Desmond Tutu aacha funzo kwa watawala, viongozi wa dini

Muktasari:

Juni 11, 2010, katika Uwanja wa FNB maarufu “Soccer City”, kulikuwa na ufunguzi wa Kombe la Dunia. Siku hiyo, Desmond Mpilo Tutu alikuwa kwenye kiwango bora cha furaha. Kwa Kiingereza unaweza kusema “he was in a good mood” au “in the best mood”.

Juni 11, 2010, katika Uwanja wa FNB maarufu “Soccer City”, kulikuwa na ufunguzi wa Kombe la Dunia. Siku hiyo, Desmond Mpilo Tutu alikuwa kwenye kiwango bora cha furaha. Kwa Kiingereza unaweza kusema “he was in a good mood” au “in the best mood”.

Tutu alikuwa amebakiza miezi minne ili atimize umri wa miaka 79, ungemwona akicheza muziki wa Kwaito, ambao ni mahadhi ya watoto wa mjini, Soweto, Johannesburg kuanzia miaka ya 1990, ungefurahi.

Uwanja wa Soccer City, Johannesburg, ukalipuka shangwe wakati Kundi la TKZee (watoto wa nyumbani) walipodondosha burudani ya wimbo “Shibobo”, ambao wamemshirikisha nyota wa zamani wa soka Afrika Kusini na duniani, Benedict McCarthy.

Basi, Tutu kwa furaha kabisa aliimba na kucheza “Shibobo” ya TKZee. Anafurahia Afrika kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza. Furaha zaidi, nchi yake aliyozaliwa na kuihudumia kwa jasho na damu, Afrika Kusini, ikawa ndio taifa la kwanza Afrika kuandaa fainali za Kombe la Dunia.

Unaweza kudhani ni juzi wanamuziki wakubwa duniani, R Kelly, Shakira, vilevile nyota wachache wateule Afrika, wakiupamba Soccer City kwa muziki mzuri. Tutu akicheza kwa furaha.

Mwili wake ulionesha kuwa na nishati ya kutosha licha ya umri wake. Zingatia, Tutu alifanya kampeni kibwa kuhakikisha Afrika Kusini inaandaa Kombe la Dunia mwaka 2010.

Imeshapita miaka 11. Baada ya hapo zimeshafanyika fainali mbili nyingine za Kombe la Dunia, Brazil mwaka 2014 na Urusi 2018. Na imebaki miezi 11, fainali nyingine zifanyike Qatar. Angalau hizo ni uhakika kuwa Tutu hataziona.

Ilimpendeza Mungu kumchukua Tutu siku ya zawadi (Boxing Day). Maana, alikuwa zawadi kwa taifa lake, Afrika Kusini na dunia. Kila Mwafrika anao wajibu wa kuuhisi mchango wa Tutu ndani ya moyo wake.

Desemba 26, mwaka huu, ikiwa ni saa chache baada ya kuagana na Krismasi ya mwaka 2021, Tutu alikubali wito wa ahadi kuu. Kwamba kila kilichotoka mavumbini, basi kwenye mavumbi kitarejea.

Tutu ameagana na dunia akiwa ameshafanya mengi yenye kumpambanua katika sura na nafasi mbalimbali. Kama mpigania haki za watu weusi na akasimama imara kukataa Waafrika kuitwa weusi. Alitaka mtu mweusi popote pale alipo duniani aitwe Mwafrika. Tutu alipenda Uafrika, na alijivunia rangi yake.

Alikuwa mwalimu, alifundisha vyuo vikuu mbalimbali hasa Afrika Kusini, Lesotho na Botswana. Alibobea katika thiolojia na aliongoza Kanisa la Anglikana kama Askofu wa Johannesburg, kisha Askofu Mkuu wa Cape Town.

Kama alivyopambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, ndivyo alivyopingana na ukandamizwaji wa jamii ya Wazungu baada ya anguko la chama cha kikaburu, National Party (NP), kilichokuwa kinaendekeza sera ya ubaguzi wa rangi.

Tutu alikuwa mpigania usawa ndio maana hakutaka yeyote abaguliwe au kukandamizwa. Alikuwa mkali na mwenye msimamo imara kutetea haki za watu weusi. Na alichora mstari wa usawa kwa weupe baada ya utawala wao kuangushwa kidemokrasia.

