Mimba zilizoharibika zinavyogharimu mabilioni

Naibu Spika wa Bunge, Tulia Ackson (katikati) akizindua ripoti ya utafiti wa gharama zinazotumiwa katika mfumo wa afya kutibu wanawake walioharibikiwa mimba. Picha na Elizabeth Edward

Muktasari:

Tanzania inatumia Sh10.4 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kugharimia matibabu kwa wanawake walioharibikiwa au kuharibu mimba (PAC).

Tanzania inatumia Sh10.4 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kugharimia matibabu kwa wanawake walioharibikiwa au kuharibu mimba (PAC).

Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Guttmacher ya Marekani kwa kushirikiana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas).

Fedha hizo zilitumika mwaka 2018 kuwahudumia wanawake 77,814 waliopatiwa matibabu hayo ili kunusuru maisha yao baada ya kuharibikiwa au kuharibu mimba, huku wengine 114,272 wenye uhitaji wa matibabu hayo wakiyakosa kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa utafiti huo, fedha hizo zilitumika kwa sababu baadhi ya waathirika walishindwa kumudu gharama za matibabu, huduma za matibabu baada ya kuharibika mimba kutopatikana katika maeneo yote, hasa vijijini, hofu ya kubainika amebeba ujauzito na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya huduma hizo.

Kiwango cha kitaifa cha utoaji mimba nchini ni wanawake 36 kwa kila wanawake 1,000 walio kwenye umri wa uzazi wa kati ya miaka 15 hadi 49.

Utafiti huo unaeleza kuwa, kiasi hicho cha fedha kinaweza kufikia Sh25.7 bilioni kwa mwaka endapo matibabu hayo yatawafikia wanawake wote wenye uhitaji.

Watafiti hao waligundua kuwa, utoaji mimba kwa siri hutokea mara nyingi na huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye vifo na kuumia kwa wajawazito.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri wa Muhas, Dk George Ruhago anasema kukabiliana na gharama hizo ni muhimu kama nguvu kubwa ikiwekezwa kwenye elimu na huduma za uzazi wa mpango ili kuepusha mimba zisizotarajiwa.

“Utoaji wa mimba hauruhusiwi kisheria isipokuwa pale inapolazimika kuokoa uhai wa mama, lakini ukweli ni kwamba utoaji mimba upo na kutokana na vitendo hivi kufanyika kwa siri wengi huishia kwenye utoaji mimba usio salama,” anasema Dk Ruhago.

“Wengi huishia kujaribu njia mbalimbali za kutoa mimba na pale wanaposhindwa kutekeleza azma yao na kuwa katika hatari ya kupoteza maisha ndipo hukimbilia hospitali kwa ajili ya kupata msaada wa matibabu.”

Dk Ruhago anasema hali hiyo inathibitisha kuwa inahitajika nguvu kubwa katika elimu ya kujiepusha na mimba zisizotarajiwa ili kupunguza idadi ya mimba zinazoharibiwa na madhara yanayoambatana na vitendo hivyo.

Nini kifanyike

Watafiti wamependekeza kuimarisha juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa huduma baada ya kuharibika kwa mimba, ambayo kwa sasa inapatikana bila ulinganifu katika maeneo mbalimbali.

Dk Progestine Muganyizi ambaye ni mmoja wa washiriki kwenye utafiti huo anasema ili huduma hizo kuwafikia wahitaji wengi ni muhimu kwa vituo vya afya katika ngazi zote viwe na dawa muhimu za kutosha.

“Vifaa vya kutolea huduma za msingi za baada ya kuharibika kwa mimba, na watoa huduma wa kawaida wanapaswa wapewe mafunzo ya kutoa huduma hizo.Ni muhimu kufanyika uwekezaji katika kufanya huduma baada ya kuharibika kwa mimba inapatikana katika ngazi zote za mfumo wa afya,

Kupunguza utoaji mimba usio salama na vifo vya wajawazito na majeraha yanayohusishwa na utoaji mimba, utahitaji kupanua upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango ili kuzuia mimba zisizotarajiwa, na kupanua upatikanaji wa huduma za baada ya kuharibika kwa mimba.

Kwa upande wake Rubago anasisitiza umuhimu wa kujumuisha utoaji wa huduma za uzazi wa mpango kama sehemu ya huduma baada ya kuharibika kwa mimba na kuhimiza kwamba kila mwanamke anayetibiwa kutokana na matatizo yanayohusiana na kutoka kwa mimba apewe ushauri wa kina na nyenzo za uzazi wa mpango.

Kuhusu kuzuia mimba zisizotarajiwa Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake Living Colman anasema njia za uzazi wa mpango zinaweza kuwa suluhu za mimba zisizotarajiwa.

Baadhi ya njia hizo ni matumizi ya vidonge, sindano na vipandikizi vya kuzuia ujauzito. Kitaalam dawa na vizuizi hivi vinazuia mayai kuzalishwa, hivyo kufanya mimba isitungwe.

“Serikali inaweza kuwekeza katika utoaji wa elimu ya uzazi wa mpango, watu wakafundishwa kwa kina kuhusu njia hizi na namna ya kuzitumia ili kila mmoja aamue kufanya uchaguzi wa njia ambayo itamuepusha kupata mimba isiyotarajiwa,” anasema Dk Colman.

Akiwakilisha bunge wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Naibu Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson alitaka utafiti zaidi kufanyika kubaini gharama ambazo zinatokana na kupoteza muda wa matibabu kwa mtu aliyeharibu au kuharibikiwa mimba.

“Natamani utafiti ungegusia pia muda ambao mtu anapoteza kwenye matibabu, zile zote ni gharama huenda zote hizi zikijumuishwa kwenye elimu watu wanaweza kuelewa ukubwa wa tatizo hili na lina athari gani kwake kiafya na kiuchumi wake binafsi na taifa kwa ujumla,” anasema Dk Tulia.

Takriban watoto 60,000 huzaliwa kabla ya wakati kila mwaka nchini Uingereza.

Nchini Uingereza, inakadiriwa kuwa mimba 1 kati ya 4 huishia kwa kuharibika wakati wa ujauzito au kujifungua.

Takwimu muhimu kuhusu ujauzito na kupoteza nchini Uingereza

Kwa mwaka 2019 peee takriban watoto 60,000 walizaliwa kabla ya wakati.

Inakadiriwa kuwa mimba moja kati ya tano ilitoka kwa na mimba moja kati ya nane ilitoka kwa kesi za kuharibika kwa mimba zilizoripotiwa nchini humo mwaka 2019 pekee.

Makadirio yanaonyesha kuwa kuna mimba 250,000 zinazoharibika kila mwaka nchini Uingereza, na karibu watu 11,000 waliolazwa kwa dharura kwa mimba zinazotoka nje ya kizazi.

Mwaka 2019 kulikuwa na vifo vya watoto wachanga 2,131, nchini humo, huku mwaka 2018 wanawake 114 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na afya ya akili wakati au hadi mwaka mmoja baada ya ujauzito kutokana na kuharibika mimba nchini Uingereza na Ireland.

Wanawake 209 walifariki wakati au hadi wiki sita baada ya ujauzito kati ya 2015 hadi 2017 , hii ni sawa na wanawake 9.2 kati ya 100,000 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na ujauzito wakati wa ujauzito au mara tu baada ya hapo.