwa wa tatizo hili.”

Dk Samina alisema usugu wa dawa umekuwa suala la kidunia linaloathiri watu milioni 2.8 kila mwaka.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elisha Osati alisema tatizo la maambukizi kwenye damu linaloambatana na kutoa dawa bila uchunguzi zaidi linaongeza uwezekano wa kusababisha usugu wa vimelea katika dawa zinazotumika.

“Matumizi ya mara kwa mara bila kupima yanasababisha wadudu kubadilika na kujitengenezea kinga dhidi ya dawa kwa kubadilisha DNA au protini zake, kwa hiyo dawa zikija ambazo zilitengenezwa kiwandani kwa ajili ya kupambana na ugonjwa husika zinakutana na kirusi ambacho tayari kimejibadilisha, hazitibu,” alisema.

Dk Osati alitolea mfano wa Taasisi ya Utafiti Kenya (Kemri) iliyotoa ripoti mapema wiki hii kuhusu aina nyingine ya ugonjwa wa kisonono na magonjwa ya zinaa ambayo yamekuwa sugu na yanakwepa dawa tunazozitumia kila siku.

“Vita vya tatu vya dunia itakuwa ni usugu wa antibaotiki. Hasara kubwa, ukishapata usugu kwa dawa tulizonazo kutengeneza mpya dhidi ya wadudu wakibadilika ni gharama kubwa, ndiyo maana utaona sasa kuna dawa zimetoka, lakini ni ghali tunashindwa kuzinunua tunaendelea kununua dawa zile zilizokuwepo,” alisema.

Alisema ni vema wagonjwa wakifika vituo vya afya wakiwa na dalili za homa au maambukizi kwenye damu wakapimwe ili kubaini ugonjwa husika.


Usimamizi wa sheria

Kutokana na baadhi ya watumishi kutopenda kutumia huduma za maabara imesababisha wagonjwa wengi kutibiwa kwa dawa za antibaotiki, ikiwa ni matumizi yasiyo rasmi, bila kupata uhakiki wa majibu kutoka maabara hivyo kuongezeka kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa mwaka hadi mwaka.

Wataalamu wa afya walishauri usugu wa dawa usiangaliwe upande wa afya pekee, kwani zinaingiliana kwenye kilimo na mifugo. Watu waache kutumia dawa zaidi ya kiwango kama mbolea na kutumia dawa nyingi kwenye mazao ya kuku, ng’ombe na mbuzi.

Rais wa PST, Fadhili Hezekiah alisema lazima kuwe na usimamizi wa sheria kwa dawa zinazoathirika na usugu wa vimelea zijulikane na kufuatiliwa, kwa kuwa sasa ukiuliza antibaotiki ngapi zinaingia nchini na zinatoka kwa cheti hilo jawabu haliwezi kupatikana.

“Dawa hizi ambazo tunaziita zinaathirika na usugu wa vimelea ni dawa za cheti, tuhakikishe dawa hizi zinapatikana kwa cheti tu, hivyo tutadhibiti usugu. Wafamasia wasimamiwe vizuri kwa kufuatiliwa kwa hakika ili kuziuza kwa kuzingatia sheria,” alisema.

Alisema pale ambapo ni lazima dawa kutumika, zitumike kwa viwango na njia stahiki.

“Muda uliowekwa toka matumizi ya dawa na matumizi ya bidhaa husika uzingatiwe, ili kuruhusu dawa husika kuisha kutoka kwa mnyama au mmea na ikiwezekana kupungua kufika kiwango kinachokubalika,” alisema.

Hezekiah alisema hatua kali zichukuliwe kwa wanaokiuka taratibu na umma uelimishwe kuhusu hatari ya matumizi holela au kupindukia ya dawa.


Maambukizi kwenye damu

Akizungumzia ukubwa wa tatizo, Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Stella Rwezaula alisema maambukizi hayo yapo kwa kiwango kikubwa, ila watu wengi wanashindwa kufanya tafsiri ya majibu ya damu.

Daktari wa magonjwa ya damu kutoka Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila, Flora Ndoboh alisema: “Tunachopima kwenye damu huwa ni mwitikio wa kuongezeka kwa seli nyeupe na hizi huwa zinaongezeka, ikiwa kuna maambukizi kwenye kifua, mfumo wa mkojo yaani UTI au magonjwa mengine. “Na hii huwa inatokea ikiwa vipimo vingine vimeshindwa kubaini, kwa hiyo kipimo kikubwa cha damu kinasaidia kutambua mabadiliko ya chembe nyeupe za damu kuongezeka,” alisema Dk Ndoboh.