Tutu alikuwa binadamu na alipingana na manyanyaso ya kiutu popote yalipokuwa. Aligeuka adui wa Israel alipoona wanawanyanyasa Wapalestina. Aliwageuka makomredi wenzake wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, alipoona wanataka kulipa kisasi kwa Wazungu.

Ndiyo sababu, Tutu akawa mpokea lawama kutoka kila upande. Wazungu walimwona ni mtu mwenye msimamo mkali anapopigania haki za weusi. Jamii za Waafrika zikamzodoa kwamba alikosa uthabiti wa Kiafrika, badala yake akawa anafuata na kutetea matakwa ya Wazungu kuliko Waafrika.

Hata hivyo, lawama hizo zilikuwa mbali mno na kitovu cha ukweli. Mathalan, Rais wa zamani wa Afrika Kusini, enzi za ubaguzi wa rangi, P. W Botha, alipata kumlaumu waziwazi Tutu kwamba alitetea matumizi ya silaha ya wanaharakati wa chama cha African National Congress (ANC) wakati huo.

Tutu alijibu kuwa ingawa haungi mkono matumizi ya silaha na nguvu, lakini yeye anakubaliana na kusudi la kutokomeza ubaguzi wa rangi ambalo ndilo lilikuwa shabaha ya ANC. Kipindi hicho kikiwa chama cha upinzani. Na chama tawala kikiwa NP.

Kuna kesi maarufu ya Sharpeville Six. Chanzo chake ni Septemba 3, 1984. Yalifanyika maandamano kwenye mji wa Sharpeville. Wananchi walirusha mawe kwenye nyumba ya aliyekuwa Naibu Meya wa Sharpeville, Kuzwayo Jacob Dlamini.

Naye, Naibu Meya Dlamini, akachukua bunduki na kurusha risasi kwa waandamanaji. Vurugu zikaongezeka. Waandamanaji wakaendelea kumshambulia Dlamini. Wakamuua.

Desemba 12, 1985, wanaharakati sita, Mojalefa Sefatsa, Theresa Ramashamola, Reid Mokoena, Oupa Diniso, Duma Khumalo na Francis Don Mokhesi, walihukumiwa kunyongwa hadi kufa. Hukumu hiyo ililaaniwa ni watetezi wa binadamu duniani kote.

Tutu, bila woga, aliendesha harakati za ndani ya nchi kupinga hukumu hiyo. Machi 1988, Tutu alifanya mazungumzo na Botha kuhusu kuwaachia watu sita waliohukumiwa kunyongwa katika kesi ya Sharpeville Six. Kikao kilifanyika ndani ya Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini, Tuynhuys.

Kikao hicho hakikumalizika salama. Tutu na Botha walirushiana maneno makali. Tutu akaondoka ofisini hapo akiwa amekasirika mno. Kwa kifupi Tutu hakuwa mwoga. Hakuogopa kuusema ukweli wala kuonesha hisia zake dhidi ya mtawala. Botha pamoja na kuogopwa kwa misimamo yake mikali ya ukandamizaji, alimtambua Tutu.

Ni presha hizo za Tutu pamoja na jumuiya ya kimataifa, zilifanya Botha alegeze msimamo. Watu hao sita wakabadilishiwa adhabu kutoka kifo hadi kifungo cha kati ya miaka 18 na 25.

Kisha, baada ya tamko la Rais Frederik de Klerk, la kuuzika mfumo wa ubaguzi wa rangi, watu hao sita waliachiwa mmoja baada ya mwingine. Diniso na Khumalo waliachiwa Julai 10, 1991, waliofuata ni Ramashamola na Mokoena, Desemba 13, 1991, wa mwisho kutoka wakawa Mokhesi na Sefatsa Septemba 26, 1992.


Mpatanishi, msuluhishi

Tutu alikuwa mpatanishi. Alishiriki vikao vya maridhiano kama sehemu ya upatanishi. Aliteuliwa na Rais Klerk kwenye kamati maalumu ya kujenga mwafaka wa kitaifa. Vikao hivyo ndivyo vilivyofanikisha kuuzika mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Tutu alikuwa mpatanishi wa ghasia za kisiasa zilizoibuka kati ya wafuasi wa vyama vya ANC na Inkhatha Freedom Party (IFP) cha Mangosuthu Buthelezi. Machafuko yalitokea Ulundi, Zululand, Machi 1990. Ilibidi Tutu aahirishe ziara yake nje ya nchi ili kuwakutanisha Buthelezi, Kiongozi wa ANC, Nelson Mandela na Rais Klerk.

