Anko Zumo: Alivyoiingiza familia yake kwenye uigizaji

Anko Zumo (kushoto), akiwa na mkewe Habiba Zumo pamoja na mwanaye maisala Zumo, maarufu Mai. Picha na mtandao
"Alitakiwa mwigizaji wa kike, wakati huo hatuna pesa ya kumlipa, ili kupata urahisi nikamwambia mke wangu, mama Mai kuna moja, mbili, tatu, unaweza?,anaanza kuelezea Anko Zumo namna alivyoiingiza familia yake kwenye uigizaji.
Familia ya Anko Zumo ambaye jina lake halisi ni Mohammed Omary, wote wanaigiza, kuanzia baba, mama na watoto wao wanne, ingawa 'binti yake wa tatu kuzaliwa Maisala (Mai Zumo) ndiye amekuwa maarufu zaidi.
Anasema alipokuwa anaoana na Habiba (mama Mai) , hakuna aliyekuwa anaigiza kwenye familia yake, hadi mwaka 2015 aliposhauriwa na rafiki yake, Oscar Martin waanze kuchekesha.
"Oscar nilikutana naye Mikocheni, alikuwa anakatisha tiketi za maegesho ya magari, mimi nilikuwa dereva. Siku hiyo nilimpeleka mama kazini, nikawa napiga stori na madereva wenzangu wakawa wanacheka sana stoey nilizokuwa nawasimulia na vituko hivi na vile.
"Akaniambia, Mohammed una kipaji cha kuchekesha, kwa nini tusifanye hivyo Instagram? Wakati huo hata sijui Instagram ni kitu gani, akaniambia nitakuelekeza.
"Tukaanza kujirekodi video fupifupi na kuziweka Instagram hadi 2017, akanishauri na mimi nifungue akaunti yangumuda wote huo alikuwa akiniita Anko, hivyo hata nilipofungua akaunti yangu nikatumia jina la Anko Zumo na kuanza kuweka video fupi za kuchekesha ambazo tulifanya na Oscar,”anasema.
Alivyomuingiza mkewe kwenye uigizaji
Anko Zumo anasema, yeye na Oscar katika kuchekesha, walihitaji mwanamke mmoja ili kuongeza ladha tofauti katika maigizo yao.
"Wakati ule hata sisi tulikuwa hatulipani hatukuwa na pesa, hivyo nikamwambia ngoja nizungumze na mke wangu Habiba kama ataweza aingie tushirikiane, akanijibu sawa.
"Kipindi hicho, Habiba (mkewe au mama Mai) alikuwa na uzoefu wa kuigiza shuleni tu katika mahafali wakati akisoma, aliingia kwenye kundi langu na Oscar tukaanza kazi.
"Nakumbuka igizo la kwanza tukiwa naye, tuliigiza kama Oscar ni mpwa wangu, amempa mimba binti ambaye mama yake alikuwa mkali sana.
"Mimi nilikuwa natibu kwa kisomo, walipomleta yule binti ili tusipate shida nikaihamisha ile mimba kutoka kwa binti kuja kwa mwanangu wa kiume, nikawaambia wazazi wa yule binti, nendeni tumechukua wenyewe tumbo letu,"anasema.
Anasema wakati huo walikuwa wakiendelea kuigiza yeye na mkewe na Oscar na kutupia video Instagram, hadi mwaka 2017 ambapo binti yake Maisala (Maizumo) alipochukuliwa kuigiza kwenye tamthilia ya Pazia
"Kabla ya kuombwa aigize kwenye tamthilia ya Kapuni, Mai alituona tukiigiza nyumba, akaanza kulia na yeye akitaka aigize, wakati huo alikuwa na miaka miwili na miezi tisa,"anasema.
Anasema binti yao huyo katika ukuaji wake, alikuwa akikariri vitu, wakalazimika kumpeleka shule akiwa na miaka miwili na miezi mitano.
"Alikuwa akiongea sana, tukaona bora aende shule akakariri nyimbo na masomo, alipofikisha miaka miwili na miezi saba tulikuwa tunafanya mazoezi akalilia, tukampa maneno ya kuzungumza akaweza, basi tukamuingiza kwenye kundi letu," anasema.
Mai zumo halisi
Katika kuigiza, binti huyo anaonekana ni mtoto mwenye majibu ya papo kwa hapo, mengine ya kukera, ingawa baba yake anasema anavyoigiza ni tofauti na maisha yake halisi.