Rais mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji, Dk Mugisha Nkoronko alisema kwenye mfumo wa damu maradhi ya maambukizi yapo ya aina nyingi.

Alitaja vyanzo vya maradhi ya vimelea hivyo husababishwa katika magonjwa ya virusi kama Uviko-19, homa ya ini, virusi vya Ukimwi na maambukizi ya mfumo wa matumbo kama wadudu wa protozoa, amoeba, amiba na magonjwa ya mfumo wa mkojo.

Alisema maambukizi mengine kutoka katika vimelea vingine vipo kwenye makundi mbalimbali, ikiwemo magonjwa ya ngono na yamekuwa yakijulikana baada ya vipimo.

“Wakati mwingine mwili unapokuwa umepata maambukizi ya aina yoyote tunapima kwa njia ya damu, hii itakuonyesha juu ya mwili wako ulivyo katika ile damu, hapo ndipo mtu anaambiwa ana ‘blood infection’.

“Ukipata aina ya bakteria kuna chembechembe nyeupe zitaongezeka, unatuma wingi wa seli nyeupe zitakazoonyesha kuongezeka kubaini kwamba sehemu fulani ya mwili kuna maambukizi ya bakteria,” alisema.

Alisema wingi wa chembechembe hizo unaangaliwa mpaka asilimia 11, mtu akiwa na maambukizi asilimia huongezeka mpaka kufikia 17 hadi 20, ina maana kuna maambukizi sehemu fulani hata kama vipimo vingine vimeshindwa kubaini kwenye mwili seli nyeupe katika damu zinaonyesha.

“Huenda maambukizi hayo yaliingilia kwenye njia ya mkojo na kwa bahati mbaya yakapita mpaka kwenye damu, mengine yalipitia kwenye chakula yakapenya na kuingia katika damu na hapo ndipo mchafuko wa damu au blood infection inapotokea,” alisema.


Usugu wa dawa

“Usugu wa dawa umeongezeka kutokana na wagonjwa kununua dawa wanavyotaka na kumeza bila ushauri wa daktari na ukiangalia utafiti mpya wa WHO unaonyesha usugu wa vimelea vya maambukizi umeongezeka zaidi baada ya ujio wa Uviko-19.

“Watu walidhani kila homa ni Uviko-19, sasa hivi tunafahamu si kila homa ni malaria, inaweza kuwa magonjwa mengine,” alisema Dk Nkoronko.

Alisisitiza kuwa ikiwa mtu atatumia dawa bila kukamilisha dozi au mpangilio wa saa unaotakiwa hutengeneza usugu.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni mifumo ya afya ya nchi, kwani wengi wamekuwa wakiugua lakini hawana tabia ya kwenda hospitali.

“Kwanza ataenda kwenye duka la dawa, akienda mara kadhaa na hajapata nafuu anakuja hospitali tayari ameshapata usugu na mbaya zaidi dawa hizi nyingi zimetengenezwa zamani na hatuna dawa mpya, tulizo nazo tuzitumie vizuri ili tusipate usugu,” alisema Dk Nkoronko.

Akielezea jinsi ya kukabiliana na usugu wa dawa za antibaotiki, Dk Samina alisema wataalamu wanatakiwa kufuata miongozo ya utoaji dawa ili kuzuia ukinzani usio wa lazima wa usugu wa dawa na kujua kwa undani tatizo la maambukizi kwenye damu.


Kauli ya Serikali

Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daud Msasi alisema asilimia 80 ya watu wamekuwa hawaponi magonjwa wanapotumia dawa za antibaotiki.

“Tuna dawa ambazo zimejenga usugu, penicillin hatuitumii sana kwa sababu tunaona kati ya watu 100, asilimia 80 hivi hawaponi. Kwa hiyo watu 20 ndio wanapona hivyo tumeiondoa ingawa kuna maeneo inaweza kutumika kutegemeana na mazingira,” alisema. Msasi alisema kutokana usugu wa dawa, Serikali imekuwa ikifanya utafiti na kusoma tafiti na kisha kuhuisha miongozo ya matibabu kila baada ya miaka mitatu ama chini ya muda huo endapo kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.

Matumizi yasiyo rasmi ya antibaotiki yanayodaiwa husababisha usugu wa vimelea kuongezeka nchini yalikuwa asilimia 39, mwaka 2002 asilimia 42, 2014 asilimia 67.7 na mwaka 2017 hadi 2022 wastani wa asilimia 65.

Matokeo ya tafiti iliyofanyika mwaka 2017 yalionyesha asilimia 92 ya wagonjwa hupata matibabu yao katika maduka ya dawa na kati yao asilimia 92.3 hununua antibiotiki holela bila kutumia cheti cha dawa kilichoidhinishwa na daktari.