Ni kwa sababu hiyo, Mandela alipenda kumwita Tutu kwamba ni “Askofu Mkuu wa Watu”, wakati Klerk alimtambulisha kama jiwe muhimu katika nguzo ya upatanisho, maridhiano na amani Afrika Kusini.

Mwaka 1987, Tutu alitoa hotuba kwenye kongamano la Baraza Kuu la Makanisa Yote Afrika (AACC), Lome, Togo, iliyotajwa kuwa kali mno kwa viongozi wa kiroho Afrika. Mkazo wa hotuba yake ulikuwa kwa kanisa kutojitenga na manyanyaso ya wananchi popote walipo. Tutu alichukia uonevu na unyanyasaji wa binadamu.

Mwaka 1995, Mandela akiwa Rais wa Afrika Kusini, akimtumia Tutu kama kilainishi cha mgogoro wa kisiasa Nigeria. Mandela alimtuma Tutu kwenda Nigeria kukutana na aliyekuwa Kiongozi wa kijeshi, Sani Abacha, kuzungumza naye ili awaachie huru wanasiasa Moshood Abiola na Olusegun Obasanjo.

Tutu ni mshindi wa tuzo nyingi za amani, zikiwemo za Martin Luther King Jr na Nobel. Baada ya kifo chake, viongozi mbalimbali mashuhuri ulimwenguni wametuma salamu za rambirambi.

Malkia Elizabeth II wa UK, amemtaja Tutu kama mtu ambaye hakuchoka kutetea haki za binadamu Afrika Kusini na duniani kote na kwamba kifo chake lazima kiwe na mguso kwa watu wengi kwenye nchi za Jumuiya ya Madola kwa sababu alikuwa na hadhi ya daraja la juu.

Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama alitoa taarifa yenye kueleza kwamba Tutu alikuwa “roho iliyoishi kabla ya ulimwengu”. Kwamba Tutu alikuwa na hisia za kila kilichotokea duniani, ndiyo maana alijitoa kupigania uhuru na haki nchini kwake na ulimwenguni kote.

Rais wa 46 wa Marekani, Joe Biden, katika rambirambi zake kwa kifo cha Tutu, alisema ukuu wa Tutu utadumu kwa vizazi vingi vijavyo. Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby, ameandika: “Ukiwa sehemu za dunia, mahali kwenye uchache wa Waanglikana na watu hawana uhakika kuhusu Kanisa la Anglikana. Itatosha kusema ni Kanisa ambalo Desmond Tutu alihudumia.”

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema kuwa kifo cha Tutu ni ukurasa mwingine wa pigo kwa taifa kwa kuagana na kizazi kilichojitoa kuipigania na kuikomboa Afrika Kusini.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis I, ameomboleza kifo cha Tutu kwa kumtaja kama mpigania usawa wa watu wa rangi zote na maridhiano Afrika Kusini.

Msimamo wa Tutu wa kuunga mkono ndoa za jinsia moja, ulimfanya aingie kwenye kitabu cha mijadala mingi ya uhalali au uharamu wa mitazamo ya kijinsia.

Askofu wa kwanza mweusi Lesotho, Johannesburg na Cape Town. Akiwa Askofu Mkuu wa Cape Town, ndio ulikuwa mwanzo wa wanawake Afrika Kusini kuchipua kama wachungaji wa Kanisa la Anglikana.

Katika maisha yake, Askofu Tutu alipata watoto wanne, wote na mkewe, Nomalizo Leah aliyefunga naye ndoa mwaka 1955. Katika watoto hao, yumo pia Mpho ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Anglikana na amefunga ndoa ya jinsia moja.

Alipostaafu uaskofu mkuu wa Cape Town mwaka 1996, alitunukiwa cheo cha heshima cha Askofu Mkuu Mstaafu. Amefariki dunia kwa maradhi ya kansa. Alipata tezi dume mwaka 1997. Alipokuwa mtoto aliugua polio, alipofikisha umri wa miaka 16, alishambuliwa na kifua kikuu. Hatimaye amepumzika akiwa na umri wa miaka 90 na miezi miwili.