Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pre-Form One na msimu wa shule binafsi ‘kupiga fedha’

Baada ya kumalizika kwa mitihani ya kuhitimu darasa la saba, wazazi kote nchini Tanzania wanapata furaha isiyo kifani kuona watoto wao wamevuka hatua hiyo muhimu katika safari ya elimu.

Picha za pongezi zimejaa kwenye mitandao ya kijamii, zikionesha furaha, matumaini, na fahari ya wazazi wanaojiandaa kupeleka watoto wao kwenye ngazi ya sekondari.

Miaka saba ya elimu ya msingi, ambayo imejaa changamoto za kila aina, sasa imehitimishwa, na familia nyingi zinaamini kuwa ndoto za watoto wao zinaanza kutimia.

Lakini nyuma ya shamrashamra hizo, swali muhimu linajitokeza: je, mipango ikoje kuhakikisha kila mwanafunzi anayehitimu anapata elimu bora kwenye ngazi ya sekondari? Tanzania inajivunia kutoa elimu ya msingi bila malipo, lakini bado shule za binafsi zinaonekana kuvutia wazazi wengi ambao wana shaka kuhusu ubora wa elimu inayotolewa na shule za umma.

Hii inadhihirisha kwamba elimu ya msingi bila malipo haijapata imani kamili kutoka kwa baadhi ya wazazi.

Shule binafsi nchini, hasa zile zinazojulikana kwa kutoa matokeo mazuri kila mwaka, hazina haja ya kujitangaza.

Wazazi wanazikimbilia wenyewe, licha ya gharama kubwa zinazohusishwa kujiunga na shule hizo.

Wakati shule nyingi za binafsi zikihaha kutafuta wanafunzi, shule zilizo na historia nzuri ya matokeo mazuri huchuja wanafunzi kwa umakini na kuweka viwango vya juu vya kujiunga.

Mbinu hii ya mchujo inawakatisha tamaa wazazi wengi, lakini inaonekana kuwa ndiyo njia pekee ya kuhakikisha shule hizi zinaendelea kutoa matokeo bora.

Katika mchakato huu wa kuandikisha wanafunzi wapya kwa kidato cha kwanza, baadhi ya shule binafsi zimeanzisha utaratibu wa Pre-Form One, ambapo wanafunzi hulazimika kusoma masomo ya awali kwa kipindi cha miezi miwili hadi sita kabla ya kuanza kidato cha kwanza rasmi.

 Ingawa utaratibu huu hautambuliki rasmi na Serikali, umeonekana kuwa maarufu katika shule nyingi binafsi.

Wazazi wanaamini kuwa kusoma Pre-Form One ni njia bora ya kumwandaa mwanafunzi kwa masomo ya kidato cha kwanza na hivyo hawasiti kulipia gharama kubwa zinazohusishwa na mpango huu.

Gharama za Pre-Form One zimekuwa changamoto kwa wazazi wengi, kwani ada zinaweza kufikia hadi Sh1 milioni.

Wakati mwingine, shule zinafanya utaratibu huu kuwa wa lazima kwa kila mwanafunzi anayetaka kujiunga.

Wale ambao hawataki kulipa gharama hizo, wanakosa nafasi ya kujiunga na shule hizo. Hii inawafanya wazazi walio na uwezo mdogo wa kifedha kujikuta wakiangalia shule za umma kama chaguo la mwisho, hata kama hawana imani kamili na ubora wa elimu inayotolewa huko.


Kasoro za mpango huu

Mpango wa Pre-Form One hauna mtalaa maalumu unaotambuliwa na Serikali, na masomo yanayofundishwa wakati huu ni yale yale ambayo wanafunzi watakutana nayo kwenye kidato cha kwanza.

Ingawa wazazi wengi hawakubaliani na utaratibu huu, bado wanashurutishwa kuufuata ili watoto wao wapate nafasi katika shule hizo maarufu.

Vilevile, utaratibu huu umeleta changamoto kwa walimu, hasa wale wanaofundisha masomo ya Kiingereza na sayansi.

Walimu hawa wanalazimika kufundisha kipindi cha Pre-Form One wakati ambao wangeweza kupumzika, hasa likizo ya Septemba.

Walimu hawa, ingawa wanabeba mzigo mkubwa wa kuwafundisha wanafunzi hawa, wanalipwa malipo duni, kama chakula cha mchana na nauli pekee.

Kwa upande wa wamiliki wa shule binafsi, mpango wa Pre-Form One umekuwa chanzo cha faida kubwa.

