Mchengerwa atoa mwongozo utoshelevu wa dawa, chanjo, vifaa tiba
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, akitembelea mabanda ya maonesho ya tafiti na ubunifu wa afya kabla ya kufungua rasmi Kongamano la 33 la Kisayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), linalofanyika jijini Arusha.
Muktasari:
- Serikali ya Tanzania inaendelea kutumia fedha nyingi kuagiza dawa, chanjo na vifaa tiba wakati ina rasilimali, wataalamu na mazingira yanayoweza kuiwezesha kuzalisha bidhaa hizo kwa matumizi ya ndani na hata kuuza katika masoko ya Afrika.
Arusha. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amewataka watafiti na wadau wa sekta ya afya nchini kuweka mikakati madhubuti itakayoiwezesha Tanzania kujitosheleza kwa dawa, chanjo na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Amesema Serikali inaendelea kutumia fedha nyingi kuagiza dawa, chanjo na vifaa tiba wakati Tanzania ina rasilimali, wataalamu na mazingira yanayoweza kuwezesha kuzalisha bidhaa hizo kwa matumizi ya ndani na hata kuuza katika masoko ya Afrika.
Mchengerwa amesema mwelekeo huo umechochewa na changamoto za kiafya, kiuchumi na kisiasa zinazoikumba dunia na kuathiri upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hali inayolazimisha Tanzania kuwekeza zaidi katika tafiti za afya na teknolojia za matibabu.
Waziri huyo ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 9, 2026 wakati akifungua Kongamano la 33 la Kisayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) jijini Arusha.
Amesema Tanzania inapaswa kufanya uamuzi mkubwa wa kimkakati ili kujijenga kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa, chanjo, vifaa tiba na teknolojia za afya, kwa lengo la kujitosheleza na kuhudumia pia masoko ya Bara la Afrika.
“Tukatae utegemezi huu ambao umeifanya nchi kuagiza sehemu kubwa ya dawa na vifaa tiba kutoka nje. Natamani ndani ya miaka mitatu ijayo tuwe tunajitosheleza kwa angalau asilimia 50 ya dawa, chanjo na vifaa tiba tunavyotumia,” amesema waziri huyo.
Amesema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika ajenda ya kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba. na sasa inahitaji ushirikiano wa watafiti, sekta binafsi na wadau wengine ili kufanikisha lengo hilo.
“Haina maana kuendelea kuagiza hata dawa za kawaida kama panadol kwa miongo mingi bila kuwa na mkakati wa kuzizalisha hapa nchini. Lazima tujenge uwezo wa ndani na kuimarisha viwanda vya dawa kwa mustakabali wa taifa letu,” amesema.
Waziri Mchengerwa amesema Serikali inatarajia kuandaa waraka maalumu utakaowataka waagizaji wa dawa na vifaa tiba kuwasilisha mipango ya uwekezaji katika uzalishaji wa ndani kama sehemu ya masharti ya kupata leseni za biashara hiyo.
“Tutamtaka kila muagizaji wa dawa atuonyeshe mpango wake wa kuzalisha hapa nchini ndani ya miaka mitatu. Kama hana mpango huo, tutatafakari nafasi yake katika mkakati wetu wa muda mrefu kwa sababu taifa linahitaji wazalishaji zaidi kuliko madalali,” amesema.
Hivyo, amesisitiza kuwa utafiti wa dawa na teknolojia za tiba si anasa bali ni hitaji muhimu kwa taifa linalotaka kujenga uchumi imara na wananchi wenye afya bora.
“Hatuwezi kufikia azma ya kujenga uchumi wa dola trilioni moja bila kuwa na wananchi wenye afya bora. Kama tunataka kufikia Dira ya Maendeleo ya 2050, lazima tuwekeze katika tafiti na kutumia matokeo yake kufanya maamuzi sahihi,” amesema.
Ametoa wito wa kupigwa vita kwa vitendo vya rushwa na udalali katika sekta ya afya, akisema maendeleo ya viwanda vya dawa na vifaa tiba yanahitaji uwazi, uwajibikaji na uzalendo.
Aidha, ameitaka NIMR kuimarisha uhusiano kati ya tafiti, viwanda na uchumi ili matokeo ya tafiti yaweze kufika sokoni, kuzalisha ajira, fursa za biashara na kutoa suluhisho kwa changamoto za wananchi.
Hivyo, amehimiza ushirikiano kati ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta binafsi ili kuharakisha ubunifu na maendeleo ya teknolojia za afya nchini.
Katika hatua nyingine, waziri huyo amewataka watafiti kuongeza juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu la malaria, ugonjwa ambao bado unaendelea kusababisha vifo vya wajawazito na watoto hali inayoathiri maendeleo ya jamii.
“Tunapaswa kujiwekea malengo ya wazi. Kama mataifa mengine yamefanikiwa kudhibiti au kutokomeza malaria, kwa nini sisi tushindwe? Tuwe na mkakati wa miaka 10 wenye malengo yanayopimika,” amesema.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Said Aboud alisema kongamano hilo limewakutanisha washiriki 450 wakiwamo watafiti, watunga sera, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Huduma za Afya kwa Wote: Kujenga Mfumo Madhubuti na Endelevu wa Afya kwa Tanzania ya 2050,” inayolenga kuhimiza matumizi ya ushahidi wa kisayansi katika kupanga na kutekeleza sera za afya.
Kwa mujibu wa profesa huyo, jumla ya mawasilisho 339 ya kisayansi yatajadiliwa katika kongamano hilo.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la NIMR, Profesa James Mdoe amesema changamoto kubwa inayokabili utafiti nchini ni utegemezi wa ufadhili wa nje na ameiomba Serikali kuongeza uwekezaji katika rasilimali za ndani ili kufadhili tafiti zinazoweza kuleta manufaa kwa taifa.