Namna Tanzania inavyoweza kuendelea kuiwezesha sekta binafsi

Monday April 13 2020
uchumi pix

Na Jasmini Mushi

Inafahamika kuwa Tanzania imekuwa na kipindi imara cha ukuaji wa kiuchumi katika muongo mmoja uliopita.

Hii imesaidia nchi hii kuwa yenye uchumi unaokua kwa kasi zaidi katika eneo la Afrika Mashariki na pia katika Bara la Afrika.

Kulingana na utafiti wa Taasisi ya Legatum ya nchini Uingereza, ukuaji wa uchumi nchini Tanzania umewezekana kutokana na uwekezaji toka serikalini na sekta binafsi. Katika haya Tanzania imekuwa muuzaji mzuri wa mawe ya thamani kama dhahabu.

Mbali na hilo, Tanzania pia imekuwa kitovu cha utalii, jambo ambalo limewezekana kutokana na uhifadhi mzuri wa vivutio. 

Katika kuelekea mbele, uwekezaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi utaendelea ili uweze kuleta tija katika kuchangia kodi, kutengeneza ajira zaidi na ubunifu. Kwa mfano, kwa mujibu wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), sekta binafsi tayari inaajira zaidi ya asilimia sabini ya vijana nchini.

Advertisement

 Maendeleo haya chanya ya sekta binafsi nchini Tanzania ndiyo yanaleta matumaini ya ukuaji siku za usoni. Hata hivyo bado yako mambo ambayo lazima kuyafanya ili sekta hii ikue na kuzaa matunda zaidi.

Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), namna moja ambayo Tanzania inaweza kukuza zaidi sekta binafsi ni kuboresha mfumo wake wa kodi.

Maeneo mengine ya uboreshaji ni kurahisisha mazingira ya kupata vibali vya kufanya kazi nchini pamoja na biashara kwa wawekezaji ambao wanakusudia kufanya hivyo hasa wale wenye ujuzi ama utaalamu usio rahisi kupatikana hapa nchini.

Katika maeneo mengine, taarifa ya Benki ya Dunia inaonesha namna mbalimbali ambazo sekta ya teknolojia inaweza kukuza sekta binafsi nchini.

 Kwa kusisitiza uwekezaji katika teknolojia, biashara ndogo na za kati zinaweza kutanua wigo na kufikia wateja wengi zaidi.

Vivyo hivyo, sekta ya utalii inaweza kunufaika kwa kuweza kufikia wateja wengi zaidi kwa njia ya matangazo ya mtandao na wepesi wa kufanya malipo.

Tukielekea mwishoni mwa mwaka 2020, inatia moyo kuona sekta binafsi imeendelea kukua. Tuendelee kuiunga mkono na kuiwekea msingi imara zaidi kwa maendeleo ya sasa na siku zijazo.

Advertisement