Mmoja wa wamiliki wa shule binafsi nchini, ambaye hakutaka kutajwa jina, alikiri kwamba kupitia mpango huu, shule yake inapata zaidi ya Sh18 milioni kila mwaka.

Fedha hizi hazitumiki zote kwa malipo ya walimu au gharama nyingine za uendeshaji, badala yake zinasaidia kuimarisha miundombinu ya shule na kulipa mishahara ya walimu.

Walimu wanaofundisha wanafunzi wa Pre-Form One wanapewa marupurupu madogo kama chakula cha mchana na nauli, huku wamiliki wa shule wakibaki na sehemu kubwa ya mapato haya.

Soko huria katika sekta ya elimu nchini limeifanya iwe vigumu kwa wazazi kulalamikia taratibu hizi ngumu, hasa kwa kuwa Serikali ina mpango wa kutoa elimu bila malipo kwa shule za umma.

Wazazi wanajikuta wakiwajibika kufuata taratibu hizi ngumu kwa sababu hawana imani na mfumo wa elimu ya umma.


Fursa nyingine kwa shule

Ukiondo mpango wa Pre form One, baadhi ya wazazi wamekuwa wakilalamikia ada kubwa zinazotozwa na shule binafsi kwa ajili ya mitihani ya usaili wa kujiunga na kidato cha kwanza.

Ada hizi zinaanzia Sh25,000 hadi 50,000 kwa mwanafunzi, lakini wazazi wanadai kuwa mitihani hiyo ni migumu mno, hali inayowafanya watoto wengi kushindwa kufaulu.

Mzazi mmoja alieleza kuwa baada ya kumpeleka mtoto wake kufanya usaili katika zaidi ya shule sita za binafsi, hakupata nafasi hata moja.

Mzazi huyo alisema kuwa licha ya mwanawe kufanya vizuri katika shule ya msingi, ameshindwa kufaulu mitihani ya usaili kwa sababu ya ugumu wa maswali.

Wakati huo huo, mzazi huyo alikiri kuwa ameshatumia zaidi ya Sh400,000 kwa ajili ya mitihani hiyo ya usaili, hali inayomweka kwenye sintofahamu kuhusu wapi atampeleka mwanawe kusoma.

“Nimelipia zaidi ya Sh400,000 mwanangu amefanya usaili shule (anazitaja shule hizo), lakini hakupata nafasi nahangaika na siwezi kumpeleka shule ya umma, nawaza niende shule gani, alilalamika mzazi huyo kwa uchungu.

Mmiliki wa shule moja maarufu jijini Arusha anasema kuwa shule yake hukusanya zaidi ya Sh100 milioni kila mwaka kutoka kwenye mauzo ya fomu za usajili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Wazazi wanalazimika kulipia gharama za fomu, na baada ya kufanya usaili, ni wachache sana wanaofaulu. Shule yake inachukua wanafunzi 300 pekee kwa kidato cha kwanza, huku wanafunzi wengine 600 wakishindwa kupata nafasi baada ya usaili.

Mmiliki huyo alikiri kuwa kiasi kikubwa cha fedha zinazokusanywa hutumika kuboresha miundombinu ya shule na kulipa mishahara ya walimu, lakini bado shule inapata faida kubwa.

Wamiliki wa shule binafsi wanasema kuwa gharama za uendeshaji wa shule ni kubwa, na kwa sababu hiyo wanalazimika kuongeza ada na kutoza gharama za usaili ili kufidia gharama hizo. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, alilalamikia mzigo wa kodi unaowakumba wamiliki wa shule binafsi.

 Alisema kuwa serikali inawatoza kodi nyingi, hali inayowafanya wamiliki wa shule kuongeza ada kwa wanafunzi ili kufidia gharama hizo.

Dk. Bagonza alisema kuwa shule nyingi za binafsi zinazomilikiwa na makanisa au taasisi za dini zina lengo la kutoa huduma bora kwa jamii, lakini zinakwamishwa na kodi kubwa zinazotozwa na Serikali.

Kwa ujumla, mfumo wa elimu nchini Tanzania unakabiliwa na changamoto nyingi, hasa kwenye shule za binafsi. Wazazi wanahangaika kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora, huku gharama kubwa na taratibu ngumu za kujiunga na shule hizo zikiwakatisha tamaa.

 Serikali inahitaji kuchukua hatua madhubuti kuboresha elimu ya umma ili iweze kushindana na elimu ya binafsi na kuwapa wanafunzi wote fursa sawa ya kupata elimu bora bila kujali hali yao ya kifedha.