"Mwanzoni tulikuwa tunamwambia maneno ndipo anaigiza, sasa hivi yupo darasa la nne anajua nini afanye hivyo huwa tunamuandikia tunampa kwa kuwa anajua kusoma, hivyo mwenyewe anakuwa na mwongozo wake," anasema.
Wanavyopiga pesa
Anko Zumo ambaye kijana wake wa pili ndiye mpiga picha na video wake kwenye video wanazoweka Instagram, anasema wanapokuwa nyumbani kama familia huwa pia wanaelekezana majukumu ya kazi.
Mbali na kuweka video Instagram, anasema mwaka 2018 mtayarishaji wa tamthilia mbalimbali ikiwamo Jua Kali, Lamata Mwendamseke aliona kazi zao Instagram akavutiwa na uigizaji wa Mai na kuwaomba amshirikishe kwenye tamthilia ya Kapuni.
"Ilikuwa ni tamthilia yake ya kwanza kuigiza, aliigiza kama mtoto wa Jackline Wolper na Gabo, alikuwa mdogo sana wakati ule lakini alifanya vizuri na pale ndipo akafungua na fursa nyingine zaidi,”anasema Zumo akitabasamu.
Anasema baada ya Mai, walimuomba Lamata awe meneja wao, alikubali na wakawa wanaendelea na kazi yao ya kuchekesha Instagram hadi Anko Zumo alipochukuliwa kuigiza tamthilia ya Jua kali.
Anasema tangu ameingia kwenye uigizaji na familia yake hata kipato kimeongezeka. "Awali kwenye kazi niliyokuwa nikifanya kwa mwaka nilikuwa ninaweka akiba Sh500,000 hadi Sh1 milioni, lakini kwenye uigizaji, kupata Sh5 milioni ya muda mfupi ni kitu cha kawaida.
"Nilipokuwa naingia kwenye hii fani, nilisema kitu cha kwanza kununua ni gari, kweli nilifanya hivyo kisha vingine vikafuata, kupitia sanaa pia wanangu wote watatu wana viwanja vyao, isipokuwa huyo mdogo wa mwisho," anasema.
Alikuwa dereva wa mabasi
Kabla ya kuingia kwenye uigizaji, Anko Zumo anasema kazi yake ilikuwa ni ufundi wa magari na udereva tangu mwaka 2003, japo haikumlipa kama sasa.
"Bado sijaacha hii fani, maana ndiyo iliniweka mjini kabla ya kuwa mwigizaji, nimekuwa dereva bodaboda, taksi, kisha daladala, lakini nimeendesha magari ya abiria mkoani. "Niliwahi kuendesha gari la Mwanza kwenda Katoro na kisha Dar es Salaam kwenda Liwale, hii ndiyo kazi niliyojifunza kabla ya kuingia kwenye uigizaji," anasema.
"Nimetoka kwenye kazi ngumu ya magari, imenisaidia kuwa na nidhamu ya pesa, hivyo Mwenyezi Mungu anapokusaidia kuwa sehemu kuna urahisi kidogo wa kupata pesa inabidi upaheshimu na kuwa na matumizi mazuri.
"Kwenye kuigiza baada ya miezi mitatu una uhakika wa kuwa na akiba ya Sh5 milioni , si jambo dogo, hakika ninashukuru sana,"anasema Zumo.
Alikutana na Habiba shuleni
Kabla ya wote kuigiza, Anko Zumo anasema alikutana na mkewe, “Wakati huo mimi ninaishi Da es Salaam, Habiba alikuwa akiishi Saadan Bagamoyo ambako alikuwa akisoma.
"Nilikwenda kijijini ambako pia ni jirani na kwetu, nikamuona kwa mara ya kwanza akiigiza katika mahafali ya kidato cha nne wakati huo alikuwa akisoma kidato cha tatu.
"Nilimuona tu, tukafahamiana, baadaye alipohitimu, Nilikutana naye tena Saadan, tukawa marafiki wa kawaida, ila nikamueleza wazo langu kuwa sitaki tuwe marafiki wa mbali nataka nimuoe.
“Akajua ni masihara kwa sababu nilizungumza kirahisi, ila nilikuwa ninamaanisha, nikapeleka barua ya posa kwao na kuanzia hapo safari ya kuwa pamoja ikaanza,”anasema Zumo huku anacheka.